MBONA IKO HIVI: Huu ni Mpira wa fitina, mpira wa corona

Saturday February 27 2021
namungo pioc

NIMEFUATILIA sakata la timu ya Namungo lililotokea nchini Angola na niseme kwamba kwa mara ya kwanza sikuamini kama nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi za Kusini mwa Afrika (SADC) wanaweza kufanyiana kitendo kama hicho, japo mechi baina ya timu zao ilishamalizika tangu juzi baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuamua zichezwe Dar.

Nilijiuliza hivyo kwa kuangalia mfano uliotokea Morocco. Katika mechi hizohizo za Ligi ya Mabingwa wa Afrika, mechi kati ya Mamelodi Sundowns na Wydad Casablanca ilifutwa kwa sababu zinazofanana na zile za mechi kati ya Petro Augusto na Namungo.

Tofauti ni kwamba Morocco iliwaambia Mamelodi ya Afrika Kusini irejee tu nyumbani kwa sababu sasa hivi kuna hofu kuhusu ukali wa kirusi cha corona kutoka Afrika Kusini na mechi yao itapigwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Waangola wangeweza kabisa kuwaambia Namungo kwamba wana wasiwasi wa kuingiziwa magonjwa na wasingependa mechi hiyo ichezwe. Namungo wangetoa taarifa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na CAF na mwishowe uamuzi wa busara ungefanyika.

Lakini hali ikawa tofauti. Namungo wakapelekwa kwenye maeneo ya hovyo na wakahudumiwa vibaya. Picha na video zilizotumwa huku nyumbani ziliwafanya baadhi ya Watanzania kukasirika kiasi cha kutaka kisasi kilipizwe.

Hiyo sio njia ambayo nataka mashabiki na klabu zetu zinazoshiriki katika mashindano ya kimataifa ziifuate. Tukifanya hivyo, tujue msemo wa majuto ni mjukuu utakuwa unatuhusu.

Advertisement

Mimi nataka tufanye nini?

Jambo la kwanza ni lazima TFF na CAF wakae chini na kuangalia suala zima la uendeshaji mpira katika nyakati hizi za ugonjwa wa corona. Wenzetu wa Ulaya tayari wamepiga hatua na kila nchi inajua ni wageni gani kutoka nje wanaruhusiwa kuingia na vipi ni vigezo na masharti vya abiria hao. Kuna utaratibu pia kuhusu ni abiria wa wapi na wapi wanaruhusiwa kuingia na kutoka ikoje. Mfano mzuri angalia kwa kocha mkuu wa Liverpool, Jurgen Klopp. Kocha huyo amefiwa na mama yake mzazi lakini ameshindwa kwenda kumzika. Kwanini? Kwa sababu kwa mujibu wa sheria za kusafiri kati ya mashirika ya ndege ya Ujerumani na Uingereza, safari hiyo ingemchukua hata siku 20 kumalizika. Kuna muda wa kukaa kwenye karantini Ujerumani na kuna muda wa kukaa karantini Uingereza. Ukijumlisha muda wote huo, Klopp akaamua bora abaki na Liverpool naye,

Tatizo la Afrika nyingi ya taarifa za namna hii hazipo wazi. Kabla Namungo haijaenda Angola, hatukujua kwamba taifa hilo linaichukulia Tanzania namna gani. Wala hakuna aliyeiona figisu hiyo ikijitokeza. Walikuja hapa washindani wa Simba na Namungo katika hatua za awali na hawakufanyiwa mchezo wowote usio wa kiungwana. Zipo taratibu za kupokea na kusindikiza wageni katika mazingira haya na hakukuwa na tatizo. Badala ya kupanga namna ya kulipiza kisasi kwa wenzetu, tuangalie ni kwa vipi tunaweza kuziepusha timu zetu na kile kilichotokea kwa Namungo. Kwa mfano, sasa tunajua kwamba Simba itakwenda Misri na itakwenda Sudan pia. Swali pekee la kujiuliza ni moja tu; tumejiandaaje na safari hizo?

Ni muhimu kuandaa wachezaji na viongozi kisaikolojia kwa lolote linaloweza kutokea wakiwa huko. Kama litatokea kwa Simba, Namungo tena au kwa wawakilishi wengine wa Tanzania katika mashindano yoyote ya kimataifa, tukio la Angola linapaswa kutumika kama mfano. Kazi kubwa zaidi inatakiwa kufanywa na CAF. Wao ndiyo wenye mashindano hayo na harakaharaka wanaweza sasa kuamua kuweka vigezo na masharti kwa timu zinazoshindana. Kwa sababu protokali za ugonjwa wa corona hufanywa na serikali za nchi na sio mashirikisho ya mpira ya nchi husika. Ni muhimu maelekezo yakatolewa kuonyesha ni kwa jinsi gani timu zitapaswa kufuata taratibu hizo za nchi.

CAF inaweza pia kupanga utaratibu wa mechi kuchezwa katika viwanja visivyo na wenyeji kama ambavyo Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (Uefa) limefanya kwa nchi zao. Kama kuna nchi zina utaratibu mgumu na zipo zenye utaratibu mwepesi, peleka mechi katika nchi nyepesi ili mpira uchezwe.

Pasipo kuingilia kati kwa CAF katika jambo hili, kunaweza kutokea mifarakano mingi barani Afrika.

Kama sio busara na uungwana wa Watanzania, unaweza kupata picha nini kingekuwa kinawasubiri Waangola mara tu walipofika Dar es Salaam.

Ni bahati, na hii ni imani yangu binafsi, kwamba mashabiki wa Namungo na wa mpira wa miguu wataamua kubaki na mapenzi yao kwa mchezo na binadamu wengine. Sisi hatuwezi kuiga Waangola. Sisi ni binadamu. Ndiyo sababu hatujawahi kutoa mtu kama Jonas Savimbi.

Ieandikwa na EZEKIEL KAMWAGA

[email protected] 

Advertisement