Mastaa wa soka wenye mivinyo inayotesa sokoni Ulaya

Muktasari:
- Supastaa Lionel Messi baada ya kubeba mataji kibao ya La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Dunia na mengine mengi ikiwamo kushinda Ballons d Or mara nane, ambayo ni rekodi, mkali huyo sasa anataka kuacha kumbukumbu nyingine kwa mashabiki wake.
LONDON, ENGLAND: SOKA limejaa kumbukumbu nyingi, tamu na chungu. Na kwenye hilo, moja linaweza kuwasukuma wanasoka kufanya kitu ambacho wanaamini kitabaki kwenye kumbukumbu njema kwa mashabiki.
Supastaa Lionel Messi baada ya kubeba mataji kibao ya La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Dunia na mengine mengi ikiwamo kushinda Ballons d Or mara nane, ambayo ni rekodi, mkali huyo sasa anataka kuacha kumbukumbu nyingine kwa mashabiki wake.
Messi baada ya kuwachachafya sana mabeki wa timu pinzani uwanjani, amehamishia makali kwenye kuzipondaponda zabibu kwa ajili ya kutengeneza mvinyo.
Kwa maana hiyo, Messi ameamua kufuata nyayo za wanasoka wengine maarufu kama Andres Iniesta, David Ginola, David Silva na Andrea Pirlo ambao wana mivinyo inayotamba sokoni.
Kwenye chupa ya mvinyo wa Messi kuna lebo iliyoandikwa GOAT 10 Lionel Collection, ambapo bei ya chupa moja ni Pauni 53, sawa na fedha ya Kitanzania, Sh190,864.
Hii hapa orodha ya masupastaa wa soka wenye mivinyo sokoni na bei zake:
Andrea Pirlo - Pratum Coller Nitor IGP Montenetto (Pauni 23)
Kiungo fundi wa boli, Mtaliano Andrea Pirlo alikuwa matata uwanjani na kuhamishia ubora wake huo kwenye chupa ya mvinyo, ambapo mvinyo wake mweupe umeripotiwa kukimbiza sana sokoni. Ladha ya mvinyo huo imeelezwa kuwa ni ya kibabe ikiwa na zabibu halisi. Pirlo anamiliki ekari 15 za zabibu na amekuwa akitengeneza chupa 30,000 za mvinyo kwa mwaka. Kama ilivyokuwa kwenye utulivu wake wakati mpira ulipokuwa kwenye miguu yake, ndivyo mvinyo wake ulivyo, ambapo huko sokoni, chupa moja ya mvinyo wa Pirlo ni Pauni 23, zaidi ya Sh 80,000 za Kitanzania.
David Silva - Tameran Malvasia Volcanica 2022 (Pauni 41)
Fundi mwingine wa soka, Mhispaniola, David Silva naye ni miongoni mwa mastaa ambao wameamua kuwapa kumbukumbu ya kipekee mashabiki wao kwa kutengenezea mvinyo ili waburudike. Staa huyo aliyenyakua mataji manne ya Ligi Kuu England alipokuwa akikipiga kwenye kikosi cha Manchester City, mvinyo wake unaripotiwa kufanya vizuri kutokana na kutengenezwa kwa ustadi mkubwa huku ukiwa na kiungo cha vanilla ndani yake. Hata hivyo, David Silva hayupo peke yake, ameungana na mtengenezaji wa mvinyo, Jonatan Garcia na mvinyo wao unaitwa Bodegas Tameran, huku chupa moja ikiuzwa kwa Pauni 41, zaidi ya Sh140,000 za Kitanzania.
David Ginola - Coste Brulade Provence Rose 2023 (Pauni 14)
Wakati anatamba kwenye kikosi cha Tottenham Hotspura kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, shughuli ya mkali David Ginola ilikuwa matata uwanjani. Staa huyo aliwafanya mabeki wa timu pinzani kile alichokuwa akitaka na kuwatasa makipa kwa mabao ya kifundi. Mkali huyo wa Mfaransa anamiliki mvinyo wake ambao umetengenezwa kwa ustadi mkubwa kiasi cha kushinda tuzo za ubora kwenye orodha ya mivinyo ya kibabe. Mvinyo wa Ginola unaitwa Coste Brulade na chupa moja imeripotiwa kuuzwa Pauni 14, zaidi ya Sh50,000 ya Kitanzania, huku ukiwa mvinyo wenye bei rahisi zaidi katika orodha hii ya mivinyo ya mastaa wa soka.
Andres Iniesta - Corazon Loco Tinto Joven 2022 (Pauni 15)
Kama uliwahi kumwona Andres Iniesta akicheza soka uwanjani, hakika ulikuwa mmoja waliokuwa wakipokea burudani tosha kutoka kwa mkali huyo wakati mipira ilipokuwa kwenye miguu yake. Iniesta alitamba kwelikweli kwenye kikosi cha Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, akifanikiwa kubeba mataji kibao. Wakati sasa nyakati za kutamba uwanjani zikiwa zimemtupa mkono, Iniesta sasa anakimbiza kwa chupa yake ya mvinyo, inayoitwa Corazon Loco Tinto Joven 2022. Corazon Loco maana yake ni moyo wa kichaa, kwa tafsiri isiyosahihi sana, huku chupa moja ikiuzwa Pauni 15, zaidi ya Sh54,000 za Kitanzania.
Lionel Messi - Sicily Syrah IGT (Pauni 53)
Baada ya kutamba kwenye soka, akibeba mataji kibao na kubamba dili za kulipwa mishahara ya kibosi, mkali wa Kiargentina, Lionel Messi amehamishia makali hayo kwenye utengenezaji wa mvinyo, huku akiuza mvinyo wake kwa gharama kubwa kutoka kwenye orodha ya mivinyo inayomilikiwa na wanasoka mahiri. Messi amehakikisha mvinyo wake wa GOAT 10 Syrah unakuwa na ladha ya kipekee kabisa, huku ukidaiwa kuwa na kilevi asilimia 14. Kinachovutia ni kwamba mvinyo huo wa Messi unatengenezwa kwa zabibu zinazozalishwa Italia, wakati yeye ni mzaliwa wa Argentina na amekulia na kusema sehemu kubwa ya maisha yake ya soka huko Hispania. Chupa moja ya mvinyo wa Messi inakaribia Sh200,000.