MJUAJI: Soka lilichezwa mtaa wa Congo

WIKI iliyopita, niliizungumzia Cosmopolitan.  Hii ni timu ambayo mwaka 1967 ilitwaa ubingwa wa Tanzania.

Nilisema timu hii ilitoa wachezaji wengi waliokuwa maarufu baadaye, wapo waliokuja kulitumikia taifa katika nafasi ya ukocha na wengi wao walikuja kuwa wachezaji wakubwa hapa nchini.

Unaujua umaarufu wa Mtaa wa Congo uliopo Kariakoo jijini Dar es Salaam?

Wengi wanaufahamu mtaa huo kwa kuwa enzi na enzi ndio kulikokuwa kukiuzwa nguo kuanzia zile za mitumba hadi za dukani.

Wapo wanaoufahamu mtaa huo kwa kuwa ndio uliokuwa chimbuka la wizi na utapeli wa kila aina.

Kuna nyimbo kadhaa za kuwatahadharisha watu kuibiwa wanapofika Mtaa wa Congo.

Lakini mtaa huo pia ulijizolea umaarufu kutokana na vita kati ya mgambo na wamachinga.


TIMU 7 MTAA MMOJA

Lakini wengi hawafahamu kama Mtaa wa Congo ulikuwa ukimiliki timu saba. Yaani katika mtaa mmoja kulikuwa na timu saba.

Hapo ndipo utakapojua kwamba, zamani soka lilikuwa linachezwa Mtaa wa Congo jijini Dar es Salaam.


KULIKUWA NA NUNGU

Hii timu zamani ilikuwa ikijulikana kwa jina la New Port lakini baadaye ilikuja kubadilisha jina na kuitwa Nungu. Ni timu iliyokuwa na umaarufu mkubwa sana jijini.

Nungu imewatoa wachezaji wengi waliokuja kutamba kwenye soka la Tanzania.

Pia katika mtaa huo kulikuwa na timu iliyoitwa Congo Shooting, hii nayo kama ilivyo jina lake masikini yake yalikuwa mtaa wa Congo na Mtambani. Nayo ilikuwa na umaarufu wake.


UNAIKUMBUKA TOLOLO

Mojawapo kati ya timu kongwe jijini Dar es Salaam. Masikani yake yalikuwa kati ya Mtaa wa Congo na Kibambawe. Nayo ilikuwa na umaarufu wake wachezaji wengi wakitokea katika timu hii iliyosheheni watoto wa mjini.

Mtaa wa Congo umevuka mtaa wa Msimbazi, badi mbele yake kulikwua na timu iliyoitwa Congo United, hii nayo ilikuwa ndani ya mtaa huo. Timu hii kwa jina la utani ilikuwa ikifahamika kama ‘Shetani Wekundu’. Kabla ya jina hilo timu hii ilitumia jina la Benfica.

Majina ya zamani ya timu zetu yalitokana na majina ya timu za nje. Vijana wengi walipenda kusafiri na waliosafiri walikuja na stori za nje na kuambukiza majina hayo kwa wenzao.


MASKANI YA SIMBA

Katika historia, inaonyesha Simba Sports Club iliwahi kuweka maskani yake kati ya Mtaa wa Congo na Mchikichi.

Kabla yake katika mtaa huo kulikuwa na timu iliyokuwa ikitambulika kwa jina la Blackpool.

Baadaye ikaja Simba ambayo ilipohama kwenda Mtaa wa Msimbazi ikaweka maskini yake.

Mbele ya mtaa huo, kulikuwa na timu ya Nyota Nyekundu. Hii ilianzishwa mwaka 1975 baada ya baadhi ya viongozi Simba kujiengua kutoka Mtaa wa Msimbazi.


VALENCIA TAWI LA SIMBA

Ukivuka barabara ya Uhuru na kuelekea kama unaenda Gerezani, ukiwa mtaa huo huo wa Congo, pia kulikuwa na timu ya Valencia.

Hii ilikuwa ni kama tawi la Simba ambapo kuna baadhi ya wachezaji waliotoka kwenye klabu hiyo na kujiunga na Mnyama, mmoja wao akiwa ni Haidary Abeid.

Wapinzani wakubwa wa Valencia walikuwa ni Gerezani United ambayo moja kwa moja ilijinasibu kuwa tawi la Yanga Afrikani.

Kilikuwa kikipigwa hapo unaambiwa ni kama vile Kuala Lumpur (Kwala) na Lunyasi.