Mizinga: Kuna ngumi nilipigwa inanisumbua hadi sasa

Muktasari:
- Mizinga mwenyewe anasimulia amepewa jina hilo kutokana na aina ya ngumi ambazo zimekuwa zikifananishwa na mizinga kutokana na uzito wake.
SALMINI Kassim ‘Mizinga’ dhahabu mpya ambayo imekosa kuimbwa katika mchezo wa ngumi za kulipwa nchini licha ya kuendelea kuweka rekodi mpya kwenye masumbwi.
Mizinga mwenyewe anasimulia amepewa jina hilo kutokana na aina ya ngumi ambazo zimekuwa zikifananishwa na mizinga kutokana na uzito wake.
Bondia huyo ambaye ni mmoja kati ya mabondia ambao wamedumu kwenye msingi wa ngumi yaani ngumi za ridhaa amekuwa na rekodi ya aina yake kabla ya kuingia kwenye ngumi za kulipwa akiwa chini ya Mafia Boxing Promotion ambao wamekuwa wakiandaa mapambano ya Knockout ya Mama.
Mizinga anatarajia kupanda ulingoni kutetea mkanda wake wa Ubingwa wa WBF Intercontinental Julai 26, mwaka huu, kwenye pambano la ‘Knockout ya Mama’ ambalo limepangwa kufanyika kwenye Viwanja vya Posta, Kijitonyama, Dar es Salaam.
Bondia huyo kwenye ngumi za kulipwa mpaka sasa amecheza mapambano tisa akiwa ameshinda saba kati ya hayo manne ameshinda kwa knockout na kutoka sare mara mbili bila kupoteza pambano lolote.
Mizinga ni bondia namba moja katika mabondia 62 wa uzani wa super bantam wakati duniani akiwa wa 33 katika mabondia 1438 huku akiwa na hadhi ya nyota tatu na nusu.
Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na bondia huyo ambaye amefunguka mambo mengi yanayomzunguka kwenye mchezo huo.
SWALI: Jambo gani limekufanya uingie kwenye mchezo wa ngumi?
JIBUI: Kwanza mchezo nilikuwa naupenda lakini nilikuwa mmoja kati ya watoto watukutu mtaani kwetu ila sababu kubwa ilitokana na unyonge wa utoto.
Nakumbuka kuna kipindi hayati baba yangu alikuwa analetewa taarifa nyumbani kwetu kwamba nimepigwa na watoto wenzangu, ila yeye alikuwa akichukua fimbo ananichapa.
Lakini sababu kubwa alikuwa akihoji kwa nini nipigwe maana yeye alikuwa anataka akipelekewa kesi ya kuwa nimepiga mtu na siyo kupigwa.
Sasa nakumbuka mara ya mwisho aliletewa kesi ya kuwa nilimpiga mtu ambaye alikuwa ndugu yangu upande wa mama ila sikuwa nafaham kama ni ndugu yangu.
Kutokana na hali hiyo mama yangu akanichukulia uhamisho wa kutoka Tanga kuja kusoma Dar, eneo la Tegeta katika shule ya Pius Msekwa. Sasa huku mazingira ya kwenda ufukweni mwa habari nakuona watu wanafanya mazoezi ya mchezo huu ndiyo nikazidi kuupenda kabisa.
SWALI: Mara kadhaa umekuwa ukisema kama siyo mama (Rais), basi ungekuwa unasumbuana na polisi?
JIBU: Unaona pale Tegeta hasa wakati nimetoka Tanga pale nilikutana na makundi mengi sasa nilikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa kwenye makundi japo nilikuwa mdogo ila watu walikuwa wakinikubali.
Kutokana na ile hali nikawa nachukuliwa ssna wakati mwengine tunaenda hadi Bagamoyo kucheza ngumi hali ambayo mama yangu aliona kwamba nimeshakata kamba siwezi kuelewa mtu yoyote na sababu alikuwa hapendi makundi yangu.
Mama amepambana sana kunizuia kucheza ngumi na nisijichanganye na makundi ya wale watu ambao aliona siyo wazuri upande wangu. Lakini licha ya mama yangu kupinga harakati zangu ila Mama Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) amekuja kuufanya mchezo huu uonekane kama kazi nyengine siyo uhuni ndiyo maana napenda sana kuongea kauli hiyo.
Kama siyo mama (Rais) na serikali yake wasingeupa kiupambele kwa Mama kuwafungua watu macho na masikio kwamba hii ni kazi kama kazi nyingine.
Unaona amekuwa akitoa zawadi za fedha katika kila pambano la knockout ya Mama ambayo imetufaidisha mabondia wengi lakini amekuwa balozi wetu mkubwa wa kuhamasisha kila pambano la knockout ya Mama.
SWALI: Umedumu kwa muda gani kwenye ngumi za ridhaa kabla ya kuingia kwenye ngumi za kulipwa?
JIBU: Kiukweli kwenye ngumi za ridhaa, nimecheza mapambano mengi yanafika 100 maana katika kipindi cha miaka mitano nilikuwa nacheza ngumi za ridhaa.
Nimefanikiwa kushinda makombe mawili, nina medali tatu za ubingwa katika mashindano tofauti ya ngumi za ridhaa ambayo nimewahi kucheza katika kipindi chote.
SWALI: Mabondia wengi wanacheza ngumi za ridhaa kwa lengo la kutafuta nafasi ya kwenda jeshini kwako ilikuwaje?
JIBU: Unalosema ni jambo la kweli kwa sababu hata mimi nimefanya mazoezi kwenye ile kambi ya Lugalo ambayo ina mabondia wengine kama akina Selemen Kidunda, Haruna Swanga na George Bonabucha ambao wote kaka zangu.
Nadhani nilikosa nafasi kwa sababu nilikosa mtu wa kunishika mkono lakini binafsi ndoto yangu ilikuwa niweze kuajiriwa katika taasisi hiyo ili nizidi kuutambulisha mchezo wa ngumi kama ajira na kazi.
Kuacha kufanya mazoezi pale ilitokana na kutatishwa tamaa kwamba kama sina wa kunishika mkono siwezi kusogea popote ingawa marehemu baba yangu alikuwa akiniambia nisiwe na haraka nitafika mbali kwenye mchezo huu.
Lakini mama yangu alikuwa hataki kabisa kuona nacheza ngumi kutokana na kuamini ni sehemu ya kujifundisha uhuni lakini nashukuru Mungu Kampuni ya Mafia Boxing Promotion imeniona ikanichukua kuwa chini yake.
SWALI: U’shawahi kupigwa ngumi ukatamani kuacha kabisa kupigana?
JIBU: Nakumbuka ilikuwa kwenye ngumi za ridhaa nilipigana siku nne mfululizo katika mashindanoo ya klabu bingwa. Nilicheza na wanajeshi nakumbuka kina Selemani Kidunda, George Bonabucha na hapo ndiyo nilijenga nao urafiki wakanipa na mawasiliano yao.
Sasa katika zile siku nne siku tatu nilipigana kwenye hatua ya nusu fainali, pambano lilikuwa na upinzani kwa sababu mpinzani nilishapigana naye awali kwenye mashindano ya mtaa kwa mtaa.
Unajua mara zote nilikuwa nampiga, sasa ile akasema lazima nidondoke. Pambano lilikuwa gumu, nakumbuka kuna ngumi alinipiga nikaangukia mkono wa kushoto kwa kuulalia.
Siwezi kusahau kwa sababu siku hiyo ndiyo niliona huu mchezo mgumu mgumu nikatamani nisiendelee, lakini nashukuru nilimpiga kwa (pointi za) majaji wote watatu na kwenda fainali ambayo pia nilishinda.
SWALI: Siku hizi watu wanadai ngumi ni kama soka kutokana na watu kupuliza sana (ushirikina), vipi upande wako umeshakutana nayo?
JIBU: Nadhani nilishakutana na hali hiyo, nakumbuka kuna pambano moja nimepigana nilikuwa najiona sipo ulingoni kabisa kutoka raundi ya kwanza hadi ya pili mwili ulikuwa umepoa kabisa na siyo kawaida.
Unajua nilikuwa ni mtu ambaye natembea sana kwenye ngumi za ridhaa yaani napiga natembea lakini hiyo siku sikuweza kabisa kufanya hivyo hadi nilipopigiwa kelele na watu.
Kiukweli katika mchezo huu na michezo mingine inahitaji sana kumuomba Mungu na kufanya dua za kutosha kwa sababu hayo mambo yapo na hata sisi hapa Mafia unakuta watu sali sala zote maana bila ya kumshirikisha Mungu huwezi kufanikiwa.
SWALI: Ngumi zimekupa gari lakini wewe ulipanga kumiliki gari baada ya muda gani?
JIBU: Nilipanga baada ya miaka mitatu ndiyo nimiliki usafiri wangu mwenyewe, lakini namshuruku Mungu nimeweza kumiliki gari mapema kutokana na juhudi za kufanya vyema kwenye mapambano yangu.
Uongozi wangu wa Mafia Boxing umeona unipe gari aina ya Toyota Rumion kama motisha ya kuendelea kupambana vyema katika mapambano yangu na kuweza kushinda mikanda mikubwa ya ubingwa.
SWALI: Familia yako inachukuliaje kwa sasa harakati zako?
JIBU: Binafsi naona familia yangu inachukulia kwa ukubwa tofauti na zamani hasa mama yangu alikuwa hapendi kabisa huu mchezo ila sasa ananiunga mkono kwa asilimia zote.
Sasa hivi nimekuwa baba wa familia kwa sababu kwetu mimi ndiyo mtoto wa kwanza halafu wapo wadogo zangu wengine wanne ambao wote kwa sasa nimekuwa tegemo lao.
Familia yangu kwa sasa inanitazama kwa umbali mkubwa sana kuhakikisha mambo yanakwenda sawa wakati wote na wamekuwa wa kwanza wao kuniombea dua na riziki inafunguka.
SWALI: Una uwezo wa kula kiasi gani kwa siku?
JIBU: Uwezo wangu wa kula kwa siku ni nusu na robo ya ugali hasa wa dona, lakini mara nyingi napenda kula ugali wa muhogo ambao naupenda sana na mwenyewe nalima hiyo mihogo kwetu Tanga.
SWALI: Umejipanga vipi kutetea ubingwa wako wa WBF kwenye pambano la Knockout ya Mama Julai 26, mwaka huu?
JIBU: Binafsi nimejipanga vizuri kwa sababu lengo ni kuipa heshima nchi yangu pamoja na menejimenti ambayo inanisimamia siku zote imekuwa chachu kubwa ya mimi kufanya vizuri katika mapambano yangu.