MJUAJI: Kibadeni aing'arisha Simba kwa wachina

KUNA kitu kinashangaza sana katika miaka hii, zamani kulikuwa na burudani sana ya michezo kwa ujumla.

Timu kutoka mataifa mbalimbali zilikuwa zinafanya ziara nchini na kucheza na timu zetu. Ilikuwa sio jambo la ajabu kwa timu kutoka Uingereza, Brazil na mataifa mengine kutua nchini.

Hata timu zetu zilikuwa zinatoka sana nje kwa ajili ya kwenda nje kwa minajili ya kujifunza soka.

Simba na Yanga zimeshakwenda Brazil, Romania, Guinea na sehemu nyingine duniani kwa ajili ya mafunzo ya mchezo wa soka.

Shida zilipokuwa zikija timu za Bara la Asia na wengi kudhani kuwa labda ni vibonde na kutegemea kupata mteremko.


WALIITWA MABAHARIA

Kuna timu za Bara la Asia zilikuja Tanzania na kufungwa mabao mengi na baadhi ya mashabiki kuwadhihaki kwa kuwaita mabaharia.

Lakini Simba ilikutana na mziki mnene ilipocheza dhidi ya Wachina ambao hadi leo hii kuna watu wanalikebehi taifa hilo kwa kuamini watu wake hawajui kusakata soka.

Ilikuwa Desemba 26, 1971 katika Uwanja wa Ilala (sasa Karume), kulikuwa na mchezo wa kusisimua na nyota wa Simba enzi hizo, Abdallah ‘King’ Kibadeni aliing’arisha timu yake.

Awali mashabiki wengi walitajia mchezo ungekuwa wa upande mmoja, lakini hadi wanatoka uwanjani walipata kitu ambacho hawaku wamekitarajia kutokana na timu kutoka China kutoa upinzani mkali.

Wachina hao walicheza soka la hali ya juu mwanzo mwisho, walikuwa na chenga za maudhi ambazo ziliwapagawisha sana wachezaji wa Simba.


WACHEZAJI HATARI

Timu ya China ilikuwa na wachezaji hatari ambao kila wakati walikuwa wakilisakama lango la Simba.

Wachezaji wasumbufu walikuwa ni Li Chou Che, Wang Chu, Chang Chung Wei, Istu Ken Pao na Chin Shang Pin.

Kitu kilichozuia Simba kuadhibiwa mapema ni kutokana na kuwa na ngome imara ingawaje kuna wakati ilisumbuliwa mno na wachezaji hao wa Kichina.

Washambuliaji wa Simba, Will Mokili, Haidar, Ngasa, Kesi Manangu na Clement- ‘Sharp Shooter’ walipoteza nafasi nyingi za kufunga.


WACHINA KIDEDEA

Safu ya mabeki wa Simba ilikuwa imeundwa na Kipa Hassans, Mohamed Kajole, Juma Mzee, Omari Chogo na Bobea.

Safu hiyo ya ulinzi ilikuwa na wakati mgumu kwani hadi mchezo unamaliza dakika 45 za kwanza, Wachina walikuwa wakiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa katika dakika ya 16 na Wang Hou Chun kwa mkwaju mkali ambao uliwashangaza mashabiki waliokuwapo uwanjani.


PELE WA TANZANIA

Kipindi cha pili wenyeji walicheza soka la kuvutia na mchezaji Abdallah Kibadeni ‘Pele wa Tanzania’ kama alivyokuwa akiitwa kipindi hicho aliwasumbua sana Wachina.

Mchezaji wa Simba, Haidari Abeid alishindwa kumaliza mchezo huo baada ya kuumia mguu alipogongana na mchezaji mmoja wa China na nafasi yake ilichukuliwa na Yusuf.

Mbali na mabadiliko hayo, Simba iliwatoa Ngassa na nafasi yake ikachukuliwa na Choteka, akatoka Clement akaingia Adam Sabu ‘Gerd Muller’.

Wakati jahazi likielekea kuzama ilitokea faulo katika lango la Wachina, ilikuwa ni ‘indirect’ na Kibadeni alichukua jukumu la kupiga friikiki hiyo.

Mchezaji huyo alipiga pasi kwa Sabu ambaye aliunganisha kwa shuti kali na kuikoa Simba kufungwa na Wachina hao.

Lakini wakati mashabiki wa Simba wakishangilia bao hilo, mshambuliaji wa timu ya China, Tseng Chuo Neng aliifungia timu yake bao la pili na kuwafanya mashabiki wa Simba kunyamaza kama vile walikuwa wamemwagiwa maji.


SIMBA YACHARUKA

Baada ya kupata bao la kusawazisha, Simba ilicharuka kwa kucheza soka la uhakika na dakika za mwisho kabisa kuweza kundikisha ushindi wa mabao 3-1 baada ya King Kibadeni kutupia mabao mawili.