Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mastaa hawa wametoa gundu la mabao Bara

Muktasari:

  • Wakati Ligi hiyo ikisimama kwa sasa, Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mastaa waliofunga mabao ya kwanza na kutoa gundu, baada ya kuandamwa na ukame wa kutokufunga kwa kipindi cha muda mrefu, tangu msimu uliopita wa 2024-2025, ulipotamatika.

LIGI Kuu Bara imesimama kupisha kalenda ya mechi za kimataifa za FIFA, ambapo hadi sasa licha tu ya kuchezwa raundi tatu kwa baadhi ya timu, ushindani umekuwa mkubwa msimu huu wa 2025-26, jambo linaloonyesha mapema utakuwa mzuri zaidi.

Wakati Ligi hiyo ikisimama kwa sasa, Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mastaa waliofunga mabao ya kwanza na kutoa gundu, baada ya kuandamwa na ukame wa kutokufunga kwa kipindi cha muda mrefu, tangu msimu uliopita wa 2024-2025, ulipotamatika.


ANDREW SIMCHIMBA (MTIBWA SUGAR)

Baada ya kufunga bao moja katika ushindi wa Mtibwa Sugar wa mabao 2-0, dhidi ya Fountain Gate, Septemba 28, 2025, nyota wa kikosi hicho, Andrew Simchimba ameondoa ukame wa siku 1,046, tangu mara ya mwisho alipofunga katika Ligi Kuu Bara.

Nyota huyo aliyejiunga na Mtibwa kwa mkopo msimu huu akitokea Singida Black Stars iliyomsajili akitoka Geita Gold ambayo inashiriki Ligi ya Championship, kabla ya kufunga bao hilo, mara ya mwisho alifunga wakati akiwa na kikosi cha Ihefu.

Kabla ya bao hilo la Mtibwa Sugar, Simchimba aliifungia Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars wakati kikosi hicho kilipochapwa mabao 2-1, dhidi ya maafande wa Polisi Tanzania, katika pambano lililopigwa jijini Mbeya, Novemba 17, 2022.

Simchimba alikuwa mfungaji bora wa Championship kwa msimu wa 2024-25, akiichezea Geita Gold baada ya kufunga mabao 18, sawa na Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar na Abdulaziz Shahame 'Haaland' aliyekuwa TMA FC, ingawa kwa sasa amehamia Namungo.

Kama utakuwa umesahau pia, Simchimba ni miongoni wa nyota waliowahi kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), msimu wa 2022-2023, alipofunga mabao saba, akiwa na kikosi cha Ihefu kwa sasa Singida Black Stars.

Nyota huyo aliiwezesha pia Geita Gold kumaliza ya nne kwa kuwa na pointi 56 na kucheza mechi za 'playoff' ili kupanda Ligi Kuu Bara ambako ilikwama baada ya kuchapwa kwa jumla ya mabao 4-2 na Stand United (iliyomaliza msimu ya tatu kwa pointi 61).


YASSIN MGAZA (DODOMA JIJI)

Bao alilofunga katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-0, dhidi ya Coastal Union, kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Septemba 27, 2025, limemfanya Mgaza kuhitimisha ukame wa siku 289, tangu mara ya mwisho alipofunga, Desemba 12, 2024.

Mgaza ni mshambuliaji anayekumbukwa zaidi akiwa na kikosi cha KMKM msimu wa 2022-23, alipoibuka mfungaji bora wa Ligi ya Zanzibar, baada ya nyota huyo kuchangia mabao 25, akifunga 17 na kuasisti manane kwenye mechi 25 kati ya 30.

Mgaza alijiunga na KMKM akitokea Mbuni ya Arusha ambayo kwa sasa inashiriki Ligi ya Championship, ingawa kwa msimu huo ilikuwa Ligi Daraja la Pili, First League, ambapo alionyesha kiwango kizuri kilichoishawishi KMKM kuihitaji saini yake.

Akiwa na Mbuni, Mgaza alihusika katika jumla ya mabao 22 kwa msimu mzima kwenye mechi 16 alizocheza baada ya kufunga mabao 16 na kuasisti mengine sita, ingawa kiwango hicho bora kwake alikiendeleza hadi alipojiunga na kikosi cha KMKM.

Baada ya hapo, mabosi wa Dodoma Jiji wakamsajili kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji kwa msimu wa 2023-24 na kubeba matarajio makubwa ndani ya kikosi hicho, lakini alikwama akiishia kufunga mabao matatu tu kwa msimu mzima.

Msimu uliopita wa 2024-25, Mgaza alifunga bao moja katika kichapo ilichokipata Dodoma Jiji cha mabao 2-1, dhidi ya Singida Black Stars, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Liti Singida, Desemba 12, 2024.


DARUWESHI SALIBOKO (KMC FC)

Saliboko ndiye mchezaji aliyeandika historia ya kufunga bao la kwanza la Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-26, katika ushindi wa timu hiyo wa 1-0, dhidi ya Dodoma Jiji, pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge, Septemba 17, 2025.

Bao hilo ni la kwanza kwa mchezaji huyo ambaye mara ya mwisho kabla ya hapo, alifunga pia katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-1, akifunga yote dhidi ya Tanzania Prisons, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Oktoba 26, 2024.

Katika mechi hiyo, Saliboko alifunga mabao hayo katika dakika ya 15 na 57, huku lile la maafande wa Prisons likifungwa na nyota wa timu hiyo, Oscar Mwajanga katika dakika ya 74, hivyo bao alilofunga na Dodoma Jiji limemfanya kuhitimisha ukame wa siku 326.


FABRICE NGOY (NAMUNGO FC)

Nyota huyu Mkongomani, hadi sasa ndiye aliyefunga bao bora la Ligi Kuu, baada ya kufunga kwa kubinuka 'tiki-taka' au 'bicycle kick', katika ushindi wa timu hiyo wa 1-0, dhidi ya Tanzania Prisons, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Septemba 21, 2025.

Bao hilo alilifunga kwa ustadi wa hali ya juu dakika ya 62 na kuhitimisha ukame wa siku 164, tangu mara ya mwisho nyota huyo alipofunga katika Ligi Kuu Bara, katika sare ya kikosi hicho ya mabao 2-2, dhidi ya JKT Tanzania, Aprili 10, 2025.

Ngoy alijiunga na Namungo msimu wa 2023-2024, akitoka Kitayosce iliyobadilishwa jina na kuitwa Tabora United na sasa TRA United, baada ya kuifungia mabao 15 ikiwa Ligi ya Championship, nyuma ya kinara, Edward Songo wa JKT Tanzania aliyefunga 18.

Mshambuliaji huyo alitua nchini kwa mara ya kwanza msimu wa 2022-23, akitokea Real Nakonde FC ya Zambia, ambako msimu uliopita wa 2024-25, akiwa na kikosi hicho cha Namungo 'Wauaji wa Kusini' alifunga mabao mawili ya Ligi Kuu Bara.


OSCAR MWAJANGA (TZ PRISONS)

Nyota huyu wa zamani wa Mbeya Kwanza, amefuta ukame wa siku 162, baada ya kuifungia Prisons bao moja pekee na la ushindi wa 1-0, dhidi ya KMC, katika pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Septemba 27, 2025.

Bao hilo alifunga katika dakika ya 14, akipokea pasi iliyopigwa na Salum Kimenya, ambapo kabla ya hapo mara ya mwisho kwa nyota huyo kufunga ilikuwa ni ushindi pia wa timu hiyo wa mabao 3-2, dhidi ya maafande wenzao wa JKT Tanzania Aprili 18, 2025.


FEISAL SALUM 'FEI TOTO' (AZAM FC)

Bao moja alilofunga kiungo mshambuliaji nyota wa Azam, Feisal Salum 'Fei Toto', katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-0, dhidi ya Mbeya City, Septemba 24, 2025, limemfanya kuhitimisha ukame wa mabao, baada ya kupita siku 297 za kutofunga.

Katika mechi hiyo, Feisal alifunga bao ambalo ni la pili kwa Azam dakika ya 46, akipokea pasi ya Baraket Hmidi, baada ya Nassor Saadun kukitanguliza kikosi hicho katika dakika ya 32, akipokea mpira uliopigwa na kiungo nyota, Abdul Suleiman 'Sopu'.

Kabla ya bao hilo, mara ya mwisho kwa nyota huyo kufunga ilikuwa ni katika ushindi wa Azam wa mabao 3-1, dhidi ya Dodoma Jiji ugenini, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Desemba 1, 2024, hivyo kuhitimisha rasmi siku 297.


HABIBU KYOMBO (MBEYA CITY)

Mshambuliaji huyo amekuwa wa kwanza kuifungia Mbeya City bao la Ligi Kuu Bara tangu ipande msimu huu wa 2025-26, baada ya kushuka msimu wa 2022-23, ambapo kikosi hicho kilishinda 1-0, ugenini dhidi ya Fountain Gate, Septemba 18, 2025.

Nyota huyo wa zamani wa Simba, alifunga bao hilo la Mbeya City kwa penalti ya dakika ya 56 na kumfanya kutoa gundu kwa sababu kabla ya hapo mara ya mwisho kufunga katika Ligi Kuu ilikuwa ni Mei 4, 2024, akichezea Singida Fountain Gate.

Katika pambano hilo la Mei 4, 2024, Singida iliifunga Dodoma Jiji mabao 2-0, ambayo yote yalifungwa na Kyombo (dakika ya 8 kwa penalti na dakika ya 76), ambapo msimu huo wa 2023-24, mshambuliaji huyo alimaliza akiwa amefunga mabao matano.

Bao hilo la Kyombo aliloifungia Mbeya City hadi sasa msimu huu, limemfanya kuhitimisha ukame wa siku 502 (karibia mwaka mmoja na nusu) kwa nyota huyo, ambaye amezichezea timu mbalimbali, zikiwemo za Singida Black Stars na Pamba Jiji alizozitumikia pia msimu wa 2024-2025.