Mapro wa muda wote Simba

SIMBA, Yanga na Azam FC zimekuwa zikisajili wachezaji kutoka nje ya nchi. Mara kadhaa klabu hizo zimekuwa zikileta wachezaji wasiokuwa na uwezo wa kuwaletea mafanikio.  Iko Imani kuwa baadhi ya viongozi huwasajili wachezaji hao kwa ajili ya kupiga pesa. Au wakati mwingine viongozi hao hushindwa kufanya ‘scouting’ ya kutosha kuwajua wachezaji hao. Lakini wapo wachezaji ambao wamesajiliwa na kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara na hata kuzing’arisha timu hizo kimataifa.
Hawa hapa ni wachezaji bora zaidi waliotoka nje na kuja kukitumikia kikosi cha Simba. Ni wachezaji ambao wametoka katika mataifa mbalimbali na katika misimu (miaka) tofauti.
Wapo waliokutana pamoja katika klabu hiyo na wengine hawakuwahi kukutana kabisa. Inaaminika kama wote wangekutana na kucheza pamoja katika kikosi cha timu hiyo? Moto ungewaka Afrika.


 1. Mackenzie Ramadhani
ALIKUWA ni kipa hodari kati ya waliotoka nje ya nchi na kusajiliwa na Simba. Mackenzie alikuwa mgumu kufungika. Raia huyo wa Burundi alisajiliwa 1990.  Alichangia ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuupoteza misimu minne tangu ilipobeba mara ya mwisho 1984. Mackenzie alikuwa mgumu kuingia wavuni pale linapofungwa bao ambalo si halali. Mfano mshambuliaji alifunga akiwa ameotea, aligoma kuingia wavuni hadi mchezaji mwingine autoe mpira. Bao la kwanza kufungwa ni dhidi ya Coastal Union kule Tanga. Lilikuwa shuti la mbali la starika Juma Mgunda (sasa kocha wa Coastal Union). Kipa huyo alipotea aliposajiliwa Mohammed Mwameja.


2. Asante Kwasi
Beki wa pembeni ambaye alikuwa fundi kupiga mipira iliyokufa. Raia huyu wa Ghana alikuwa na wakati mzuri chini ya Kocha Mfaransa Pierre Lechentre. Alimweka benchi Mohamed Husssein. Alicheza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry 2018. Baadaye Tshabalala alichukua namba yake ndio ikawa mwisho wake kuonekana.


3.Ramazan Wasso
Mmoja kati wachezaji wa kwanza wa kigeni kuitumikia Simba miaka ya 2000. Wasso alikuwa bonge la beki wa pembeni. Aliipeleka hatua ya makundi baada ya kuitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 2003. Baadaye aliomba kuachwa akacheze Ubelgiji, lakini alijiunga na Yanga na umaarufu ukaishia hapo. Hata aliporudi Simba hakung’ara.


4. Joash Onyango
Bado yupo kikosini. Ni beki mgumu na mwenye mafanikio Simba. Raia huyu wa Kenya ni beki wa kati kaifikisha timu hiyo robo fainali za CAF mara mbili.


5. Method Mwanjali
Aliletwa Simba na raia mwenzake wa Zimbabwe, kiungo Justice Majabvi 2016. Alikuja kuhitimisha Simba kunyanyaswa na mastraika wa Yanga, Donald Ngoma na Francis Chirwa. Umri wa Mwanjali ulishaenda na alihitimisha soka lake lakini alikuwa beki bora a wa kati kuwahi kutokea kati ya walioitumikia Simba kutoka nje ya nchi.


6. Patrick Mafisango
Mwaka 2010 Simba ilitaka kusamjili kiungo huyu wa Rwanda aliyezaliwa DR Congo. Lakini Azam FC ikaizidi ujanja kwa kuweka dau kubwa na kumchukua.  Mwaka 2011 mabosi wa Azam walichoshwa na vituko vyake wakawaita Simba na kuchukua Sh10 milioni na wachezaji wawili. Hakuna ubishi, pamoja na kwamba James Kotei alipata mafanikio  kucheza kimataifa na Simba, kama wangekuwa pa-moja asingepata namba. Mei 17, 2012 Mafisango alifariki dunia katika ajali ya gari.


7. Emmanuel Okwi
Amerudi Simba mara tatu. Okwi raia wa Uganda alikuwa na ufalme wake pale Msimbazi. Ni mchezaji aliyeimbwa na mashabiki wa Simba. Mara ya kwanza aliitumikia 2010.  Okwi aliifikisha Simba raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Ahly Shandi ya Sudan.
Mwaka 2013 aliuzwa Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia. Alirudi Simba tena 2014 akitokea kwa watani wao za jadi Yanga. Hata hivyo, hakukaa sana 2015 akauzwa Sonderjyske
Okwi alirudi tena Simba 2017 na kubeba ubingwa Ligi Kuu baada ya kuukosa miaka mitano.  Hapa ndio Okwi anakwenda na Simba hadi robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na kutolewa na TP Mazembe.


8. Clatous Chama
Mwamba wa Lusaka. Ni mfalme mwingine ndani ya Msimbazi. Chama akiwa katika ubora wake alifunga bao la kisigino dhidi ya ndugu zake Wazambia, Nkana Red Devils 2018 na kuiingiza Simba hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kama haitoshi tena mwaka huohuo akaipeleka timu hiyo robo fainali dhidi ya AS Vita ya DR Congo na hatimaye kutolewa na Mazembe.


9.Felix Sunzu
Ni mchezaji mahiri aliyekuja  kumalizia zama zake. Sunzu aliyetua Msimbazi 2011 aliijua sana goli. Raia wa Zambia juhudi zake uwanjani zilichangia kuipa Simba ubingwa 2011.


10. Meddie Kagere
Alitua Msimbazi 2018. Jamaa ni staika anayejua kujipanga. Ni mchezaji anayehitaji kulishwa mipira ili kuweza kufunga kuliko kutafuta mwenyewe.
Amekuwa mfungaji bora kwa misimu miwili mfululizo - 2018-19 mabao 23 na uliofuata alifunga mabao 22.

11. Luis Miquissone
Aliitumikia Simba msimu mmoja wa 2021- 22 akicheza mechi 50 na kufunga mabao 18. Bao lake dhidi ya miamba ya soka ya Afrika, Al Ahly katika Ligi ya Mabingwa lilitosha kumpa tiketi ya kusajiliwa na klabu hiyo ya Misri. Miquissone, raia wa Msumbiji  mchango wake uliifikisha Simba hatua ya robo fainali Afrika 2021.


WACHEZAJI WA AKIBA


Vincent Agban
Alikuwa kipa bora ingawa hakuwa na mafanikio makubwa Simba. Ni raia wa Ivory Coast.


James Kotei
Mghana huyu alikuwa na uwezo mkubwa sana pindi alipopewa jukumu la kucheza kiungo wa chini. Kotei ‘Invible man’ alikuwa akikaba kwa kufika na kugongana na wachezaji wa timu pinzani hadi mwisho.


Joseph Owino
Kama sio mafanikio ya Onyango, Owino ndiye angepaswa kuwemo katika kikosi cha kwanza. Ni beki wa kati ambaye alikuwa anajua kuitumikia nafasi yake.


Hillary Echesa
Kiungo bora kabisa, amewahi kuamua matokea ya mechi ya watani wa jadi kwa kufunga bao la ushindi dhidi ya watani wa jadi. Matokeo yakiwa 3-3, Echesa alifunga bao la nne katika dakika za nyongeza Aprili 18, 2010 na kuifanya Simba iibuke kidedea.


Mark Silengo
Winga hatari sana. Alishiriki kuipa ubingwa wa Tusker Simba jijini Nairobi mwaka 2005 chini ya Kocha Phiri.
Haruna Niyonzima
Mwite Fabrigas. Niyonzima raia wa Rwanda alitoa mchango kwa kuanzisha muvu ya bao la ushindi lililoipeleka Simba robo fainali dhidi AS Vita.


KOCHA JAMES SIANG’A
Hayati Siang’a ndiye kocha wa kikosi hiki. Raia wa Kenya ambaye 2003 aliingiza Simba hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika. Siang’a aliitoa Zamalek ya Misri kwa penalti.


MKURUGENZI WA UFUNDI - PATRICK PHIRI
Mzambia huyu ni mmoja wa makocha wa kigeni aliyeipa mafanikio Simba. Ndiye aliyeipa ubingwa bila ya kufungwa 2010. Ndiye aliyeipa Simba ubingwa nje ya Tanzania wa Kombe la Tusker kule Kenya 2005.