Mo Salah anavyoburuza namba akisugua benchi
Muktasari:
- Salah amekuwa na mwaka mgumu katika kile kinachoweza kuwa msimu wake wa mwisho akiwa mchezaji wa Liverpool, ambapo aligombana na kocha Arne Slot mwishoni mwa mwaka jana nje ya uwanja, na pia akaonekana kupoteza makali yake uwanjani.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL wanaonekana ‘kufika mwisho’ na Mohamed Salah msimu huu, lakini takwimu zake bado zinampita winga wa Arsenal, Bukayo Saka kuonyesha kwamba bado Mmisri huyo yupo vizuri zaidi.
Huenda Mo Salah anapitia msimu mbaya zaidi katika maisha yake ya soka akiwa Liverpool, lakini ana michango mingi zaidi ya mabao kuliko Bukayo Saka, na hilo linaonyesha wazi ubora wake kulingana na wachambuzi wa Inside Liverpool kupitia talkSPORT.
Salah amekuwa na mwaka mgumu katika kile kinachoweza kuwa msimu wake wa mwisho akiwa mchezaji wa Liverpool, ambapo aligombana na kocha Arne Slot mwishoni mwa mwaka jana nje ya uwanja, na pia akaonekana kupoteza makali yake uwanjani.
Hata hivyo, katikati ya wiki hii mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 aliwaonyesha watu kuwa bado ana kitu cha ziada ndani yake alipofunga bao zuri la kipekee na kusaidia Liverpool kubadili matokeo ikiifunga Galatasaray 4-0 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Huo ulikuwa ni wakati maalumu kwa Salah ambao mashabiki wote waliufurahia Anfield, lakini pia watalazimika kufurahia muda uliobaki, kwani inaonekana huenda akaondoka klabuni wakati wa majira ya joto.
Mtangazaji wa Inside Liverpool, Sam Ellard alisema: “Tumemkosoa Salah msimu huu, lakini kumuona mbele ya Kop, usiku wa Ligi ya Mabingwa, na vaibu la mashabiki dhidi yake kilikuwa kitu cha kipekee.”
Shabiki wa Liverpool na bondia wa zamani, Paul Smith aliongeza: “Hasa baada ya kukosa penalti, lakini mashabiki waliendelea kuimba jina lake, uwanja mzima ulikuwa hivyo. Ni wazi anakosa kujiamini, na mchezaji akiwa hivyo, hakuna maana ya kumkosoa kwa maneno hasi.
“Salah ni aina ya mchezaji ambaye hata akiwa na mchezo mbaya anaweza kufunga bao la ajabu. Hilo analo.”
Smith aliendelea: “Nadhani katika michezo mingi unapokaribia mwisho dalili huonekana, na naamini tumeanza kuziona. Nadhani tunakaribia mwisho wake, lakini hilo ni jambo la kawaida kwa wachezaji wa umri wake na waliodumu kwa kiwango cha juu kwa muda mrefu.
Bao lake dhidi ya Galatasaray lilikuwa la 10 msimu huu katika mashindano yote, na kumfanya afikishe jumla ya michango 19 (mabao na asisti), ukijumuisha asisti tisa. Hata hivyo, kwa mchezaji ambaye kwa wastani amekuwa na michango 44 kwa msimu katika miaka minane iliyopita, hiyo ni idadi ndogo.
Salah mbele ya Saka
Wachambuzi wa Inside Liverpool walibainisha kuwa hata akiwa chini ya kiwango chake cha kawaida, Salah bado yuko juu kuliko nyota wengine wa Ligi Kuu England, akiwa na michango mingi kuliko Bukayo Saka wa Arsenal ambaye ana 14 msimu huu, na pia kuliko winga wa Manchester City, Jeremy Doku mwenye 12.
Baada ya kuambiwa takwimu hizo, mchezaji wa zamani wa Liverpool Jermaine Pennant alisema: “Hiyo ni sifa kubwa kwake. Huu ndio msimu wake mbaya zaidi akiwa Liverpool, lakini bado ana takwimu bora kuliko wachezaji wengine wakubwa. Hilo linaonyesha jinsi alivyo mzuri kwa Liverpool.
Amebadilishwa nafasi?
Inaonekana Salah anacheza zaidi katikati kidogo kuliko kawaida, na anafaidika na mabadiliko hayo licha ya muda mfupi wa kuchezeshwa uwanjani.
Kocha Slot alikuwa akimtumia pembeni sana msimu huu, lakini kumuingiza ndani kunaonekana kuleta matokeo mazuri na Pennant anaeleza: “Hivyo ndivyo Salah anavyopenda kucheza. Anapenda kuwa pembeni, lakini pia kucheza karibu na washambuliaji ili kupiga pasi za haraka. Lakini mwanzoni mwa msimu huu tulimuona akiwa karibu na mstari wa pembeni, jambo ambalo lilikuwa gumu kwake kwani hawezi kuwapita wachezaji kirahisi.
“Kadri anavyocheza karibu na lango, ndivyo tunavyoona uwezo wake, na hilo ndilo tuliloliona msimu uliopita. Msimu uliopita hakuwa bora kila mchezo, lakini wakati fulani angeibuka na bao au pasi ya bao.”