Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapya ukimya tuzo za TFF, wahusika watia neno

TUZO Pict


WAKATI Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2025-2026 ikitarajiwa kumalizika Juni 18, 2026, Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), msimu wa 2024/2025 bado hazijatolewa huku giza nene likitawala.


TFF ndiyo msimamizi mkuu wa tuzo hizo ambazo zinatakiwa kutolewa kila mwaka baada ya msimu wa ligi kumalizika kwa mujibu wa kanuni za shirikisho hilo.


Tuzo hizo zinatakiwa kutolewa kwenye makundi mbalimbali ambayo upande wa Ligi Kuu kuna Mchezaji Bora, Kipa Bora, Kiungo Bora, Beki Bora, Mchezaji Bora Chipukizi. Pia Tuzo za Kombe la Shirikisho la CRDB. Kuna tuzo za Ligi Kuu ya Wanawake, Tuzo za Ligi nyingine zikiwa Ligi ya Championship, First League, Ligi Kuu Wanawake, Wachezaji Wanaocheza nje ya nchi, Tuzo za Utawala, Tuzo za Waamuzi na nyinginezo.

Awali TFF ilitangaza kuwa tuzo hizo zilitakiwa kutolewa kabla msimu mpya wa ligi haujaanza, lakini baadaye ikatoa taarifa kuwa tuzo hizo zingetolewa Desemba 5, 2025, kisha ikatangaza kuwa zitatolewa pale shirikisho hilo litakapotangaza tena na hadi sasa ni zaidi ya miezi mitatu imepita.

Hata hivyo, chanzo chetu kimetueleza kuwa, tuzo hizo zimeshindwa kutolewa kutokana na msuguano uliopo kati ya wadhamini wawili wakubwa wanaofanya kazi na TFF kwenye ligi mbili tofauti, huku kila mmoja akitaka yeye ndiye asimamie utoaji wa tuzo hizo au kila mmoja atoe zake.

“Ninachofahamu mimi kuna msuguano, kuna vitu bado havijakaa sawa kwa wadhamini wawili ambao wanafanya kazi na (TFF), kila mmoja anaamini kuwa yeye ndiye anastahili kusimamia mchakato wa tuzo hizo kwa kuwa pia wanadhamini mashindano mawili ambayo ni makubwa hapa nchini na yote yanatoa tuzo, labda wakifikia muafaka tuzo zitatolewa lakini ni ishu ya kibiashara zaidi,” kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, kwenye kanuni za Ligi hakuna sehemu yoyote ambayo inaeleza ni nani anadhamini tuzo hizo pamoja na kwamba huko nyuma zimekuwa zikitolewa kwa mafanikio makubwa sana.

Ukiacha tuzo ambazo zilikuwa hazifahamiki ni nani atashinda, lakini tuzo ya Kipa Bora inafahamika kuwa ilitakiwa kwenda kwa Moussa Camara ambaye alikuwa kipa wa Simba na kumaliza msimu na Clean Sheet 19, pamoja na ile ya mfungaji bora ambayo ilikuwa inakwenda cha Jean Charles Ahoua ambaye pia alikuwa akiitumikia Simba ambapo alimaliza msimu na mabao 16, zaidi ya wachezaji wengine. Licha ya kuwepo na mambo mengine yaliyoingia baada ya ligi kumalizika ikiwamo michuano ya Chan 2024, Kufuzu Kombe la Dunia, Uchaguzi wa TFF na michuano ya Kombe la Kagame, lakini jambo hili lilitakiwa liwe katika ratiba za baada ya msimu kwani ni la siku moja, hivyo kamati inaweza kuendelea na maandalizi yake wakati mambo mengine yakiendelea.

TUZ 02

KANUNI ZINASEMAJE KUHUSU TUZO

Kanuni : 11 Vikombe na Tuzo

(1) Timu Bingwa wa Ligi Kuu itakabidhiwa kikombe cha ubingwa wa Ligi Kuu ambapo Bodi ya Ligi Kuu itapanga utaratibu wa sherehe.

(2) Endapo timu itachukua ubingwa kabla ya ligi kumalizika itapata heshima kutoka kwa timu pinzani kwa kila mchezo uliosalia wa Ligi Kuu itakaocheza kwa kujipanga kusalimiana kwa pongezi (guard of honour) kabla ya ukaguzi wa kuanza mchezo.

(3) Klabu Bingwa wa Ligi Kuu itahodhi kikombe cha ubingwa ilichokabidhiwa mpaka itakapotakiwa na Bodi ya Ligi Kuu kukirejesha. Endapo Klabu Bingwa itatakiwa kurejesha kikombe itapewa kikombe kingine kinachofanana badala yake.

(4) Medali, tuzo na kikombe kingine chochote kinachotolewa kama zawadi kwenye Ligi Kuu hakitarejeshwa, kitakuwa cha kudumu kwa aliyetunukiwa.

(5) Wachezaji, Kocha Mkuu na Maafisa wa Benchi la Ufundi wa Klabu Bingwa ya Ligi Kuu watapewa Medali za Ubingwa wa Ligi Kuu. Wahusika wengine wa kutunukiwa Tuzo/Medali watatunukiwa kwa Utaratibu utakaowekwa.

(6) Rais wa TFF ndiye atakayetoa Medali, Kombe na zawadi nyinginezo kwa Timu Bingwa na wahusika wengine. Endapo kutakuwa na Mgeni Rasmi aliyealikwa, Rais wa TFF atamshirikisha ipasavyo Mgeni Rasmi husika na wageni wengineo katika zoezi la Utoaji zawadi mbalimbali kwa wahusika.

(7) TFF kwa kushirikiana na TPLB itaweka miongozo, sifa na vigezo vya ushindi

(zitakazosomeka pamoja na kanuni hizi) kwa wahusika/makundi maalum yatakayoshinda kwa kupewa tuzo za Ligi Kuu. Washindi wa Tuzo mbalimbali za Ligi Kuu watapatikana kutokana na kupata alama zaidi ya washindani wao kwa mujibu wa sifa na vigezo vilivyowekwa.

(8) Hairuhusiwi kwa Timu, Kiongozi, Kocha, Mwamuzi, Mchezaji na Ofisa mwingine yeyote wa timu ya Ligi Kuu kushiriki au kuchukua kikombe au tuzo yoyote kuhusiana na Ligi Kuu au ushiriki wake kwenye Ligi Kuu kutoka

kwa mamlaka nyingine yoyote bila idhini ya TFF au kukaidi miongozo kuhusiana na Tuzo kwa Ligi Kuu. Ukiukwaji wa sharti hili utavutia adhabu ya faini au kifungo au vyote kwa pamoja kwa mhusika.

(9) Muhusika yoyote aliyeteuliwa katika Orodha ya wanaowania Tuzo za Ligi Kuu anawajibika kufuata maelekezo ya TFF kwa ajili ya Tuzo za Ligi Kuu ikiwemo ulazima wa kuhudhuria Sherehe za Tuzo. Mteule yoyote kuwania Tuzo za Ligi Kuu atakayeshindwa kufuata Utaratibu, maelekezo na Kuhudhuria Sherehe za Tuzo bila ridhaa ya TFF/TPLB atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo faini, kufungiwa michezo au kipindi fulani pamoja na kupoteza nafasi ya kuwa Mshindi na nafasi yake kuchukuliwa na mshindani anayemfuatia kutokana na vigezo.

(10) Bodi ya Ligi Kuu kwa kushirikiana na TFF itatayarisha na kusimamia utaratibu wa kupatikana kwa mchezaji Bora wa mchezo kwa kila mchezo wa Ligi Kuu.

(11) Sherehe za tuzo zitafanyika baada ya kumalizika kwa msimu husika katika tarehe itakayotangazwa na TFF.

(12) Kutakuwa na Tuzo ya Mfungaji Bora kulingana na mashindano mbalimbali ambayo Kamati ya Tuzo itakuwa imeamua kutoa tuzo kwa wahusika.

12.1 Mashindano yaliyokuwa na mfumo wa hatua ya kwanza na fainali zake kwa pamoja, magoli ya wafungaji bora yatahesabika kuanzia hatua ya awali hadi fainali.

(13) Mshindi wa tuzo ya Mfungaji Bora ni mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kuliko wengine katika shindano husika. Ikitokea wachezaji zaidi ya mmoja wamefungana idadi ya mabao, vigezo vifuatavyo vitatumika kwa kufuata mpangilio ili kumpata mshindi; 13.1 Magoli yaliyofungwa kwa njia ya kawaida yatakuwa na alama mbili (2) na magoli yaliyofungwa kwa njia ya penati yatakuwa na alama moja (1). Mchezaji mwenye alama nyingi atakuwa mshindi. 13.2 Endapo watalingana alama, mchezaji aliyecheza muda mchache zaidi atakuwa mshindi. 13.3 Endapo watafanana katika vigezo vyote viwili hapo juu, mchezaji aliyefunga mabao mengi ugenini atakuwa mshindi. 13.4 Katika mashindano ya mtoano, Mshindi atakuwa mchezaji ambaye timu yake imefika hatua ya juu zaidi kuliko mwingine na endapo hatua hii haitatoa mshindi kipengele cha i-iii vitatumika kwa mpangilio wake.

TUZ 01

KUVUNJA KANUNI

Kutokana na jinsi kanuni zilivyo, ina maana kuwa kama TFF halitasimamia kutolewa kwa tuzo hizo, basi litakuwa limeshiriki kwa njia moja ama nyingine kuvunja kanuni, jambo ambalo kwa klabu au mshirika yeyote wa soka nchini akifanya hivyo anatakiwa kupewa adhabu stahiki.

TUZ 03

KAULI YA TFF

Baada ya hali hii, Mwanaspoti lilimtafuta Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo ili kufahamu ni tarehe gani tuzo hizo zitatolewa kwa mujibu wa kanuni.

Ndimbo alisema hadi sasa hakuna taarifa mpya zaidi ya ile iliyotolewa awali kufuatia kuahirishwa kwa tuzo hizo zilizokuwa zitolewe Desemba 2025.

“TFF haijapanga tarehe rasmi ya kufanyika kwa tuzo hizo na pindi itakapopangwa umma utajulishwa, ni vyema watu wakaendelea kuwa watulivu.

“Shirikisho bado linasimama kwenye taarifa yake ya awali tuliyotoa wakati wa kuahirisha tuzo hizo, kwamba hadi sasa bado hakuna tarehe rasmi iliyopangwa, hivyo ni vyema kusubiri,” alisema Ndimbo kwa ufupi na kukata simu.

TUZ 04

AHOUA AZUNGUMZIA TUZO YAKE

Aliyekuwa kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua, ambaye alimaliza akiwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara, kwa sasa anaitumikia CR Belouizdad ya Algeria ambapo alisema yeye anasubiri muda ambao ataelezwa kuwa tuzo yake ipo, kwa kuwa anafahamu kuwa ni jambo la kikanuni na itatolewa muda wowote.

“Sina shaka sana, nasubiri tuzo yangu naamini kuna siku nitaipata, hii ya ufungaji bora ni ya kwangu mwenyewe kwa kuwa sina mshindani ukiachana na zile sehemu nyingine ambazo niliwekwa na wachezaji wengine, mfano mchezaji bora na kiungo bora,” alisema kiungo huyo raia wa Ivory Coast.

TUZ 05

TIMU ZINATAMANI HATA LEO

Ingawa baadhi waliogopa kutajwa majina yao kwenye habari hii, lakini kila klabu inayoshiriki Ligi Kuu Bara ilitoa kauli ya kuonesha kuwa zinatamani tuzo hizo zitolewa hata leo.

Mtendaji Mkuu wa Coastal Union, Omar Ayoub alisema kama viongozi ilibidi waelewe kwa sababu ya udhuru ya michuano ya CHAN 2025 ambayo ilikuwa mbele na TFF walipambana kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri. “Kulikuwa na michuano ya CHAN kwa kipindi kile jambo lolote ambalo TFF wangesema tulikuwa tunalielewa, lakini sasa huu ndio muda sahihi wa kulikamilisha hilo kwani tuzo sio tukio tu bali ni morali na hamasa kwa wachezaji.

“Ligi yetu ni kubwa, msimu kupita bila tuzo sio suala la kawaida na kila mmoja anafahamu, hivyo jambo jema ni kwamba tukio hilo lifanyike kabla ya msimu kumalizika ili tukienda msimu ujao tunakuwa na mambo mengine,” alisema kiongozi huyo.

Katibu wa Dodoma Jiji, Johnson Fortunatus alisema haoni kama ni jambo zuri TFF kuendelea kukaa kimya bila kutoa taarifa ya nini kimekwamisha jambo hilo. “Siyo jambo zuri kukaa kimya bila kutoa taarifa za kitu kilichokwamisha tuzo zisitolewe, kama vitu haviendi sawa siyo dhambi wala kosa kukosekana kwa tuzo hizo, jambo la msingi ni kuwajulisha wadau ili wasiendelee kujiuliza na kutengeneza maneno mengi mtaani.

TUZ 07

“Mbona miaka ya nyuma kuna kipindi zilikosekana na walipotoa taarifa hakukuwa na maswali, ninachokiona ni mamlaka zizungumze kitu.

“Tuzo hizo zinaleta thamani kwa wachezaji na morali ya kujituma kwa bidii, ila kama inashindikana hakuna dhambi wala lawama, jambo ninaloliona na la msingi kwa sasa ni mamlaka husika zitoea tamko juu ya hilo, zipo au hazipo na kwanini,” alisema Fortunatus.

Hata hivyo, kulionekana kuwa na hofu kwa baadhi ya viongozi wa timu kuzungumzia hili huku kiongozi mmoja akisema kuwa anafahamu tuzo hizo za msimu uliopita haziwezi kutoka.

“Unajua mara nyingi kwa sasa ukizungumza watu hawaamini sana kwenye maoni yako, lakini ni ukweli kwamba inaumiza kuona tuzo hazijatolewa hadi leo, ukiniuliza nitakuambia kuwa TFF wamefanya kazi kubwa sana tangu uongozi wa Wallace Karia ulipoingia madarakani lakini naona hili linaweza kushusha ile thamani yao, ninachoelewa mimi ni kwamba zile za msimu uliopita hazitatolewa kutokana na ratiba ilivyo.

“Lakini za msimu ujao zitatoka tena mapema tu baada ya ligi kumalizika na kutakuwa na hotuba ndefu sana ambayo itaeleza kwanini hazijatoka za msimu uliopita kitu ambacho kwangu naamini siyo sawa, jambo la msingi hapa wafanya watakavyoweza ili kumaliza jambo hili,” alisema kiongozi mmoja wa timu kubwa ambaye hakutaka jina lake litajwa.

TUZ 06

MTENDAMEMA, MWANGATA

Beki wa zamani wa Yanga, William Mtendamema alisema tatizo siyo tuzo lakini ni ukimya ambao upo na maisha yanaendelea tu kitu ambacho siyo sahihi.

“Ukimya ndiyo changamoto na hauleti tafsiri nzuri zaidi ya kuzua sintofahamu, vyombo husika vingetoa tamko ili watu wajue kama tuzo zipo ama hazitakuwepo, kuliko kunyamaza na watu kuendelea kujiuliza maswali yasiyo na majibu hili siyo jambo sahihi hata kidogo, watoke wasema kwa kuwa ni ishu ya kanuni huko nyuma zilitolewa vizuri na watu wakapongeza,” alisema.

Kwa upande wa Kocha wa Makipa wa Mbeya City, Patrick Mwangata ambaye timu yake ilikuwa inategemea tuzo kutoka Championship alisema: “Hatuwezi kuingilia hilo, ila waandaaji wenyewe ndiyo wanajua kwa nini wamechelewa, maana kipindi cha nyuma zilikuwa zinatoka kwa wakati, hivyo hatujajua katika maandalizi yao kimetokea kitu gani, tusubiri.”