Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MAONI: Miaka 34 bila kucheza Afcon, aibu iliyoje

Muktasari:

  • Awali fainali za michuano hii inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zilipangwa kufanyika Morocco lakini wenyeji hao wakaamua kujitoa na ndipo Guinea ya Ikweta ilipokabidhiwa jukumu la kuwa mwenyeji.

FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika au Afcon 2015 zinaanza rasmi leo huko Guinea ya Ikweta.

Awali fainali za michuano hii inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zilipangwa kufanyika Morocco lakini wenyeji hao wakaamua kujitoa na ndipo Guinea ya Ikweta ilipokabidhiwa jukumu la kuwa mwenyeji.

Kumekuwa na habari kubwa ambayo imetawala katika fainali za mwaka huu ambazo zitafikia ukomo mapema mwezi ujao kwamba hazitakuwa na mvuto.

Moja ya sababu inayotajwa kuchangia fainali kutokuwa na mvuto ni kitendo cha mwenyeji wa awali Morocco kujitoa kwa madai ya kuhofu maambukizi ya Ugonjwa wa Ebola.

Baada ya Morocco kujitoa ziliibuka dhana kwamba huenda fainali za mwaka 2015 zisifanyike kutokana na hofu ya maradhi hayo ambayo tayari yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 8,000 wengi wao wakiwa ni kutoka nchi za Afrika Magharibi.

Hata hivyo, kwa Watanzania hasa waliopewa dhamana ya soka dhana ya mashindano kukosa mvuto ni dhana ambayo inakosa nguvu hasa kutokana na ukweli kwamba Tanzania ina zaidi ya miaka zaidi 30 haijashiriki fainali za Afcon.

Mara ya kwanza na ya mwisho Tanzania kushiriki fainali hizi ilikuwa ni mwaka 1980 nchini Nigeria wakati huo mashindano haya yakijulikana kama fainali za Mataifa Huru ya Afrika.

Ni wakati ambao Afrika Kusini ilikuwa hairuhusiwi kushiriki kutokana na sera za ubaguzi wa rangi zilizokuwa zikitumika nchini humo.

Watanzania walio na mapenzi ya soka ni wazi kwamba wamekuwa na shauku ya kuona siku moja Tanzania ikiwa  miongoni mwa nchi shiriki kwenye  Afcon.

Juhudi zimekuwa zikifanyika lakini mara zote mambo yameendelea kuwa magumu hali ambayo imezidi kuifanya Tanzania kuwa ni timu mshiriki wa kusaka tiketi ambaye ameshindwa kutimiza ndoto ya kufuzu.

Tunadhani imefika wakati kwa Watanzania hasa waliopewa dhamana kuja na mikakati ambayo itaifanya Tanzania ifuzu fainali za Afcon 2017 ambazo awali zilipangwa kufanyika Libya lakini hali ya kisiasa imesababisha uamuzi huo ufutwe na mwenyeji mwingine anatarajiwa kutangazwa na CAF.

Tunaamini Tanzania inaweza kufuzu fainali hizo kama tu kila aliyepewa dhamana atawajibika na kuzitumia fainali za mwaka huu kuwa sababu ya kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa timu shiriki.

Ni vizuri kujiuliza ni kwa nini nchi kama Zambia na nyinginezo ambazo uchumi wao si mkubwa  kiasi cha kutisha zinaweza kufuzu na hata kuchukua kombe wakati kwa Tanzania suala la kufuzu tu limeendelea kuwa gumu kwa miaka zaidi ya 30.

Ile imani yetu kwamba katika soka la Tanzania mipango mizuri imekosekana ndiyo jibu sahihi la kwanini Tanzania inahaha kusaka tiketi ya Afcon kwa miaka zaidi ya 30. Mipango tunayoizungumzia hapa itakuwa na maana kama viongozi wenye dhamana watajifunza kutoka kwa nchi ambazo zimewahi kufuzu.

Tunaamini na tutaendelea kuamini kwamba jambo hili likifanyika Tanzania inaweza kufuzu Afcon na kuondokana na aibu hii ya miaka zaidi ya 30.

Na hata isipofuzu ushindani wa kusaka tiketi utaonekana kwani kwa kipindi kirefu Tanzania mbali na kushindwa kufuzu bado haijaweza kutoa ushindani wa kweli kwa timu inazoshindana nazo kuwania kufuzu Afcon.