Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mke wa Van Persie, AFCON 2025 mule mule!

SHOWBIZ Pict

Muktasari:

  • Akiwa mchezaji mkubwa wa Arsenal na mmoja wa washambuliaji bora kuwahi kutokea katika kizazi chake, ni mashabiki wachache wa soka wasiomjua Mdachi huyo.

GWIJI wa soka kutoka Uholanzi, Robin van Persie, 42, amekuwa katika ndoa kwa miaka mingi na Bouchra, 42, mwenye asili ya Morocco, nchi mwenyeji wa michuano ya Afcon 2025 inayoendelea kwa sasa.

Akiwa mchezaji mkubwa wa Arsenal na mmoja wa washambuliaji bora kuwahi kutokea katika kizazi chake, ni mashabiki wachache wa soka wasiomjua Mdachi huyo.

Hata hivyo, leo tunaweka pembeni mafanikio yake ya soka na kujikita zaidi kwenye maisha ya familia akiwa amemuoa mpenzi wake wa ujanani na uhusiano wao umekuwepo kwa miaka zaidi ya 20.

SHOW 01

Bouchra ni mwanamke mwenye haiba ya kipekee na amekuwa chanzo kikubwa cha nguvu na motisha kwa Van Persie, mwanafainali wa Kombe la Dunia 2010 huko Afrika Kusini.

Wawili hao waliokutana wakiwa bado vijana wadogo, hadithi yao ya mapenzi ilianza nchini Uholanzi, na tangu hapo wamezunguka sehemu nyingi duniani pamoja wakionyesha kuwa ni watu wenye dhamira moja maishani.

Hawajawahi kuweka wazi kama yalikuwa ni mapenzi ya mara ya kwanza (love at first sight), lakini wanakiri wazi kwamba kila mmoja wao alihisi kuvutiwa na mwenzake tangu mwanzo.

Wote wakiwa katika umri wa miaka ya ishirini, ndipo walifunga ndoa hapo Machi 2004, na harusi yao ilikuwa ya faragha kwa kiasi ikihudhuriwa na ndugu wa karibu na marafiki wachache.

SHOW 05

Mnamo Novemba 2004, Bouchra akamzaa mtoto wao wa kwanza wa kiume, Shakeel ambaye sasa naye anacheza soka, na kisha baadaye walibarikiwa kupata mtoto wa kike, Dina aliyezaliwa Oktoba 2009.

Kuwa wazazi kwa mara ya kwanza ni tukio la furaha kubwa, na wanandoa hao walifurahia kila hatua ya safari hiyo na hata sasa kupitia mitandao ya kijamii wameonyesha kuwapenda watoto wao.

Bouchra alizaliwa Oktoba 5, 1983 huko Uholanzi, mama yake anatokea Morocco, hivyo michuano ya Afcon 2025 inayofanyika nchini humo, inamuhusu kwa sehemu kwa sababu ana ndugu zake wengi huko.

SHOW 02

Licha ya kuwa mtu mwenye kupenda kuonekana hadharani na kujitokeza kwenye vyombo vya habari, Bouchra ameweza kuficha kwa mafanikio taarifa nyingi kuhusu familia yake kwa miaka mingi.

Hajawahi kushiriki taarifa zozote kuhusu baba au mama yake lakini kinachojulikana ni kwamba ana asili ya Morocco, mabingwa wa Afcon 1976.

Kwa kifupi bibie anachagua kwa umakini mkubwa aina ya taarifa anazotoa katika vyombo vya habari, na ameweza kulinda sana maisha yake binafsi hadi sasa.

SHOW 04

Lakini inajulikana kuwa yeye ni mpanda farasi (equestrian) mahiri, anapenda sana kupanda farasi na hutumia muda wake mwingi kutunza na kuendesha mazizi ya farasi wake.

Mara nyingi katika ukurasa wake wa Instagram anaposti picha na video za safari zake akiwa amepanda farasi,na hata binti yake Dina anaonekana kufuata nyoyo zake.

Vilevile Bouchra ni mwanamitindo akiwa amefanya kazi na baadhi ya chapa kubwa akionekana kwenye majarida mbalimbali, mojawapo likiwa jarida la Helden.

Ana ushawishi Instagram akiwa na wafuasi zaidi ya 77,000, ni mtu mwenye shughuli nyingi kwenye mtandao huo, ambapo mara nyingi huposti picha akiwa na mume wake na watoto wao, pamoja na picha za farasi wake.

Ikiwa ni miaka 21 tangu Bouchra amefunga ndoa na Van Persie, mtoto wao kwanza, Shakeel tayari yupo katika soka la kulipwa akichezea Feyenoord inayoshiriki Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie).

SHOW 03

Shakeel alianza safari yake ya soka katika akademi ya Manchester City, kuanzia Julai 2015 hadi Juni 2017, alicheza katika akademi ya Fenerbahce, kipindi ambacho baba yake alikuwa akiichezea klabu hiyo ya Uturuki.

Alirejea Uholanzi na kujiunga na Feyenoord, kisha Mei 2022, akasaini mkataba wake wa kwanza wa kulipwa na Feyenoord, mkataba wa miaka mitatu.

Novemba 27, 2025, akacheza mechi ya kwanza timu ya wakubwa chini ya kocha wake ambaye pia ni baba yake, Van Persie, akiingia dakika ya 80 katika mchezo wa Europa ambao walipoteza 3-1 dhidi ya Celtic.

Ikumbukwe Van Persie alianza safari ya soka akiwa mdogo kwenye kikosi cha Excelsior, kisha Feyenoord ambapo alionyesha mapenzi makubwa ya soka na akaanza kuimarisha uwezo wake wa kufunga mabao. 

Mwaka 2004, Arsenal chini ya kocha Arsene Wenger ilimsajili Van Persie ambaye katika kipindi chake cha miaka minane klabuni hapo aling’ara sana kwa kuonyesha kiwango kikubwa.

Hata hivyo, baadaye alihamia kwa wapinzani wao wakubwa, Manchester United, jambo lililowashangaza na kuwakasirisha mashabiki wa Arsenal waliotilia shaka uaminifu wake.

Licha ya hilo, aliendelea kuwatesa washindani wake kwa kiwango bora, na hatimaye Januari 2018 alirejea kwenye klabu yake ya utotoni, Feyenoord akitokea Fenerbahce, kabla ya kustaafu rasmi mwaka uliofuatia.