Mitihani mitatu ya kuishinda Masaka England
Muktasari:
- Ulikuwa uhamisho mkubwa uliogonga vichwa vya habari duniani baada ya nyota huyo kuandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kike kutoka Tanzania kucheza Ligi Kuu England yenye ushindani mkubwa.
BAADA ya kuonekana kama mmoja wa nyota chipukizi wenye vipaji vikubwa kwenye soka la wanawake Tanzania, jina la Aisha Masaka lilipata umaarufu mkubwa kimataifa mwaka 2024 baada ya kutambulishwa Brighton Hove Albion Women ya England akitokea BK Hacken ya Sweden.
Ulikuwa uhamisho mkubwa uliogonga vichwa vya habari duniani baada ya nyota huyo kuandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kike kutoka Tanzania kucheza Ligi Kuu England yenye ushindani mkubwa.
Hata hivyo, matarajio hayakuwa kama vile mashabiki wengi kutoka Afrika waliotamani nyota huyo kucheza na kuanza kwenye kikosi cha kwanza, tofauti na matarajio hayo kiuhalisia soka la Ulaya limejaa ushindani mkubwa kwa timu hadi wachezaji wenyewe wanaowania kucheza na kung’ara.
Msimu wa kwanza 2024/25, Masaka hakupata muda wa kutosha kucheza akiishia benchi na mara kadhaa alionekana mazoezini tu. Swali, je Masaka bado ana nafasi ya kucheza na kung’ara Ulaya?
Ipo mifano kadhaa ya wachezaji wa kike kutoka Afrika ambao walifanya vizuri kwenye ligi walizotoka wakapata nafasi ya kuanza kwenye vikosi vya kwanza na hadi leo ni wachezaji muhimu katika timu wanazocheza.
Mzambia Racheal Kundananji, mwaka 2021, alisajiliwa Eibar ya Ligi Kuu Hispania akitokea BIIK Kazygurt ya Kazakhstan. Hakupata nafasi ya kucheza na kuanza kikosi cha kwanza kutokana na kushindwa kuzoea kasi ya ligi hiyo maarufu kama Liga F.
Msimu uliofuata alisajiliwa Madrid CFF ambako alipata nafasi ya kucheza na kuonyesha kiwango bora akifunga mabao 20 na akawa mmoja wa wafungaji bora kwenye ligi hiyo. Hakukawia mwaka 2024 akasajiliwa na Bay FC ya Marekani kwa dau la Dola 860,000 akiweka rekodi ya kuwa mchezaji kutoka Afrika aliyeuzwa kwa dau kubwa.
Mchezaji mwingine ni Salma Paralluelo aliyesajiliwa Barcelona ya wanawake msimu 2022/23 kama mchezaji kijana akitokea Zaragoza CFF. Alipambana kuzoea mazingira ya ligi ya Hispania kwani hakuwa chaguo la kwanza kama ilivyokuwa kwa Masaka msimu wa kwanza.
Msimu uliofuata akawa mshambuliaji tegemeo Barca akifunga mabao muhimu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Dunia la Wanawake 2023 akiiwezesha Hispania kutwaa ubingwa wa dunia akiwa mchezaji muhimu.
Hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao hawakuanza vizuri kwenye timu walizopita, lakini baadaye wakafanya vizuri. Ujao ni msimu mpya ambao sasa ni kama fursa kwa Masaka na nafasi ya kuonyesha kuwa bado anaitaka nafasi ya kucheza kwenye kikosi hcha Brighton.
Mwanaspoti linakuchambulia mitihani mitatu anayotakiwa kuivuka Masaka ili kupata nafasi ya kucheza Brighton na kuonyesha kiwango bora - mitihani ambayo huenda ikafungua mlango wa mafanikio yake katika soka la kulipwa Ulaya.
UBORA WAKE
Tangu alipotua Brighton 2024 akitokea BK Hacken ya Sweden amecheza mechi mbili pekee. .
Ndani ya msimu huo alikumbana na changamoto ya majeraha yaliyomuweka nje kwa takribani nusu msimu.
Baada ya kupata nafasi finyu msimu uliopita, Aisha atapaswa kuonyesha kuwa bado ana uwezo mkubwa wa kushindania nafasi yake mbele ya nyota wa kimataifa alioana katika kikosi hicho.
Kwa hali hiyo anapaswa kuongeza juhudi kwenye uwanja wa mazoezi na kuongeza kujiamini kila anapopewa nafasi ya kucheza dakika chache.
KIKOSI CHA KWANZA
Timu hiyo ina wachezaji wazuri eneo hilo na wamekomaa kimwili na kiakili - wakicheza mechi nyingi zenye ushindani, hivyo nafasi kikosini hapo inaonekana kuwa na ushindani.
Msimu uliopita Brighton iliachana na nyota Michelle Agyemang ambaye alikuwapo kwa mkopo akitokea Arsenal, Nikita Paris ambaye alikuwa na pacha nzuri eneo hilo na Fran Kirby wakifunga mabao 19 kwa ujumla na Lee Geummin ambaye hakuwa anacheza mara kwa mara.
Msimu ujao Brighton haitakuwa na nyota hao kwani imeshawapa mkono wa kwaheri akisalia Masaka pekee kwenye eneo la ushambuliaji, na tayari imemsajili Carla Camacho kutoka Real Madrid ambaye alicheza mechi 15 akifunga bao moja.
Ili kushindania nafasi Masaka anapaswa kufanya vizuri kwenye mechi za kirafiki na mashindano mengine ya kawaida ambayo hutoa nafasi kwa wachezaji ambao hawaanzi mara kwa mara.
Pia anapaswa kuonyesha utofauti na washambuliaji wengine ikiwamo kucheza kwa kasi, uwezo wa kupiga mashuti nje ya boksi na utoaji wa assisti.
KIMWILI
Tofauti na Tanzania na Sweden alikocheza, soka la England ni la kasi na linahitaji umara kimwili na kiakili ili kuendana na ligi.
Tayari amekuwapo huko msimu mmoja, hivyo ni wazi ameshafahamu mazingira ya soka ambalo wachezaji wengi kutoka mataifa mbalimbali huanza kujifunza taratibu na baadaye huingia moja kwa moja kwenye mifumo
Umbo linambeba mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ‘Twiga Stars’. Hali hiyo pia inampasa kuongeza stamina na kuwa na uwezo wa kukabiliana na mabeki wenye nguvu.
Hivi karibuni nyota huyo aliutaarufu umma kuwa asingeshiriki mashindano ya WAFCON na hakushiriki, baada ya kupata jeraha la goti, hivyo anapaswa kufanyia kazi ushauri atakaopewa na benchi la ufundi la Brighton ili kuuweka mwili wake sawa.
Ikiwa Masaka atavuka mitihani hiyo anaweza kurudi kwenye ubora wake wa awali na hata kufikia kiwango bora kabisa cha kuanza katika kikosi cha kwanza cha timu yake.