Mjue farasi aliyesababisha anguko la Man United

Muktasari:
- Kwa tafsiri ya neno kwa neno, Rat Race maana yake ni Mbio za Panya, lakini maana ya jumla ni harakati za mapambano kwenye maisha kwa ajili ya mali na madaraka, na kupelekea watu kuhamaki na kupata kiwewe.
Mwaka 1975 Bob Marley aliimba wimbo wa Rat Race uliokuwemo kwenye albamu ya Rastaman Vibration iliyotoka mwaka mmoja baadaye, 1976.
Kwa tafsiri ya neno kwa neno, Rat Race maana yake ni Mbio za Panya, lakini maana ya jumla ni harakati za mapambano kwenye maisha kwa ajili ya mali na madaraka, na kupelekea watu kuhamaki na kupata kiwewe.
Ndani yake Bob Marley alisema “When you think it’s peace and safety A sudden destruction Collective security for surety, yeah.”
Pale unapodhani kuna amani na usalama, Ghafla (unatokea) uharibifu mkubwa (Unatakiwa) Usalama wa pamoja kwa hakika, yeah.
Hiki ndicho kilichoitokea Manchester United hadi kufikwa na uharibifu mkubwa, wakitoka kwenye amani na utulivu wao wa zamani.
Kuanzia mwaka 1993 hadi 2013, Manchester United ilikuwa kwenye amani na utulivu mkubwa sana wakishinda mataji wanavyotaka .
Baadaye ghafla wakajikuta mambo yameharibika na wengi kulalamikia kustaafu kwa kocha wao Sir Alex Ferguson, mwaka 2013.
Lakini sasa zimeibuka taarifa za kwamba anguko la klabu hiyo siyo kustaafu kwa Sir Alex Ferguson bali RAT RACE kama alivyosema Bob Marley, kwa kuzingatia maana ya jumla ya wimbo huo.
Harakati za mapambano kwenye maisha kwa ajili ya mali na madaraka, na kupelekea watu kuhamaki na kupata kiwewe.
Taarifa rasmi inasema anguko la Manchester United lilianzia mwaka 2002 pale ilipotokea RAT RACE kati ya Sir Alex Ferguson na wenzake watatu.

ILIKUWAJE
Zaidi ya kuwa kocha wa mpira, Sir Alex Ferguson alikuwa shabiki mkubwa wa mbio za farasi na yeye mwenyewe binafsi.
Mwaka 2001, Sir Alex Ferguson aliwekeza hisia za umiliki kwenye farasi mmoja maarufu aliyeitwa Rock of Gibraltar, yaani mwamba wa Gibraltar.
Farasi huyu aliyezaliwa 1999, alikuwa akimilikiwa na bwana John Magnier na mkewe Susan, pamoja na JP MacMamus.
Kwa hiyo Sir Alex Ferguson akawa mmiliki wa tatu, na kutokana na ushawishi wake, farasi huyu akawa anakimbia akivaa rangi za Manchester United.
Rock of Gibraltar akatokea kuwa farasi mwenye mafanikio zaidi mwaka 2002 akishinda mashindano yote aliyoshiriki.
Ghafla ukatokea mgogoro baina ya wamiliki wa farasi huyu, yaani Sirl Alex Ferguson na mtu na mkewe, na MacManus.
Mgogoro huu wa kibiashara ukawa mkubwa kiasi cha kuamuriwa mahakamani baada ya watu hawa kushindwa kuelewana mezani.
Chanzo cha mgogoro ni kwamba wataalamu wa tathmini ya thamani za wanamichezo walimkadiria farasi huyo kuwa na thamani ya pauni za Uingereza, milioni hamsini, na Sir Alex Ferguson akasema yeye hisa zake ni aslimia hamsini ya pesa hizo…hapo ndipo mgogoro ulipoanza.
Hawa jamaa wengine, John Magnier na JP MacManus pia walikuwa wakimiliki asilimia 28 za hisa za Manchester United.
Mgogoro wao ukasababisha wakasirike na kuuza hisa zao zote ndani ya Manchester United.

Kuuza kwa hisa zao kukawaribisha wanafamilia wa Glazer, kuinunua klabu hiyo, biashara iliyokamilika mwaka 2005.
Familia hii ya Glazer ndiyo iliyokuja kuiangusha Manchester United kutokana na sera zao mbaya za uwekezajji klabuni na usimamizi mbaya wa klabu.
Lakini haya yote yasingetokea kama siyo yule farasi aliyewagombanisha Sir Alex Ferguson na wenzake,
FAMILIA YA GLAZER ILIVYOIANGUSHA MANCHESTER UNITED
Joel, Bryan na Avram Glazer walikamilisha manunuzi ya Manchester United, Juni 30, 2005.
Ikiwa imekaribia kufika miaka 20 kamili tangu wainunue klabu hiyo, haya ni makosa yao makubwa yaliyoiangusha Manchester United.
1. MADENI
Manchester United iliuzwa kwa bei ya pauni milioni 790. Familia ya Glazer walitoa pauni milioni 270 taslimu, na kiasi kilichobaki cha pauni milioni 520 kikawa mkopo ambao ulitakiwa kulipwa na klabu.
Angalia hapa, bei ilikuwa pauni milioni 790, wao wakatoa taslimu pauni milioni 270 na na 520 zilizobaki zilipwe na klabu waliyoinunua.

Na hiyo pesa utalipwa mkopo, maana yake ni deni. Kwa hiyo Manchester United chini ya familia ya Glazer ilianza kwa deni la pauni milioni 520.
Kabla ya hapo klabu hiyo haikuwa na deni hata kidogo.
2. UWEKEZAJI
Manchester United iliorodheshwa kwenye soko la hisa la London tangu mwaka 1991 na mara zote ilikuwa ikitoa gawio kwa wana hisa wake kila mwisho wa mwaka huku faida ikirudishwa klabuni kufanya uwekezajji kwa ajili ya maendeleo ya klabu.
Na hii ilimsaidia sana Sir Alex Ferguson kiutawala soko la wachezaji, kama kutoa pauni milioni 27 kumnunua Wayne Rooney akiwa na miaka 18 tu, mwaka 2004.
Kuanzia 1992 hadi 2005, kabla ya ujio wa akina Glazer, Manchester United ilifanikiwa kuutanua uwanja wao wa Old Trafford kutoka kuingiza watu 40,000 hadi 75,000.

Hii yote ilitokana na uwekezajji uliotokana na kurudishwa klabuni kwa faida iliyotokana na faida za biashara za klabu.
Lakini tangu waingie akina Glazer, hiyo haipo tena. Faida zote zimekuwa zikitumika kulipa lile deni la manunuzi ya klabu pamoja na riba.
Uwanja wa Old Trafford umetelekezwa kiasi cha kuvuja maji kutokana na mvua, kama ilivyojidhihirisha msimu uliopita.
3. HASIRA ZA MASHABIKI
Ukienda Ettihad, uwanja wa nyumbani wa Manchester City, kuna bango kubwa la mashabiki linalomshukuru Sheikh Mansour, tajiri wao.
Stamford Bridge, uwanja wa nyumbani wa Chelsea, kulikuwa na bango kubwa sana la kumshukuru Roman Abramovich, lililoandikwa ‘Roman Empire’.
Lakini liliondolewa kwa amri ya serikali baada ya Abramovich kulazimishwa kuiuza klabu hiyo kama sehemu ya vikwazo kwa watu wote waliokuwa karibu na Vladimir Putin baada ya vita vya Ukraine na Urusi.

Hata hivyo, ukienda Old Trafford hukuti mabango ya kumshukuru tajiri yao, bali kumlalamikia .
‘Love United, Hate Glazers’, hilo ni bango kubwa lililopo Old Trafford kente ujumbe mkali dhidi ya tajiri.
Mashabiki wa Manchester United walimkataa mwekezaji wao tangu alipotangazwa kuwa atainunua klabu hiyo.
Kuna wengine walikasirika na kuanzisha klabu yao na kuiita FC United of Manchester, na kusema hawatoenda tena Old Trafford hadi Glazer waondoke.
Timu hiyo kwa sasa iko daraja la saba.
Hasıra za mashabiki wa Manchester United dhidi ya Glazer zilifika kilele chake mwaka 2023 walipovamia uwanja na kusababisha mchezo dhidi ya Liverpool usichezwe, kushinikiza Glazers wawaachie timu yao.
Hayo ndiyo maisha ya Manchester United tangu timu yao iangukie mikononi mwa mabwanyenye wa kimarekani, akina Glazer.
Na hii isiingewezekana kama siyo Rat Race ya Sir Alex Ferguson na wenzake kuhusu farasi wa Rock of Gibraltar.