Mikataba inavyowapa mamilioni wabongo

Muktasari:
- Katika ulimwengu wa soka kuvunjwa kwa mikataba ya wachezaji ni jambo linalotokea mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali kama vile utovu wa nidhamu, kushuka kwa viwango vya uchezaji, au mabadiliko ya kiufundi ndani ya klabu.
KUMEKUWA na wimbi la wachezaji wa Bongo wanaocheza soka la kulipwa nchi mbalimbali kukutana na changamoto za kuvunjiwa mikataba ambayo sasa wanapambana na kupata haki zao.
Katika ulimwengu wa soka kuvunjwa kwa mikataba ya wachezaji ni jambo linalotokea mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali kama vile utovu wa nidhamu, kushuka kwa viwango vya uchezaji, au mabadiliko ya kiufundi ndani ya klabu.
Kwa Tanzania klabu kubwa kama Yanga inapitia changamoto hiyo bada ya kuvunja mkataba na aliyewahi kuwa mchezaji wake, Augustine Okrah.
Mwanaspoti imekuchambulia baadhi ya wachezaji wa Kitanzania wanaokipiga nje ya nchi wanavyopata mamilioni kupitia klabu zao kuvunja mikataba nao, shukrani kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambalo limekuwa likiwalinda wachezaji wote ambao wako katika hatari ya kudhulumiwa.

1. Abdi Banda
Kwa sasa Banda karudi zake Bongo akisaini mkataba wa miezi sita na Dodoma Jiji baada ya kuondoka Baroka FC ya Afrika Kusini.
Hii sio mara ya kwanza Banda kucheza Baroka. Awali alijiunga na timu hiyo akitokea Simba Julai 12, 2017.
Banda aliondoka kikosini hapo ikiwa miezi mitano tu tangu ajiunge nao Septemba mwaka jana.
Hata hivyo, Banda alivunja mkataba ambao ulikuwa na makubaliano ya pande zote huku sababu ikitajwa beki huyo wa Tanzania alitaka kupata changamoto sehemu nyingine.
Achana na ishu hiyo ambayo kiraka huyo alivuna pesa nyingi licha ya kutoweka wazi kitita hicho lakini Novemba mwaka jana alishinda kesi ya mamilioni dhidi ya Richard Bays ya nchini humo.
Novemba, Fifa iliiamuru Richard Bays FC aliyokuwa akiichezea Banda kumlipa nyota huyo wa kimataifa pesa zake za mshahara na usajili anazowadai kiasi cha Sh115 milioni ndani ya siku 45 ambazo kama isingemlipa ndani ya muda huo basi ingekutana na rungu la kufungiwa kusajili wachezaji.
Hii sio mara ya kwanza kwa Banda mwenye umri wa miaka 29, kukumbana na kesi hiyo, kwani mwaka 2023 akiwa na Chippa United ya Afrika Kusini alifungua kesi ya madai baada ya timu hiyo kuvunja mkataba wake mapema mwaka mmoja tu baada ya kujiunga.
Chippa ilishindwa kumlipa Mtanzania huyo kwa muda uliopangwa kiasi cha Sh180 milioni jambo lililoifanya klabu hiyo kupigwa rungu la kusajili wachezaji kabla ya baadae kumalizana naye na Januari ikaondolewa adhabu hiyo.
Nyota huyo aliichezea Richard Bay msimu uliopita kabla ya kurejea Baroka FC ambako hakupata nafasi kubwa ya kucheza kwani katika msimu huo alicheza mechi nane za mashindano yote.
Banda aliwasilisha malalamiko kwa chombo cha kusimamia malalamiko ya mikataba kwa wachezaji (Dispute Resolution Chamber, DRC) Novemba 21 mwaka huu dhidi ya klabu hiyo kwa madai ya kuvunjiwa mkataba wake.
Hatua ya Banda ya kufikisha suala hilo FIFA ilikuja baada ya changamoto alizokutana nazo akiwa klabuni ikiwamo kutolipwa mishahara na ukosefu wa nafasi za kutosha za kucheza.

2. Simon Msuva
Ni mchezaji muhimu kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kutokana na umahiri wake wa kufunga mabao.
Nyota huyo anayekipiga Al Talaba ya Iraq Julai 2022 aliishtaki Wydad AC klabu aliyowahi kuitumikia kwa kosa la kuvunja mkataba kinyume cha utaratibu baada ya kuwa katika mvutano wa kimaslahi na vigogo hao wa soka la Afrika ambao walimsajili Novemba 2020 akitokea Difaa El Jadida ya nchini humo.
Baada ya kesi hiyo FIFA iliiamuru timu hiyo kumlipa Dola 700,000 sawa na zaidi ya Sh1.6 bilioni Mtanzania huyo kutokana na kushindwa kumlipa pesa za usajili ikiwemo malimbikizo ya mshahara.
Hata hivyo, Wydad ilikaidi maagizo hayo na Novemba mwaka jana ikafungiwa kusajili wachezaji wa ndani na nje hadi pale itakapomlipa Msuva fedha zake.

3. Abdallah Shaibu ‘Ninja’
Beki huyo wa zamani wa Yanga alivunja mkataba na FC Lupopo mwaka jana baada ya kujiunga nayo Julai ambako hakuwa anapata nafasi kutokana na kusumbuliwa na majeraha.
Sababu ya kuvunja mkataba huo ambao ulibakia miezi sita Ninja alieleza ni changamoto za kimaslahi.
Ninja alijiunga na klabu hiyo msimu huu akitokea Lubumbashi Sports ya nchini humo ambayo aliichezea kwa msimu mmoja kati ya miwili aliyokuwa amesaini ambapo sababu ya kuachana nayo ni changamoto ya mshahara.

4.Gadiel Michael
Beki huyu wa kushoto hakudumu muda mrefu kwenye kikosi cha Chippa United ya Afrika Kusini kwani Desemba mwaka jana alivunja mkataba na kurejea Singida Black Stars.
Hakuna sababu maalumu zilizowekwa wazi kuhusu kuvunjwa kwa mkataba wa kiraka huyo aliyetimka Afrika Kusini.
Gadiel alijiunga na timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Cape Town Spurs ya nchini humo na kuungana na Mtanzania mwenzie Baraka Majogoro aliyesalia klabuni hapo.
Mbali na hilo Gadiel tangu ajiunge na timu hiyo Septemba amedumu klabuni hapo kwa miezi minne na kurudi Bongo. Maokoto yanazingatiwa.