MASTORI YA OSCAR: Kwanini Ofisa Habari wa klabu amzidi hadi Rais wa nchi kuongea?

Aliyekuwa Msemaji wa Yanga, Haji Manara alipowasili kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa katika kilele cha Wiki ya Mwananchi. Picha na Yanga

MOJA kati ya shida kubwa za maofisa habari wa klabu zetu ni kuongea sana. Ni rahisi sana kumuona ofisa habari wa Simba anakwenda kwenye chombo cha habari kuzungumzia timu kwa saa tatu.

Ni jambo la kawaida kabisa kumuona ofisa habari wa Yanga akienda kufanyiwa mahojiano juu ya klabu yake kwa saa tatu. Kuna uwezekano mkubwa tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aingie madarakani hajawahi kuhutubia popote kwa zaidi ya saa mbili.

Kuna uwezekano mkubwa tangu Rais, Mama Samia Suluhu Hassan aingie madarakani ukiachilia mbali hotuba yake bungeni wakati anaingia tu mzigono, naye hajawahi kuhutubia mahali popote kwa zaidi ya saa mbili.

Ofisa habari wa Yanga anawezaje kufanya hivyo? Inashangaza. Ofisa habari wa Simba anawezaje kufanya hivyo? Unabaki kushangaa tu. Wenzetu Ulaya na mahali kwingine ambako watu wameendelea msemaji wa mkuu wa mambo ya utawala na uongozi ni ofisa mtendaji mkuu wa klabu.

Msemaji mkuu wa mambo yote ya timu ni kocha mkuu. Na siyo kwamba Arsenal FC hawana ofisa habari. Siyo kwamba Manchester United haina ofisa habari. Wapo lakini kazi yao siyo kuzungumza kila siku. Wapo lakini kazi yao siyo kuzungukia leo chombo hiki cha habari, kesho kile. Hapa ndipo tofauti yao inapoonekana.

Ofisa habari asipozungumza kwa muda mrefu uwezekano wa kupunguza makosa ni mkubwa. Wao siku hizi ndiyo wanaotoa habari za wachezaji majeruhi. Wao ndiyo wanaozungumzia habari za udhamini. Wanazungumzia habari za kuvunjika kwa mikataba ya mchezaji.

Haya hayapaswi kuwa majukumu yao. Kwa sababu wanaongea sana ndiyo maana utawasikia wanakashifiana klabu moja na klabu nyingine. Ndiyo maana wanachambana ofisa habari mmoja na mwingine. Wamejipa majukumu makubwa mno. Hata huu mtindo wa kuhamasisha watu kuja uwanjani sijui umetoka wapi. Ukishakuwa na timu bora watu wanapaswa kuja tu wenyewe.

Watu wa kitengo cha masoko na uhamasishaji wanapaswa kufanya kazi yao vizuri huku ofisa habari akitulia kabisa. Tuko kwenye nchi ambayo kuwa ofisa habari wa klabu kwa sasa ni kama kuwa mtendaji mkuu. CEO wa klabu pengine watu hata hawamjui kwa sababu ofisa hahari anapiga mdomo kila siku.

Badala ya kupata maoni ya kiufundi kutoka kwa kocha au wachezaji, siku hizi tunapata tambo za maofisa habari. Mpira wetu unakuza zaidi siasa kuliko sayansi ya mpira. Kama ofisa habari angekuwa anaongea kwa muda mfupi tungepunguza makosa mengi.

Haiwezekana kuhamasisha tu watu kuja uwanjani mahojiano yawe ya saa tatu redioni. Haiwezekani kuzungumzia ushindi tu wa jana ofisa habari azungumze kwa saa tatu redioni.

Nafasi ya ofisa habari ilikuwa na hadhi ya chini sana kabla ya Jerry Muro na Haji Manara kuja na zama zao. Huko nyuma kumewahi kuwa na maofisa habari wengi tu, lakini hawakuwa na ushawishi mkubwa kama zama za Muro na Manara.

Ni zama hizi pia ambazo hawa maofisa habari walianza kuongea sana. Ni nyakati hizi pia ndizo watu walianza kuvunjiana heshima. Dharau, kashfa na matusi yalitawala. Ukiniuliza ni nini? Jibu langu ni rahisi tu - hawa watu walikuwa wanaongea sana na vyombo vya habari.

Hawa watu kila siku walikuwa na mikutano na waandishi wa habari. Ofisa habari ni ofisi ndogo tu ndani ya klabu, lakini namna wanavyoichukulia utadhani wao ndiyo watendaji wakuu. Hata Rais wa nchi hafanyi hotuba za saa tatu. Waziri Mkuu hazunguki kwenye vyombo vya hahari kila siku. Wasemaji wa mpira wetu kila siku wako mtaani na vyombo vya habari. Mtendaji mkuu wa Klabu ya Simba ni Barbara Gonzalez, lakini hajawahi kwenda kwenye redio kuzungumza kwa saa tatu. Andre Mtine ni mtendaji mkuu wa Yanga tangu atangazwe hajawahi kwenda kwenye redio yoyote. Lakini ofisa hahari tayari ameshaongea na redio karibu zote.

Pale Simba ukitaka hadi habari za kocha mkuu kupewa mkataba wa muda mrefu, msemaji wake ni ofisa habari. Nadhani umefika wakati wa kuondoka kwenye zama hizi. Kazi ya ofisa habari haipaswi kuwa ni kuongea na vyombo vya habari kila siku.

Ofisa habari anapaswa kuongea kidogo sana kwa sababu chochote kile anachozungumza ni maagizo kutoka kwa mtendaji mkuu. Kazi kubwa ya ofisa habari inapaswa kuwa ni kutoa taarifa kwa wapenzi na mashabiki, lakini sio kwa kuongea kila siku.

Kama ni mambo ya kiutawala atamleta mtendaji mkuu kuzungumza. Kama ni mambo ya kiufundi atamleta kocha mkuu kuzungumza. Ni rahisi tu. Mambo ya kuwaambia watu PSG ikija Uwanja wa Mkapa imefungwa tuyaondoe. Hayana maana. Zama zake zimepita. Mambo ya kusema Yanga ina uwekezaji mkubwa kuliko Al Hilal tuyaache kwa sababu zama zake zimepita.

Maofisa habari wetu wasiongee sana, wauache mpira uongee uwanjani. Kama hata Rais wa nchi hana hotuba ya saa tatu wewe ofisa habari unaanzia wapi? Vijana wetu wengi wanajipa majukumu ambayo kimsingi sio yao. Siku hizi wanaongea sana hadi sauti zinawakauka.

Tuleteeni CEO aje kuzungumza jambo la kiutawala. Tuleteeni kocha mkuu aje kuzungumzia mambo ya kiufundi. Maofisa habari acheni kufanya kazi zisizo zenu. Punguzeni safari za redioni kila siku. Punguzeni kuongea na vyombo vya habari kila siku.