Kisa Salah, mastaa kibao watajwa Liverpool
Muktasari:
- Salah anaondoka akiwa mchezaji wa tatu kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo, na ili kuziba pengo, Liverpool inataka kusajili washambuliaji wawili wapya, mmoja mwenye jina kubwa na mwingine mwenye umri mdogo anayechipukia.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL ipo katika mchakato wa kuboresha safu ya ushambuliaji kwa kusajili washambuliaji wawili wapya kwenye dirisha lijalo la usajili wa kiangazi ambao pia wataziba pengo la Mohamed Salah anayeondoka mwisho wa msimu huu.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Misri mwenye miaka 33 alitangaza mapema wiki iliyopita kuwa ataondoka mwishoni mwa msimu wa 2025-26, baada ya kuitumikia Liverpool kwa miaka tisa.
Salah anaondoka akiwa mchezaji wa tatu kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo, na ili kuziba pengo, Liverpool inataka kusajili washambuliaji wawili wapya, mmoja mwenye jina kubwa na mwingine mwenye umri mdogo anayechipukia.
Kwa mujibu wa The i Paper, staa wa Juventus anayeweza kuuzwa kwa Pauni 52 milioni, Francisco Conceicao ni mmoja ya wachezaji wanaoweza kusajiliwa na timu hiyo.
Nyota huyo wa Juventus ameonyesha kiwango bora akiwa na Ureno na klabu yake, jambo lililoivutia sana Liverpool.
Morgan Rogers wa Aston Villa pia yuko kwenye rada za Liverpool baada ya kuonyesha kiwango bora kwa zaidi ya misimu miwili sasa. Hata hivyo, ada yake ya uhamisho inatarajiwa kuwa kubwa sana kutokana na urefu wa mkataba wake, hivyo inaweza kuwa ngumu kumpata.
Kwa upande mwingine, Liverpool inamtazama staa wa Bayern Munich, Michael Olise, ingawa naye gharama inaonekana kuwa kubwa.
Nyota huyo wa zamani wa Crystal Palace ameonyesha kiwango cha juu tangu ajiunge na vigogo hao wa Bundesliga, na haonekani kuwa na mpango wa kuondoka pia.
Bradley Barcola anaonekana kuwa chaguo rahisi zaidi kupatikana pamoja na Yan Diomande ambaye anawindwa pia na Manchester United.