Michael Olise Winga mwenye mikoba yake Bayern Munich
Muktasari:
- Kupitia uwezo wake wa kupiga vyenga, kutoa pasi za mwisho na kufunga mabao muhimu, Olise mwenye mabao 11 na asisti 20 kwenye Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga huku akiwa na mabao matatu na asisti saba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ameanza kutajwa miongoni mwa wachezaji bora kabisa katika nafasi yake duniani.
BERLIN, UJERUMANI: WINGA mahiri wa Bayern Munich, Michael Olise, ameibuka kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi barani Ulaya, akigeuka kuwa mhimili mkuu wa ubunifu ndani ya kikosi hicho cha Ujerumani.
Ndani ya muda mfupi tangu ajiunge na klabu hiyo, tayari ameweka alama kubwa na kuifanya Bayern kuwa na makali zaidi katika safu ya ushambuliaji.
Kupitia uwezo wake wa kupiga vyenga, kutoa pasi za mwisho na kufunga mabao muhimu, Olise mwenye mabao 11 na asisti 20 kwenye Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga huku akiwa na mabao matatu na asisti saba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ameanza kutajwa miongoni mwa wachezaji bora kabisa katika nafasi yake duniani.
Wataalamu wengi wa soka wanaamini kuwa nyota huyo bado hajafikia kilele chake, jambo linalozidi kuwapa matumaini mashabiki wa Bayern.
Kwa sasa, jina lake limekuwa gumzo katika soka la Ulaya, huku klabu kubwa zikianza kuonyesha nia ya kumtaka, jambo linaloonyesha thamani yake imepanda kwa kasi kubwa.
Liverpool Wamnyemelea
Ripoti za hivi karibuni zinaeleza kuwa Liverpool wanamtazama Olise kama mbadala sahihi wa Mohamed Salah ambaye anaweza kuondoka mwishoni mwa msimu. Hata hivyo, juhudi za kumshawishi mchezaji huyo zinaonekana kuwa ngumu kutokana na msimamo wa Bayern Munich.
Uongozi wa Bayern umeweka wazi kuwa hauna mpango wowote wa kumuuza nyota huyo, hasa ikizingatiwa mchango wake mkubwa ndani ya kikosi. Kauli ya rais wa heshima wa klabu hiyo, Uli Hoeness, imeonyesha wazi msimamo huo.
“Liverpool walitumia fedha nyingi lakini bado hawako kwenye kiwango kizuri. Hatuwezi kuwasaidia kuwa bora zaidi,†anasema Hoeness, akionyesha wazi kuwa Bayern wanalinda maslahi yao ya kisoka kuliko fedha.
Kauli hiyo inaonyesha kuwa Bayern wako tayari kumjenga Olise kuwa sehemu ya msingi ya mafanikio yao ya baadaye.
Usajili uliozua mjadala
Wakati Bayern walipolipa euro 60milioni kumsajili Olise kutoka Crystal Palace mwaka 2024, wengi walishangazwa na uamuzi huo. Baadhi ya wachambuzi walihoji kama mchezaji huyo angeweza kuhimili presha ya kucheza katika klabu kubwa kama Bayern.
Hata hivyo, kulikuwa na kundi la watu waliotambua kipaji chake mapema. Nguli wa soka Thierry Henry alikuwa mmoja wao, akieleza kuwa Olise ana uwezo wa kipekee ambao haupatikani kirahisi kwa wachezaji wengi.
Licha ya mashaka yaliyokuwepo, Olise amethibitisha kuwa uwekezaji huo ulikuwa sahihi. Ameonyesha nidhamu, uwezo huku akiepuka majeraha ambayo yalikuwa yakimwandama mara kwa mara awali.
Leo hii, wachambuzi wengi wanakubaliana kuwa huo ulikuwa mmoja wa usajili bora zaidi kuwahi kufanywa katika Bundesliga katika miaka ya hivi karibuni.
Anajibu kwa vitendo
Olise sio mchezaji wa kuzungumza sana nje ya uwanja. Mara nyingi amekuwa akionekana mwenye aibu au mwenye majibu mafupi anapozungumza na vyombo vya habari.
Lakini tofauti kabisa huonekana anapokuwa uwanjani. Hapo ndipo anapotoa majibu yake halisi kupitia kiwango chake.
Kupitia ubunifu wake, pasi za mwisho na uwezo wa kufunga mabao, Olise amewafanya mashabiki wa Bayern kumpenda haraka sana. Ameonyesha kuwa ana uwezo wa kubadilisha matokeo ya mchezo ndani ya muda mfupi.
Ndani ya Kikosi
Katika msimu wake wa kwanza, Olise aliweka rekodi ya aina yake kwa kucheza mechi zote za Bundesliga, jambo lililoonyesha uimara wake.
Alifunga mabao 20 na kutoa pasi za mabao 23 katika mashindano yote, takwimu ambazo ni nadra kwa mchezaji mpya katika ligi hiyo.
Kocha Vincent Kompany alikiri kuwa mchango wake ni mkubwa sana kwa timu maana sio jambo la kawaida kwa mchezaji mpya kuzoea haraka mazingira mapya kwa kiwango hicho.
Zaidi ya hayo, uwepo wake umeongeza ubora wa safu ya ushambuliaji ya Bayern, akishirikiana vyema na wachezaji wengine wa mbele.
Anaendelea Kupaa Zaidi
Wengi walidhani kuwa msimu wake wa kwanza ndio ungekuwa bora zaidi lakini Olise ameonyesha kuwa bado ana mengi ya kuonyesha. Katika msimu wa 2025/26, ameendelea kung’ara zaidi, akihusika moja kwa moja na mabao 37 katika mashindano yote.
Uwezo wake wa kucheza katika nafasi mbalimbali za ushambuliaji umemfanya kuwa mche zaji muhimu katika mipango ya kocha wake.
Hali hii imeongeza thamani yake sokoni na kumfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaomezewa mate zaidi barani Ulaya kwa sasa.
Kulinganishwa na magwiji
Kutokana na uwezo wake, Olise amekuwa akilinganishwa na baadhi ya wachezaji wakubwa waliowahi kucheza katika nafasi hiyo, akiwemo Arjen Robben.
Hata hivyo, kocha Kompany anaamini kuwa Olise ana sifa zinazofanana zaidi na Kevin De Bruyne, hasa katika ubunifu na namna anavyoona mchezo.
Kwa mujibu wa Kompany, Olise ana nidhamu ya hali ya juu na umakini mkubwa katika mazoezi na mechi, jambo linalompa nafasi ya kufikia kiwango cha juu zaidi.
Winga bora zaidi kwa sasa?
Kwa kiwango anachoonyesha kwa sasa, wachambuzi wengi wanaamini kuwa Olise ni miongoni mwa winga bora duniani, kama si bora kabisa.
Kauli ya Sami Khedira imethibitisha hilo, akisema kuwa Olise ana kila kitu kinachohitajika kwa mchezaji wa kiwango cha juu kuanzia kasi, ubunifu na uwezo wa kuamua matokeo ya mchezo.
Akiwa na umri wa miaka 24 pekee, nyota huyo bado ana muda mwingi wa kuendelea kuboresha kiwango na kufikia mafanikio makubwa zaidi.
Ikiwa ataendelea kwa kasi aliyo nayo hakuna shaka kuwa dunia ya soka bado haijakiona kilele cha uwezo wake na huenda akawa mmoja wa mastaa wakubwa zaidi katika historia ya mchezo huo.