Mbogo aliingia Yanga na kuishia benchi

WAKATI wa maandalizi ya msimu wa 2012/13 wa Ligi Kuu Bara, simu ya beki katili kipindi hicho Ladislaus Mbogo ilikuwa bize akipokea simu za mabosi wa timu mbalimbali ikiwamo Yanga waliokuwa wakitaka huduma yake.

Mbogo kipindi hicho alikuwa anakipiga Toto Africans na alikuwa mmoja wa mabeki hatari wa kati ambaye alikuwa akiwatesa washambuliaji wa Yanga na Simba.

Ilikuwa kazi ngumu sana kumpita beki huyo kwani alikuwa imara sana kitu ambacho Yanga walitamani kumsajili ili kuimarisha safu yao ya ulinzi kwa kusaidiana na kina Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani na Mbuyu Twite.

Anasema haikuwa kazi ngumu kwake kutua Yanga kwani ilikuwa ni timu ambayo alikuwa anaipenda kitu ambacho kilifanya asaini mkataba na kuachana na timu nyingine zilizokuwa zikimhitaji.


YANGA HADI ULAYA

Anasema baada ya kutua Yanga alipata nafasi ya kwenda nchini Uturuki ambako waliweka kambi ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya wa 2012/13.

“Baada ya hapo sijawahi kwenda tena Ulaya, ile safari ilikuwa ya furaha sana kwangu kwani nilijifunza vitu vingi sana nikiwa Uturuki,” anasema.


ALIISHIA BENCHI

Anasema wakati anatua Yanga kwenye nafasi yao kulikuwa na mabeki wakali akiwamo Cannavaro na Yondani jambo lililofanya ushindani wa namba kikosi cha kwanza uwe mkubwa.

“Yanga sikupata msimu mzuri wa kucheza kwa sababu nafasi niliyokuwa nacheza kulikuwa na wachezaji kama watano na wote walikuwa wakali na isitoshe nilitumia muda mrefu kuuguza majeraha baada ya kufanyiwa matibabu nikajikuta mwaka mzima sijacheza,” anasema.

Anasema baada ya msimu kumalizika na mkataba wake kumalizika ndani ya Yanga alijiunga na Rhino Rangers ya Tabora lakini ilishuka daraja ndipo alirejea nyumbani Mwanza na kujiunga na timu yake ya zamani Toto Africans.

“Nashukuru kwa sababu katika vitu ambavyo Yanga walinifanyia ni matibabu mazuri kwani nilifanyiwa upasuaji ulienda vizuri kiukweli walinipa maisha, baada ya hapo nilikaa muda mrefu hadi msimu unaisha sikucheza,” anasema.


ALIENDA BURUNDI

Baada ya kuondoka Yanga, Rhino Rangers na hatimaye Toto Africans aliiwezesha kupanda tena daraja mwaka 2015 na baada ya kuisaidia kupanda daraja aliamua kuachana nao ndipo alitimkia Burundi alikojiunga na Olympic Star alikocheza nusu msimu.

“Nilicheza mzunguko wa kwanza nikarudi nyumbani mapumziko nikakuta Toto imeshuka tena daraja mwaka 2016 viongozi wakanishawishi tena kujiunga nao nikakubali tukaibakisha kwenye ligi wakaniacha tena,” anasema na kuongeza kwamba alirudi Burundi ingawa pia hakukaa sana akarudi kujiunga Toto na kushuka nayo daraja jumla hadi sasa iko daraja la nne wilaya ya Nyamagana.



KUACHA SOKA

Anasema baada ya Toto kushuka daraja alikata tamaa ya kuendelea kucheza soka na sasa anajishughulisha na uuzaji wa vifaa vya michezo.

“Toto ilinilea na nilitangaza jina langu pale kwahiyo iliposhuka kutoka Ligi Kuu na kuporomoka tena hadi la pili, nilikata tamaa ya mpira, nikaamua nifanye shughuli zangu nyingine huku nikicheza mpira wa kujifurahisha tu na maveterani.

“Nilipoachana na soka, niliamua nifanye shughuli zangu kwa sasa nauza vifaa vya michezo, nafanya mazoezi na timu yangu ya Mwanza Starehe Veterani na nafundisha pia vijana wadogo wa miaka tisa hadi 17,” anasema.


ANAOWAKUBALI

Anamtaja beki wa kati wa Yanga, Dikcson Job aliyesajiliwa msimu huu kutoka Mtibwa Sugar kuwa ni mchezaji anayemvutia kutokana na kiwango bora anachokionyesha kwa sasa akiwa na uwezo mkubwa wa kunusa hatari na kuilinda timu.

“Kuna madogo wanaokuja kama Job ni beki mzuri anayekuja na akiendelea na mwendelezo huo akajitunza vizuri basi atakuwa faida kwa nchi hii.

“Kuna beki wa Yanga, Yannick Bangala kwa namna anavyocheza ananifurahisha sana lakini kuna mtu kama Kelvin Yondani japo anaitwa mkongwe ila ni beki mzuri,” anasema.


IMEANDIKWA NA ANANIA KAJUNI NA DAMIAN MASYENENE