Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mazito yaibuka mastaa Ligi Kuu kubeti, vita ngazi zote makocha wafunguka -2

BETI Pict

Muktasari:

  • Uchunguzi wa Mwanaspoti kupitia mahojiano na wachezaji mbalimbali na viongozi umebaini kwamba sababu kubwa ni vipato vidogo kwa wachezaji, kukosa uzalendo kwa wachezaji na viongozi pamoja na kurubuniwa na wadau wakubwa wa kubeti ambao ni mashabiki maarufu mtaani kama ‘wawekezaji’.

JANA tulianza kuchapisha makala za ripoti ya kuangalizia jinsi wachezaji, viongozi na watu wao wa karibu wanavyojihusisha na suala la uchezaji kamari kwenye mechi za Ligi Kuu Bara, ambapo tuliona baadhi ya viongozi wa timu wanavyodiriki kushiriki ili kujipatia kipato, lakini jinsi hata wachezaji wanavyowatumia wake au wenza ama ndugu zao kubashiri na kuhusika kutengeneza matokeo. Leo endelea na sehemu inayofuata.


MAMBO NI MAZITO

Uchunguzi wa Mwanaspoti kupitia mahojiano na wachezaji mbalimbali na viongozi umebaini kwamba sababu kubwa ni vipato vidogo kwa wachezaji, kukosa uzalendo kwa wachezaji na viongozi pamoja na kurubuniwa na wadau wakubwa wa kubeti ambao ni mashabiki maarufu mtaani kama ‘wawekezaji’.

Mmoja wa wachezaji wa timu iliyoko kwenye nafasi tatu za chini kwenye msimamo kwa sasa amedokeza kuwa, “unakuta mtu mshahara wangu haufiki laki 5 lakini unasikia wenzako wamecheza na mkeka wamepata mpaka milioni 10 kwa pamoja. Na huwezi kuwashtaki kwavile ni wana ndio maana unakuta na wewe unatumia akili uishi.”

“Wewe ukitaka kujua huu mchezo ulivyo hata makampuni yenyewe yameshashtukia kwamba yanaumizwa, kuna timu kibao hizi nafasi za tano kushuka kwenye msimamo haziwekwi kabisa kwenye mikeka, fuatilia utagundua.” Hayo yaanadokezwa na mchezaji mmoja anayeweka wazi kwamba miezi michache iliyopita timu yake ilitoa adhabu kwa wachezaji kadhaa kwa tuhuma za kubeti lakini ikaishia kimyakimya ndani kwa kuhofia kuchafua taswira ya taasisi pamoja na kufungiwa maisha. Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini pia kwamba kuna baadhi ya viongozi wa timu wamekuwa wakibeti baadhi ya mechi kwa kuweka kiasi kadhaa cha fedha ili kupata fedha za kujiendesha na jambo hilo limekuwa likifanywa kwa siri kubwa kati yao na wachezaji.

BET 01

VITA NGAZI ZOTE

Viongozi wa klabu kadhaa za Ligi Kuu Bara wameanzisha mapambano ya wazi dhidi ya sakata hii. Mwenyekiti wa Singida Black Stars, Ibrahim Mirambo anasema: ”Sisi tunachukulia suala la nidhamu kwa uzito mkubwa. Kila mchezaji anasaini mkataba unaomzuia kujihusisha na hayo mambo na tukigundua, tunachukua hatua bila huruma.”

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani inaelezwa klabu za Simba na Yanga katika miezi ya hivikaribuni zimekuwa na utaratibu wa kufuatilia mawasiliano ya wachezaji wao, hasa wanapokuwa na mashaka na ufanisi wa baadhi yao hususani kwenye kuruhusu mabao ya wazi.

Wapo wachezaji wa klabu hizo kwa vipindi tofauti ambao waliwahi kushutumiwa, mfano mzuri kipa Beno Kakolanya na hapa anaeleza uzoefu wake.

“Nimewahi kushutumiwa kuuza mechi, haikuwa kweli bali zilikuwa ni hisia tu za kiongozi, siwezi kusema kwa undani zaidi ilivyokuwa,” anasema Kakolanya aliyewahi kuwika na Tanzania Prisons, Yanga, Singida FG na Namungo waliotemana nao hivi karibuni.

BET 02

TATIZO NI MAADILI?

Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Sunday Manara ‘Computer’, amezungumzia hali hiyo akisema: “Sisi wakati wetu tulicheza kwa ajili ya heshima na bendera ya timu, si pesa. Leo, wengi wameuza roho zao. Soka letu linakufa taratibu mikononi mwa tamaa.”

Kwa Manara, mabadiliko haya mabaya yanatokana na kuporomoka kwa maadili ya kijamii, kupungua kwa uzalendo wa kitaifa na mabadiliko ya kasi ya teknolojia ambayo yamerahisisha kila mtu kubeti kupitia simu yake ya mkononi tu.

Kiungo wa zamani wa Yanga na Twiga Sports, Credo Mwaipopo, ameenda mbali zaidi kwa kusema: “Siku hizi vijana wanaingia mazoezini huku ‘betting apps’ zikiwa bado wazi katika simu zao. Unafundisha mazoezi, lakini akili zao ziko kwenye odds.”

Kwa Credo, ufumbuzi wa kweli hauwezi kuwa adhabu tu, lazima kuwe na mpango mkubwa wa kufundisha nidhamu na kuwapa vijana motisha wa kitaaluma mapema kuanzia ngazi ya chini.

BET 06

MAKOCHA WATOA YA MOYONI

Patrick Aussems, aliyewahi kuinoa Simba, amefunguka kuwa: “Tatizo la Afrika ni mishahara midogo, ucheleweshaji wa malipo na maisha magumu. Mchezaji maskini ni rahisi kurubuniwa.”

Kwa upande wa kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyetemeshwa kibarua baada ya timu hiyo kufungwa mabao 5-1 katika Dabi ya Kariakoo ya Novemba 5, 2023 anasema, “mapambano haya ya kupambana na betting lazima yaanze kwenye akademi. Waambieni vijana mapema, heshima na taaluma hujengwa kutoka chini.”

Pia anasema ni vyema klabu zikajenga nidhamu ya kuwaelimisha wachezaji juu ya kanuni zilizopo ambazo zinakataza vitendo vyote vya upangaji matokeo ikijumuisha kubeti na rushwa kwani zinaharibu mchezo huo na kuwaharibia vijana wenye vipaji wanaotegemea soka kuendesha maisha yao ya kila siku.

Kocha wa KenGold, Omary Kapilima, amesema suala la kubeti linahitaji uchunguzi, kwa vile sio rahisi kulithibitisha lakini kama lipo wachezaji wanajiondoa wenyewe kwenye ushindani. “Sina utaalamu sana na naamini kama yapo basi yanafanywa kwa siri kubwa, hivyo kamati iundwe kuchunguza,” anasema Kapilima, staa wa zamani wa Yanga na Mtibwa Sugar akiongeza kuwa;

“Ki michezo sio jambo zuri kwani inakwamisha juhudi kubwa za uwekezaji lakini pia nguvu kazi ya makocha wanawekeza nguvu kiufundi lakini wanaangushwa na watu wachache kwa hisia zao ovu za kuipa timu matokeo mabaya.”

Kocha wa Pamba Jiji ambaye aliwahi kutamba na Yanga, Fred Felix ‘Minziro’ anasema ni tuhuma ambazo zinazungumzwa na kuna viongozi walikaririwa kuwa na ushahidi ili kuepuka minong’ono ni vyema mamlaka husika zikasimama kidete kuzuia hili.

“Kubeti huenda ukawa ni mchezo mchafu unaofanywa na watu, kinachotakiwa hapa ni uthibitisho wa wazi kutoka kwa mamlaka husika mambo ya kuzungumzwa mdomoni hayasaidii zaidi yanaendelea kudidimiza mpira wetu.

“Mpira una uwekezaji mkubwa, hauwezi kuangushwa na watu wachache, kanuni haziruhusu wachezaji wala viongozi wanaojihusisha na mpira kufanya suala kama hilo ili kudhibiti ni kutoa mfano kwa kuwaweka wazi hao wanaodhaniwa wanafanya hivyo,” anasema Minziro.

BET 03

BOSI WA WAAMUZI: TULETEENI

Waamuzi wamekuwa wakituhumiwa kubeti idadi ya kadi za njano na nyekundu kwenye mechi za Ligi Kuu Bara. Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Nassoro Hamduni, amesema kubeti ni utashi na msukumo wa mtu binafsi, lakini hadi mambo yameanza kutoka basi kuna jambo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Hamduni amesema wao kama viongozi wa Shirikisho wakifuata sheria za soka kwa mujibu wa FIFA klabu haziruhusiwi kujihusisha na mambo ya kamari, hivyo kama kuna wadau wanafahamu hilo wanawakaribisha kuwafahamisha.

“Sijawahi kupokea taarifa yoyote inayoashiria waamuzi wangu kubeti lakini kama yameanza kuzungumzwa huenda kuna watu wanafahamu hilo, tunawakaribisha, ofisi zetu zipo wazi ili tulifanyie kazi kwa uharaka,” amesema na kuongeza:

“Kuna msemo unasema lisemwalo lipo na kama halipo laja, hivyo kama kamati tutatoa macho kwenye hilo lakini pia wadau na waamuzi wenyewe tushirikiane kukemea suala hili sio zuri kwa ukuaji wa mpira wetu.”


‘HAKUNA MALALAMIKO BODI YA LIGI’

Mamlaka za soka hapa nchini, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), msimamo wao ni katika kusimamia kanuni za ligi, hivyo yeyote anayekutwa na hatia, adhabu inamuhusu. Kanuni ya 40 (6) ya Ligi Kuu Bara toleo la 2024, inasema: “Ni marufuku kwa kocha, mchezaji, kiongozi au ofisa wa mchezo kushiriki michezo ya kubashiri (betting). Kocha, mchezaji, kiongozi au ofisa wa mchezo atakayekiuka, atafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu au Kamati ya Maadili ya TFF.”

Ofisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda amesema wamekuwa wakisikia tu tuhuma za upangaji matokeo na kuuza mechi lakini hakuna timu wala mtu aliyefikisha mezani kwao malalamiko rasmi, hivyo hawawezi kuchukua hatua yoyote. Hata hivyo, Boimanda amesema kanuni za Ligi Kuu Bara zinaelezea adhabu ya atakayekutwa na hatia za upangaji matokeo lakini pia kama Takukuru ikiwafikishia uthibitisho wowote, hawasiti kuufanyia kazi kwa mujibu wa kanuni.

“Tumekuwa tukisikia tu na kuona mitandaoni hizo tuhuma za upangaji matokeo, lakini sisi kama Bodi hatujapata malalamiko rasmi, kama hali hiyo ipo na kuthibitika Takukuru watatufikishia kwa ajili ya sisi upande wetu tuchukue hatua kinanuni.” anasema Boimanda.

TPLB inafahamu kwamba kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa msimu, kumekuwa na matukio mengi yanayohusishwa na masuala ya upangaji matokeo, hivyo wapo macho kufuatilia miendeneo ya ligi zinavyochezwa na ikibainika kuna udanganyifu, hatua kali zitachukuliwa.

“Kwa sababu inafahamika kuwa ushindani na msukumo umeongezeka zaidi katika kipindi hiki na klabu zinafanya jitihada za kutimiza malengo yao ya msimu, Bodi imeongeza nguvu katika usimamizi wa michezo hiyo ili msukumo huo uzae burudani viwanjani badala ya kusababisha uvunjifu wa Kanuni za Ligi na sheria za mpira wa miguu.

“Ni wajibu wa kila mdau wa Ligi hiyo kuhakikisha anafuata Kanuni za Ligi ikiwemo kujiepusha na kukumbusha wengine kutojihusisha na vitendo vyovyote vinavyoashiria upangaji wa matokeo.

“Bodi ya Ligi Kuu Tanzania itachukua hatua kali za kikanuni kwa kila mdau atakayebainika na kuthibitika amejihusisha kwa namna yoyote na upangaji wa matokeo kwa sababu jambo hilo ni katika mambo yanayoweza kushusha hadhi ya Ligi. Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inawatakia kila la kheri wadau wote wa Ligi hiyo kuelekea michezo iliyosalia,” amesema.

BET 04

KAULI YA TAKUKURU

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Manyara, Bahati Haule amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio la kipa wa Fountain Gate, John Noble.

Haule amesema baada ya kupokea taarifa hiyo wanaendelea na uchunguzi na kupitia vielelezo kabla ya kukamilisha. Amesema wanajiridhisha kisha wanaingia kwenye hatua ya awali ya uchunguzi kisha wanakusanya vielelezo na kuhoji mashahidi.

Ameendelea kusema wakishakusanya vielelezo na kuhoji mashahidi watachambua taarifa nzima kupitia ushahidi walionao kisha watatoa taarifa. “Tukishamaliza kufanya uchunguzi wa tukio hilo tutatoa taarifa juu ya suala hilo, ila kwa sasa bado tupo kwenye hatua za mbele za uchunguzi,” amesema Haule. Aprili 21, 2025, kipa wa Fountain Gate, John Noble, alijikuta kwenye shutuma za kucheza chini ya kiwango na kusababisha kuruhusu mabao yaliyoonekana kuwa rahisi wakati timu hiyo ikifungwa nyumbani 4-0 na Yanga. Sakata hilo la Noble, limeifanya Fountain Gate kumpeleka Kamati ya Maadili ya klabu hiyo, kwa lengo la kumuhoji kutokana na makosa mawili aliyofanya ya kuruhusu mabao hayo. Mbali na tukio la Fountain, kumekuwa na tuhuma pia zikihusisha klabu ya Tabora United na Pamba Jiji. Ambazo bado mamlaka hazitoa ufafanuzi wa kinachoendelea zaidi ya kusisitiza wanafanyia uchunguzi.


TUKIO LA ZANZIBAR

Kashfa ya upangaji matokeo imepamba moto baada ya klabu ya Junguni United inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar kutangaza kwa mshtuko mkubwa imewasimamisha wachezaji saba kwa tuhuma za kubeti na kupanga matokeo.

Salum Athumani ‘Chubi’, Ramadhan Ally Omar ‘Matuidi’, Abdallah Sebastian, Danford Moses Kaswa, Bakari Athumani ‘Jomba Jomba’, Rashid Abdalla Njete na Iddi Said Karongo ni majina yaliyotajwa hadharani.

Hatua hiyo ilizua mjadala mzito kwa sababu si jambo la kawaida kuona klabu ikiamua kuchukua hatua kali bila kuogopa.

Lakini zaidi ya hayo, tukio hili lilifichua ukweli mchungu, kubeti haipo tena kwenye hisia tu, bali imepenya hadi katika mishipa ya uchezaji wenyewe.

BET 05

HALI ILIVYO AFRIKA/ULAYA

Katika miaka ya hivi karibuni, kashfa kama hizi zimeitikisa Kenya, Ghana na Afrika Kusini. Wapo wachezaji Kenya, ambao waliingia matatani baada ya kuhusishwa na upangaji matokeo. Mwaka 2018, Ghana ilikumbwa na kashfa kubwa ya rushwa katika soka iliyofichuliwa na mwandishi wa uchunguzi Anas Aremeyaw Anas kupitia video maarufu iitwayo “Number 12”.

Katika ile video, viongozi wakubwa wa soka (akiwemo Rais wa Chama cha Soka cha Ghana, Kwesi Nyantakyi) pamoja na maofisa wa waamuzi, walinaswa wakipokea rushwa ili kupanga matokeo ya mechi.

Baada ya kashfa hiyo, Serikali ya Ghana ilivunja rasmi Shirikisho la Soka Ghana. Mashindano yote ya Ligi Kuu nchini humo yalisimamishwa kwa muda kwa sababu ya uchunguzi na ukarabati wa mfumo. FIFA ililazimika kuingilia kati kuisaidia Ghana kuunda Kamati Maalumu kusimamia soka la nchi hiyo hadi hali ilipotengemaa.

Afrika Kusini nako ilishuhudia maelfu ya mashabiki wakikosa imani na ligi yao baada ya tuhuma nzito za upangaji mechi.

Nchini Kenya, Machi 27, 2025, Shirikisho la Soka la nchi hiyo (FKF) lilianzisha uchunguzi juu ya kipa wa Kakamega Homeboyz, Patrick Matasi aliyetuhumiwa katika upangaji wa matokeo.

Matasi alianza kuchunguzwa baada ya kusambaa kwa video ikimuonesha mtu mmoja ambaye hakujulikana ni nani akizungumza na kipa huyo wa kimataifa wa Kenya juu ya kupanga matokeo. Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), baada ya kuwepo kwa tuhuma hizo, Matasi amesimamishwa kwa siku 90 kupisha uchunguzi huo.

Juni 2024, Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) lilifungia watu 13, wakiwemo waamuzi 10, mchezaji mmoja, na wasimamizi wawili kwa kushirikiana katika kupanga matokeo baada ya kuhongwa na watu wa kubeti.

Nje ya mipaka ya Afrika, hali ipo hivyo pia na tayari kuna wachezaji wamekutwa na hatia wakakumbana na kibano. Pale England, mchezaji wa kimataifa wa taifa hilo, Ivan Toney alifungiwa miezi minane baada ya kukutwa na hatia ya kujihusisha na masuala ya kubeti, akifanya hivyo mara 232 kati ya mwaka 2017 hadi 2021.

Kiungo wa Newcastle United, Sandro Tonali ni miongoni mwa wachezaji wengine waliokutwa na hatia hivi karibuni baada ya kujihusisha na masuala ya kubeti.

Tonali raia wa Italia, alikubali makosa na kujisalimisha mwenyewe kwa mamlaka hali iliyosababisha apunguziwe adhabu kwa kupewa onyo tu na faini ya Pauni 20,000, lakini amepewa kifungo cha miezi miwili cha kutojihusisha na soka ila kitakuwa hai ikiwa tu atarudia tena.