Mapema tu, umaarufu wao ulitesa muda mfupi

Mpole amshusha Minziro presha

LICHA ya kuwepo sababu mbalimbali zinazoweza kuwaondoa wanasoka wengi kwenye ustaa, mtaalamu wa saikolojia, Charles Nduku anaeleza namna baadhi ambavyo hawakuziandaa akili zao kupokea jambo katika maisha.

Nduki anasema misingi imara ya jambo lolote haiwezi kuondoa malengo yatakayokumbana na changamoto kwa sababu mhusika atakuwa anajua anachotafuta katika kazi zake.

“Tutolee mfano wanasoka. Wapo ambao umaarufu wao umedumu muda mrefu, wengine mwaka mmoja unaofuatia hawasikiki tena, ingawa zipo sababu nyingi ila wengi wao (wakati) unakuwa umewajia ghafla kwani hawakujenga misingi ya wanachotaka nini kwenye kazi hiyo,” anasema Nduku.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya wanasoka waliovuma mwaka mmoja kisha wakapotea kwenye midomo ya mashabiki wao na baadhi wanaendelea kucheza ilhali wengine wamegeukia shughuli nyingine.


GEORGE MPOLE

Jina lake lilikuwa linatajwa kila kona msimu uliopita kutokana na kumaliza akiwa kinara wa mabao 17 katika Ligi Kuu Bara na namna alivyokuwa anashindana kufunga na straika wa Yanga, Fiston Mayele, ambaye alimaliza nyuma yake akiwa na 16.

Ubora wake ulizivutia Simba, Azam FC na nyingine kutoka nje zilizohitaji huduma yake, huku akiwa bandika bandua timu ya taifa ‘Taifa Stars’. Ajabu imekuwa tofauti msimu huu ambapo muda mwingine anaonekana mbali na waajiri wake, Geita Gold.

Endapo Mpole hatatuliza akili na timu yake ambayo siku za karibuni imeonekana kana kwamba hakuna maelewano mazuri baina yao itakuwa ngumu kulinda umarufu aliokuwa nao msimu uliopita.


SALUM AIYEE

Katika msimu wa 2019/20 straika Salum Aiyee akiwa na Mwadui FC alimaliza na mabao 19 yaliyompa umarufu mkubwa na kuifanya KMC imsajili, lakini akaishia kusugua benchi, kisha akacheza timu mbalimbali kama DTB (sasa Singida Big Stars) kisha Fountain Gate.

Japokuwa bado anacheza, lakini jina lake halitajwi na wengine hawajui alipo zaidi ya kuishi na historia yake ya kile alichofanya akiwa Mwadui.


SAID BAHANUZI

Mwaka 2012 aliyekuwa straika wa Yanga, Said Bahanuzi alijizolea umarufu mkubwa baada ya kuibuka kinara wa mabao saba kwenye Kombe la Kagame, lakini ilikuwa kama tiketi ya mwanzo wake mbaya wa kuondoka kwenye ramani ya soka.

Baada ya hapo kiwango chake kilishuka na sasa yupo nje ya kazi hiyo akiendelea na shughuli nyingine kama anavyosema: “Kikubwa nachoweza kuwashauri wachezaji waliopo Simba, Yanga watumie fursa hiyo (ya kucheza), kufanya kazi vizuri kwa ajili ya kesho yao.”


MALIMI BUSUNGU

Wakati anatua Yanga mwaka 2015 akitokea Mgambo JKT ya Tanga, jina lake lilitakata kila sehemu, lakini baada ya msimu mmoja lilianza kufifia. Licha ya kuhamia Lipuli ya Iringa hakuwika kama mwanzo na sasa anaendelea na mambo mengine.

Busungu anasema: “Soka lina mambo mengi. Mchezaji anatakiwa awe na utayari wa kukabiliana nayo. Nimeamua kupumzisha akili yangu na kuendelea na shughuli nyingine nilizoziona zitanitengenezea kipato.”


GODFREY MWASHIUYA

Yanga ilimsajili akiwa kinda mwaka 2015 akitokea Kimondo ya Mbozi, na akiwa kwenye kiwango cha juu kilichofanya Simba itamani kuzungumza naye ingawa iliwahiwa na Yanga Alikuwa maarufu kwelikweli kipindi hicho, lakini msimu uliofuata akawa wa kawaida. Baada ya kuondoka Yanga, Mwashiuya alizunguka timu mbalimbali kama Mbeya City, Singida United kisha Singida Big Stars. Lakini anaonekana ni mchezaji wa kawaida sana tofauti na vile alivyokuwa akifananishwa na winga machachari wa enzi hizo Yanga, Edibily Lunyamila.


MOHAMMED IBRAHIM

Huyu ni kiungo aliyesajiliwa na Simba kipindi hicho kutoka Mtibwa Sugar na kiwango chake kilifanya awe anatazamwa kwa karibu na mashabiki wengi na pia kuzungumziwa kila kona, lakini ghafla alianza kupoteza umaarufu.

Nyota huyo maarufu kama Mo Ibrahim bado anacheza na kuna wakati alikuwa akikipiga JKT Tanzania, lakini kwa sasa hasikikii akizungumzwa kama mwanzo.

Mbali na nyota hao, mastaa wengine waliowahi kung’ara katika soka ni pamoja na Juma Mahadhi alipotoka Coastal Union kwenda Yanga, Mohamed Rashid kutoka Tanzania Prisons kwenda Simba, Marcel Kaheza alitoka Majimaji kwenda Simba na Emmanuel Mseja aliyetoka Mbao FC kwenda Simba.