Prime
Mashujaa ukiingia vibaya inakula kwako

KAULI mbiu yao ni ‘Hatoki Mtu’ ambayo inamaanisha timu yoyote itakayoenda kucheza uwanja wao wa nyumbani uliopo Ujiji, Kigoma basi kufungwa ni lazima.
Mashujaa FC imepanda na inashiriki Ligi Kuu Bara msimu baada ya kuishusha daraja Mbeya City iliyodumu kwenye ligi hiyo kwa zaidi ya miaka sita.
Makazi yao ni kwenye kambi ya jeshi maeneo ya Bulonge nje kidogo ya mji kwasababu ni timu inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Mashujaa imekusanya kijiji hasa pale inapocheza mechi zake na ilidhihirika wakati timu hiyo ilipokuwa ikishiriki Ligi ya Championship msimu uliopita, ilikuwa inajaza uwanja ikicheza nyumbani na hata ugenini ilipoenda kuishusha Mbeya City na ile mechi ya awali pale jijini Mwanza ilipocheza dhidi ya Pamba FC ambayo sasa inajulikana kama Pamba Jiji.
Mashujaa FC imepambana kupanda Ligi Kuu kwa miaka mitatu na ilianzishwa na wanajeshi wa kikosi cha 24 walioanza kama utani kwani waliunda timu yao ambayo lengo lilikuwa ni kufanya mazoezi tu kwa ajili ya kuimarisha afya zao tu.
Lakini baadaye waliona ni vyema ikawa timu rasmi inayojihusisha na mchezo wa soka na kuanza kuwahusisha wananchi ambao ni raia wa kawaida.
Mwanaspoti ambalo lipo Mjini Kigoma lilifanya mahojiano maalumu na mwenyekiti wa klabu hiyo, Meja Yahya Ismail Mgaya ambaye anaeleza mambo kadhaa juu ya timu yao ikiwemo mipango ya baadaye.
“Kama ilivyo kawaida huwezi kuanza moja kwa moja Ligi Kuu, tulianzia ligi za chini na tumepambana huko kwa miaka mitatu, timu yetu ina muunganiko wa wanajeshi na raia.
“Lilianza wazo kama timu ya kufanya mazoezi ya kuweka utimamu wa mwili kama wanajeshi ingawa baadaye tuliona ni vyema iwe timu rasmi, tulifuata taratibu zote na zikakubalika na wananchi, Chama cha Soka Kigoma (KFA), jeshi na serikali ya mkoa,” anasema Mgaya.
KAMATI ZA HAMASA
Mgaya anasema msimu uliopita walipoona kuna mwanga wa kupanda daraja ndipo kamati za hamasa zilipoundwa rasmi ili kuhamasisha wachezaji wanajituma zaidi kupata matokeo mazuri.
“Unajua Mkoa wa Kigoma haukuwa na timu ya Ligi Kuu kwa takribani miaka 20 nyuma, hivyo tulidhamiria kupanda daraja ili kuleta furaha zaidi kwa Wanakigoma. Lengo letu moja Kigoma nzima.
“Kila kamati ilijipanga kuona tunapanda Ligi Kuu na kweli ilikuwa hivyo, sasa kazi iliyobaki ni kuhakikisha tunakaa kwenye ligi moja kwa moja ikiwa na maana kwamba hatutaki kurudi tulikotoka.”
Miongoni mwa kamati za hamasa zilizoundwa ni kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa, mashabiki na wadau wengine ambao hawakutajwa wazi kutokana na nafasi zao.
MASHABIKI WAO
Mechi za mwishoni za msimu uliopita wa Championship timu hiyo ilipocheza mashabiki waliujaza uwanja, ikaonyesha kwamba watu wa Mkoa wa Kigoma wanapenda soka na wanapenda vya kwao.
Meja Mgaya anaeleza nini siri ya mashabiki hao; “Tuna mashabiki wengi sana, wananchi wa hapa wanapenda timu yao na wanapenda soka, tuna makundi zaidi ya 10 ya mashabiki hapa.
“Hii sio nguvu ya soda ndio maana hata mechi za Championship tulikuwa tunasafiri nao, hata sasa tutasafiri nao kwa utaratibu utakaokuwa unawekwa, hili mashabiki wetu popote walipo walibebe kuwa mashabiki wa Mashujaa popote timu itakapokwenda nao watakuwepo.
“Si mashabiki pekee hata kile chungu chetu kitasafiri na timu popote pale maana hiyo ndiyo nembo ama alama ya utambulisho wetu kuonyesha uasili.
“Hivyo mashabiki na chungu wanatasafiri pamoja. Na tutaendelea kuujaza uwanja popote hasa uwanja wa nyumbani uliobeba kauli mbiu yetu.”
Mashabiki wa Mashujaa wakiwa uwanjani kwao, Lake Tanganyika walisikika wakiimba nyimbo za timu mbalimbali kama vile ‘Leo ndio leo kivumbi na jasho’, ‘Kidedea’ zinazotumiwa na Simba na Yanga na ‘Mungu Ibariki Mashujaa’ ambao wamechukua maneno ya Wimbo wa Taifa.
“Mashabiki wetu wanaimba nyimbo za timu nyingine hiyo sio dhambi kikubwa hawaimbi matusi. Sisi ni timu changa hivyo wanachojaribu kukifanya ni kuimba nyimbo ambazo ni nyepesi kila mmoja kuziimba na si vinginevyo.
“Hatuna wimbo maalumu wa mashabiki wetu walioimba kwa ajili ya timu, ila tunaamini huko mbele wataimba nyimbo zao ingawa sasa huwa wanachanganya na nyimbo za asili yetu ya hapa.
“Kwasasa ni ruksa kwao kuimba wimbo wowote hata kama utakuwa wa timu nyingine ila ni kuzingatia maadili na nidhamu,” anasema Meja Mgaya
WANACHAMA
Bosi huyo anayataja matawi matatu ambayo yapo rasmi hadi sasa kuwa ni Ujiji, Mwandiga na Urusi ambayo yalizinduliwa hivi karibuni.
“Kama nilivyosema hapo awali timu hii ina uhusiano na wananchi wa kawaida, hivyo hapo baadaye tutakuwa na wanachama na wa kwanza atakuwa ni Mkuu wa Majeshi Tanzania, Generali Jacob Jonh Mkunda.
“Wanachama wengine ni wanajeshi na wananchi kwa ujumla. Mchakato huu umeanza ingawa unaweza kuchukua muda kidogo maana ni lazima tufuate taratibu zote,” anasema Meja Mgaya.
UJENZI WA UWANJA
Bosi huyu anasema kutokana na miundombinu ya viwanja Mjini Kigoma kutokuwa rafiki, jeshi limeanza ukarabati wa uwanja wake uliopo Bulonge.
“Kila kitu kinafanyika kwenye kambi yetu ya jeshi, hata wachezaji wetu wote wanaishi huko. Kuna nyumba ya ghorofa nne. Kwa kweli kwa hapa kwetu viwanja bado ni tatizo ukiachana na huo mkubwa wa Lake Tanganyika.
“Sasa huo huwezi ukaenda kufanya mazoezi kila siku, huwa tunaruhusiwa mara mbili kwa wiki siku nyingine tunafanya kwenye viwanja vya mchangani ambavyo sio rafiki sana kwa wachezaji wetu.
“Tumeanza ukarabati wa uwanja wetu ulioko kambini, tunaamini hadi kufika Januari utakuwa umekamilika na kuanza kutumika. Utakuwa uwanja wa kisasi ambao utakidhi vigezo na kabla ya kuanza kuutumia tutauzindua.”
WACHEZAJI MAISHA FRESHI
Kwenye suala la pesa Mashujaa hawako vibaya, huku kukiwa na taarifa kwamba wachezaji wanapoenda kucheza mechi hulipwa posho nzuri tu ukiachana na mishahara yao ya kila mwezi. Huku kwenye posho inadaiwa kila mmoja hupewa Sh 150,000. Kwa hapa vigogo wa Mashujaa hawajaanza vibaya.
“Yote yanawezekana kulipwa kiasi hicho ama la. Ila watambue tu kwamba Mashujaa haina njaa, wachezaji wanalipwa vizuri na kwa wakati, kwasasa naweza kusema katika timu tano za Ligi Kuu zinazolipa vizuri, basi Mashujaa ni miongoni mwa hizo.
“Hatutaki sababu, bali tunachotaka kuwaona wachezaji wanaishi vizuri ibaki wao kutekeleza kilichowaleta hapa, tunahitaji matokeo mazuri. Ila niweke wazi bajeti tuliyoitumia kuipandisha timu, bajeti ya msimu huu na ya uwanja vinabaki kuwa siri ya kambi,” anasema.
MAPATO
Meja Mgaya anasema mbali na pesa wanayoipata kutoka kwa wadhamini wa Ligi Kuu wanaendelea kutafuta udhamini mwingine.
“Hatuna vyanzo binafsi vya mapato kutokana na uchanga wetu ila kwasasa tunategemea pesa ya udhamini uliopo, mauzo ya jezi tutakazoanza kuuza hivi karibuni na viingilio ila pamoja na hilo jeshi halishindwi kitu mambo yatakuwa mazuri tu.”
MTIHANI WA BARESI
Mashabiki wa Kigoma hawapendi kusikia timu yao inapoteza mechi, yaani wanaona hayo sio maisha yao kwani wanaonekana wamezoea ushindi tu kuanzia huko Championship.
Sasa hii ni kazi nzito kwa kocha wao Mohamed Abdalla ‘Baresi’ kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na wakiteleza basi iwe sare na si vinginevyo.
Baresi anasema; “Ingawa mpira una matokeo matatu ambayo mengine ni ya kikatili lakini mashabiki wa Mashujaa wanapenda kusikia ushindi tu huo ni mtihani mkubwa sana.
“Shida ni kwamba walikotoka walifanya vizuri, tumeanza ligi vizuri kwa maana kwamba hatujapoteza mchezo, hivyo wanachoamini ni ushindi tu hadi mwisho.
“Ni vigumu kuwaahidi moja kwa moja kuwa tutashinda mechi zote, huu ni mpira ambao hata mpinzani wetu pia anataka kushinda ila ninachoweza kuahidi Mashujaa haitashuka daraja itakuwepo sana kwenye ligi.
“Nina kikosi kizuri ambacho naamini huko mbele kitakuwa vizuri zaidi ya sasa kutokana na usajili uliofanywa, ratiba kwetu imekaa vizuri tunacheza mechi tatu nyumbani, tunaenda ugenini mechi mbili halafu tunarudi hapa.”
MALENGO YAO
Meja Mgaya na Baresi wana mawazo yanayoendana msimu huu wa kwanza ni kuhakikisha wanajenga kikosi imara ili kubaki ligi msimu ujao.
“Unajua tulipanda Ligi Kuu mwishoni yaani tulikuwa wa mwisho, hivyo mambo mengi hayakufanyika maana kitu cha kwanza tulichokiangalia kwa wakati huo ni usajili. Ila kuna mambo mengi ya kufanya ili kufikia malengo yetu.
“Hii ligi ni ngumu, yanahitajika maandalizi yanayoendana na mipango thabiti ya klabu, lakini kwasasa malengo makuu ni kubaki kwenye ligi huku tukipambana kufikia malengo ya misimu mingine ya Top Four,” anasema Meja Mgaya .