Mbeya City ina cha kujifunza
Muktasari:
- Timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, tangu ulipopanda Ligi Kuu msimu wa 2013-2014 iliweka heshima ya kumaliza nafasi ya tatu ikizidiwa na Yanga na Azam pekee.
LICHA ya kubaki salama Ligi Kuu ya NBC, Mbeya City inapaswa kujiuliza na kujifunza jambo msimu ujao ili kurejesha heshima yake iliyoiweka kwa miaka 10 nyuma katika medani za soka nchini.
Timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, tangu ulipopanda Ligi Kuu msimu wa 2013-2014 iliweka heshima ya kumaliza nafasi ya tatu ikizidiwa na Yanga na Azam pekee.
Kama haitoshi, msimu uliofuata wa 2014-2015, timu hiyo ilifanya kweli kwa kumaliza nafasi ya nne ikizidiwa na Yanga, Simba na Azam na kuwavuta mashabiki wengi ndani na nje ya Jiji la Mbeya.
Mafanikio hayo haikuwa tu heshima kwao na mashabiki, bali wadau wa soka nchini waliiona kama timu mojawapo ya kuleta mageuzi kwenye soka la Tanzania kutokana na msingi waliokuwa wameuweka.
Pamoja na mafanikio hayo, timu hiyo imepitia magumu ndani na nje ya uwanja ikiwamo mabadiliko ya uongozi wa mara kwa mara, timuatimua ya makocha na muingiliano wa kisiasa ulioiathiri kwa muda.
HISTORIA YAKE
Kabla ya kuwepo kwa timu hiyo, wazo lilitokea mwaka 2009 wakati wa michuano ya Shirikisho la Michezo kwa Serikali za Mitaa (Shimisemita), ambapo uongozi wa Halmashauri waliazimia kuwa na timu ya ushindani.
Wakati huo jiji hilo likiwa chini ya Mkurugenzi wake, Juma Idd aliyekuwa mdau na mpenda soka, timu ikaanza kushiriki mashindano ngazi ya Wilaya, Mkoa, ambapo haikufanikiwa kufikia malengo katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).
Hata hivyo, Halmashauri ililazimika kufikia malengo kwa kununua timu iliyoitwa Rhino ya mkoani Arusha ambayo ilikuwa Ligi Daraja la Kwanza (kwa sasa Championship) na kuipa usajili wa Mbeya City mwaka 2011.
Bada ya kukamilisha taratibu hizo, timu hiyo ilihamishiwa jijini Mbeya na kushiriki msimu mmoja tu Championship na kufanikiwa kupanda Ligi Kuu na kuweka historia mpya ya Jiji la Mbeya kuwa na timu kwenye ligi hiyo.
Baada ya kupanda Ligi Kuu, iliweka historia mpya ya kuwa timu ‘ndogo’ kudumu muda mrefu Ligi Kuu ikifanya hivyo miaka 10 mfululizo kabla ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023.
YASHUKA DARAJA
Baada ya kucheza Ligi Kuu kwa misimu 10 mfululizo, timu hiyo ilijikuta ikishuka daraja msimu wa 2022-2023 ilipomaliza nafasi ya 14 kwa pointi 31 na kuangukia hatua ya mtoano ‘play off’ dhidi ya KMC iliyomaliza nafasi ya 13 kwa pointi 32.
Katika msimu huo, Yanga ndio ilitwaa ubingwa ilipoongoza msimamo kwa pointi 78, Simba nafasi ya pili kwa pointi 73 na Azam nafasi ya tatu kwa pointi 59, huku Singida Fountain Gate ikifunga ‘Top Four’ kwa pointi 53.
Timu za Polisi Tanzania na Ruvu Shooting ndizo zilishuka daraja kwa kumaliza nafasi ya 15 na 16, ikiwa Polisi ilikusanya pointi 25 huku Ruvu Shooting ikiishia pointi 20.
Katika mtoano wa kwanza, Mbeya City matokeo ya jumla ilipoteza kwa mabao 3-2, ilianzia nyumbani ikishinda 2-1, huku mechi ya mwisho KMC ikashinda 2-0.
Mbeya City ilikutana dhidi ya Mashujaa iliyokuwa Championship, ambapo mechi ya kwanza iliyopigwa Lake Tanganyika, wenyeji Mashujaa walishinda mabao 3-1 na mechi ya marudiano jijini Mbeya, City ilitota bao 1-0 na kushuka rasmi daraja kwa kipigo cha jumla ya mabao 4-1.
MABADILIKO YA UONGOZI
Hadi sasa Emanuel Kimbe anaendelea kutajwa kuwa moja wa aliyekuwa Mtendaji Mkuu mwenye mafanikio makubwa kwa Mbeya City kufuatia matokeo iliyopata chini yake kwenye Ligi Kuu.
Kimbe akiwa CEO wa kwanza wa timu hiyo, aliiongoza kwa zaidi ya miaka 12, ambapo kwa mara ya kwanza wakicheza Ligi Kuu walimaliza nafasi ya tatu, msimu uliofuata walimaliza nafasi ya tatu.
Hata hivyo, mafaniko kwa kigogo huyo ni kuisimamia misimu 10 mfulululizo bila kushuka daraja hadi alipotangaza kuachia ngazi msimu wa 2022-2023 wakati timu inashuka daraja.
Baada ya kuachia ngazi, timu ilikabidhiwa kwa aliyekuwa Mchumi wa Halamashauri ya Jiji la Mbeya, Ally Nnunduma ambapo aliiongoza kwa mechi tisa ikiwa Championship na kushindwa kupanda daraja.
Hata hivyo, mipango ya Nnunduma ilionekana kuwa safi kwani msimu uliofuata wa 2023-2024 ilifanikiwa kurejea Ligi Kuu, ambapo aliiongoza mechi tatu akishinda mbili na sare moja baadaye kupata uhamisho.
Nnunduma baada ya mafanikio hayo alipandishwa cheo kuwa Kaimu Mkurugenzi Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wenye Ulemavu sehemu ya Sera, Utafiti na Ubunifu na kuhamishiwa jijini Dodoma.
Kwa sasa timu hiyo ipo chini ya Mtendaji Mkuu, John Kilua ambaye pia ni Afisa Mawasiliano na Uhusiano Jiji la Mbeya, ambaye amepambana kuinusuru na aibu ya kushuka daraja.
TIMUATIMUA MAKOCHA
Ukiachana na makocha zaidi ya 10 waliowahi kuinoa timu hiyo tangu ilipoanda daraja chini ya aliyekuwa Kocha wake, Juma Mwambusi anayeheshimika kikosini humo hadi sasa, msimu huu Mbeya City imeongozwa na makocha watatu.
Timu hiyo ilianza msimu chini ya Kocha Malale Hamsini aliyeipandisha daraja alipoachiwa jukumu na mtangulizi wake, Salum Mayanga kisha kutemwa kumvuta Mecky Maxime na kumaliza ligi chini ya Salum Mayanga.
Mbeya City iliangukia play off baada ya kumaliza nafasi ya 14 kwa pointi 30 na kukutana na ndugu zao, Tanzania Prisons iliyomaliza nafasi ya 13 kwa pointi 32 na kushinda kwa jumla ya mabao 2-0.
KAULI YA KOCHA
Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga, amesema haikuwa kazi rahisi kubaki salama akiwapongeza na kuwashukuru wachezaji, mashabiki na uongozi kwa umoja na ushirikiano.
Amesema matokeo hayo ni fundisho kwao katika kujiandaa na msimu ujao kuhakikisha anabadilisha kikosi pale palipo na upungufu haswa katika maeneo ya beki, kiungo na ushambuliaji.
“Lakini katika maboresho ni kuanza maandalizi mapema, ligi imebadilika lazima tuwe na kikosi chenye kuendana na mahitaji ya ligi kuanzia kimbinu na kiufundi, lazima tuje na mabadiliko.
“Ripoti itawasilishwa, kimsingi nashukuru kuibakiza timu Ligi Kuu baada ya kukabidhiwa kazi katika wakati mgumu, mashabiki na uongozi walitoa sapoti na tutarudi kivingine,” amesema Mayanga.
Kuhusu hatma yake kubaki au kuondoka, Mayanga amesema hilo bado ni mapema kwakuwa linahitaji mazungumzo ya pande zote akieleza kuwa uongozi ndio wanajua nafasi yake.
MSIKIE KIPA
Kipa wa timu hiyo, Soud Dondola amesema licha ya kusbiri matokeo ya mtoano ‘Play Off’ lakini ni kama malengo yao yamefikia kutoshusha timu akieleza kuwa maeneo yaliyoonekana kupwaya wahusika watayafanyia kazi.
Amewapongeza wenzake kikosini kutokata tamaa tangu walipoanza ligi licha ya changamoto walizopitia ndani ya uwanja, akieleza kuwa matarajio yao msimu ujao huenda wakafanya vizuri.
“Hata sisi wachezaji tutaenda kujitathimini kuhakikisha tulipokosea tunarekebisha, lakini kikubwa kila mmoja alijituma hadi timu kubaki salama kama ilivyokuwa malengo yetu,” amesema kipa huyo.
USHAURI WA MASHABIKI
Kiongozi wa mashabiki wa Mbeya City, Martin Geofrey amesema timu inahitaji mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji kutemwa kupisha wengine akieleza kuwa msimu huu ulikuwa wa mazoea.
“Lazima timu ije na mabadiliko baadhi watupishe kuanzia golini hadi ushambuliaji, tusirudie hii presha na badala yake tupambanie nafasi tatu za juu, uongozi lazima ufanye tathimini ya kina,” amesema Geofrey.