Mashabiki wa Simba sasa wanapona
Muktasari:
- Mchezo huo uliochezwa kuanzia saa 2:15 usiku ulihudhuriwa na mashabiki wengi wakiwamo waliosafiri kutoka sehemu mbalimbali, ambapo waliuhanikiza Uwanja wa New Amaan unaobeba watu 15,000.
KATIKA mchezo wa Ligi Kuu ya NBC, Dabi ya Kariakoo kati ya Yanga na Simba uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ilishuhudiwa watani hao wa jadi wakitoka suluhu (0-0).
Mchezo huo uliochezwa kuanzia saa 2:15 usiku ulihudhuriwa na mashabiki wengi wakiwamo waliosafiri kutoka sehemu mbalimbali, ambapo waliuhanikiza Uwanja wa New Amaan unaobeba watu 15,000.
Maelfu ya mashabiki hao kikubwa wanachotaka kukipata ni ushindi au, la sivyo, droo. Vinginevyo, matokeo ya kufungwa hayakubaliki kwa sababu yanawaumiza kihisia.
Jaribu kupata picha kama Simba angefungwa ingekuwaje? Siku za karibuni mashabiki wa Simba walionyesha vitendo vya hasira pale timu ilipofanya vibaya, kiasi cha kuwashutumu baadhi ya viongozi, wakiwamo mwenyekiti wao.
Katika mchezo huo, wachezaji wa Simba walicheza katika kiwango kizuri huku wakimiliki mpira kwa kiasi kikubwa. Ingawa hawakushinda, matokeo haya yamewapa imani ya kufanya vizuri hapo baadaye.
Tafiti za sayansi ya saikolojia zinaonyesha kuwa shabiki anayepata matokeo yanayompa furaha huwa na afya njema kwani huepuka msongo wa mawazo, shinikizo na hofu.
Vilevile, tafiti zimeonyesha mashabiki wanapopata furaha ya ushindi au droo hupata hisia chanya zaidi; uwezo wa kiakili na umakini huwa mzuri zaidi, ikiwamo kufikiri, kutambua, kuamua na kutatua changamoto.
Ikumbukwe kuwa timu hizo zinapendwa sana na maelfu ya mashabiki. Kitendo cha kufungwa huwaacha wakiwa na maumivu makali ya kihisia yanayoambatana na huzuni na hasira.
Kabla ya mchezo huo, Simba ilikuwa imepoteza michezo sita ya ligi mfululizo dhidi ya Yanga. Matokeo haya yanaponesha maumivu waliyokuwa nayo kwa muda mrefu. Furaha ya droo itasaidia kuanza kupona maumivu waliyoyabeba moyoni.
Tangu mchezo ulipoanza wachezaji walionekana kuwa watulivu kimwili na kiakili, jambo lililowafanya mashabiki wa Simba kujenga imani ya ushindi kiasi cha kushangilia kwa nguvu.
Kisaikolojia, binadamu anapoanza kuonyesha furaha huwa ni hisia chanya, hali ambayo ina faida kiafya ikiwamo kupona majeraha ya kihisia yaliyotokana na kuumizwa. Kufungwa mechi zilizopita kuliwapa hisia hasi, ikiwamo hofu au woga. Tumaini walilopata baada ya mechi hii linakwenda kuwafanya mashabiki kupona kutoka katika maumivu ya kihisia waliyoyapata mara kwa mara walipokutana na Yanga katika mashindano mbalimbali.
Matokeo hayo yanawafanya mashabiki wa Simba kukaa mtaani wakiwa na furaha, kwani hata watani wao wameona jinsi kiwango chao kilivyo; hivyo si rahisi kutaniwa na kupata hasira.
Timu hizo moja inapopoteza, huwaachia maumivu makali ya kihisia, ikiwamo huzuni, hasira, kujitenga, hofu na msongo wa mawazo. Kwenye vijiwe, mitandaoni na ofisini uchokozi wa kuzidisha hasira huwa mwingi hasa unapokuwa umefungwa.
Mara nyingi hali kama hizi huweza kudumu kwa mashabiki hata kwa wiki nzima. Kubeba hisia za aina hii huwafanya hata wakiwa mtaani na ofisini kuonekana na huzuni.
Lakini, matokeo hayo na kiwango walichoonyesha vinawafanya kupona na kuwa huru na maumivu ya kihisia ya awali. Kumbukumbu mbaya za matokeo ya zamani sasa zitasahaulika.
Kadiri walivyokuwa wanacheza vizuri uwanjani ndivyo mashabiki walivyozidi kushangilia kwa nguvu. Jambo hilo liliwapa hamasa wachezaji na hatimaye kucheza kwa kasi na kushambulia zaidi.
Faida za kiafya za kimazingira
Mechi hii imechezwa kisiwani Zanzibar, ambako hali ya hewa huwa na upepo mwanana wa baharini. Hali hii humfanya mwanadamu kupata burudani na hatimaye utulivu wa hisia na akili.
Mchezo ulichezwa majira ya saa tatu usiku, muda ambao hakuna jua kali wala joto kali. Hii husaidia kupunguza shinikizo katika mwili kwani hakuna joto linaloweza kusababisha jasho jingi kupitia ngozi. Hali ya mazingira yenye joto kali huufanya mwili kuchoka mapema sana. Hii ilikuwa faida hata kwa wachezaji ambao wanapocheza hupoteza maji mengi kupitia jasho.
Muda uliochezwa uliwafanya hata wachezaji waliofunga kufaidika, kwani muda wa kufuturu chakula na kunywa maji hadi kuanza kwa mechi ulikuwa umetosha kwa chakula kusagwa na kurejesha maji mwilini.
Mchezaji aliyefunga huwa anakabiliwa na upungufu wa maji mwilini kwa sababu hushinda muda mrefu bila kula wala kunywa.
Muda huo na mazingira hayo yaliwabeba kujihami dhidi ya upungufu wa maji na madini. Vitu hivi ni muhimu kwa kazi za mwili; vinapopungua ni hatari ya kuchoka, kubanwa misuli na kupoteza umakini.
Kisaikolojia, mwanadamu anapopata mazingira mageni ya kuvutia hupata burudisho la kiakili. Hii humsaidia kuondoka na shinikizo la akili au msongo wa mawazo na hatimaye kupata usingizi mzuri baadaye.
Mazingira ya Zanzibar ni ya kitalii na yenye kuvutia, hivyo mshabiki aliyekwenda amefaidika kwa upande wa afya ya akili na kimwili. Hata wachezaji wamepata mapumziko mazuri yaliyowajenga kiakili.
Ukilinganisha na msongamano wa dimba la Benjamin Mkapa ule wa New Amaan ni nafuu zaidi kwani hauna msongamano mkubwa na haujazongwa na vizuizi vya majengo marefu.
Kupona zaidi kihisia wafanye hivi
Mashabiki wa Simba wanatakiwa kuendelea kuwa na hisia chanya na timu yao. Hii itawajengea hamasa ya kuishangilia kwa nguvu katika mechi zijazo na kuwapa wachezaji ari ya kushinda.
Wanapaswa kuepuka vitendo vya hasira au vinavyoleta mifarakano. Vitendo hivyo vinaweza kuleta hofu na wasiwasi na kuondoa hisia chanya walizopata katika mchezo wa Jumapili.
Kujitokeza kwa wingi na kushangilia katika michezo mingine kunawafanya wachezaji kuongeza juhudi na kutafuta ushindi. Mchezo uliopita tayari umewajenga kuamini wanaweza kufanya vizuri.
Wepuke kusoma kumbukumbu za zamani za timu kufanya vibaya; badala yake wajikite kufuatilia matokeo mazuri ya sasa. Kumbukumbu za kuumiza huufanya mwili kupata hisia za hasira na huzuni.