Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo matatu yanamkwamisha Chama Yanga

CHAMA Pict

Muktasari:

  • Kuna muda ukifika mchezaji hatakuwa kama alivyokuwa hapo awali, ipo mifano hai hapa nchini, kina Benard Morrison aliisimamisha Dar nzima kwa tukio lake la kesi ya kuhama kutoka Simba na kwenda Yanga lakini sasa yuko zake Ken Gold akiuguza majeraha.

KWENYE maisha ya soka ni kawaida kuona wachezaji wengi waliokuwa na viwango bora lakini baada ya kuhamia timu nyingine ubora wao ukapungua.

Sababu za kushuka viwango vyao inaweza kuwa aina ya mifumo ya timu mpya, majeraha ya mara kwa mara, changamoto za kisaikolojia, kutofautiana na makocha au mazingira mapya yasiyoendana na mtindo wa kiuchezaji.

Usajili wa kiungo mshambuliaji, Clatous Chota Chama kwenda Yanga ulitazamwa kwa namna tofauti kila mmoja akisema lake lakini ilikuwa maumivu kwa mashabiki wa Simba ambao walikuwa bado na uhitaji nae.

Shamrashamra zilikuwa kubwa upande wa Jangwani walioamini kuwa na mchezaji mwenye mafanikio makubwa Afrika ingewasaidia hasa kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga ilitolewa hatua ya makundi.

Hata Chama alipoulizwa malengo yake makubwa Yanga alisema ni kuchukua ubingwa wa Afrika akiwa na Yanga lakini mambo hayakwenda sawa badala yake amekuwa akisugua benchi na sababu zilitajwa anacheza taratibu na Yanga inacheza soka la kushambulia.

Kila mmoja aliongea lake wengine wakisema kiwango chake kimeshuka ndiyo maana hachezi wakati ambao hakuwahi kupewa mechi kuthibitisha Mwamba wa Lusaka kiwango chake kimeshuka au la.

CHA 01

Swali ni je, hivi ni kweli Chama kashuka kiwango? inaweza kuwa kweli au sio kweli kila mmoja ana maoni na hoja yake lakini ubora wa wachezaji wa Yanga eneo hilo linaweza kufanya kiungo huyo kuonekana wa kawaida.

Kuna muda ukifika mchezaji hatakuwa kama alivyokuwa hapo awali, ipo mifano hai hapa nchini, kina Benard Morrison aliisimamisha Dar nzima kwa tukio lake la kesi ya kuhama kutoka Simba na kwenda Yanga lakini sasa yuko zake Ken Gold akiuguza majeraha.

Achana na stori ya Morrison 'Toto Tundu' duniani kuna mifano kibao, wapo wachezaji kama Philippe Coutinho aliyeng'ara akiwa Liverpool, lakini baada ya kuhamia Barcelona mwaka 2018 kwa dau kubwa, alishindwa kuonyesha kiwango kilekile na kutolewa kwa mkopo Bayern Munich na Aston Villa.

Eden Hazard akiwa Chelsea alitajwa kuwa mmoja wa wachezaji bora duniani, lakini baada ya kuhamia Real Madrid mwaka 2019, alikumbwa na majeraha na kushindwa kuonyesha ubora wake, Alexis Sánchez – alikuwa nyota wa Arsenal, lakini baada ya kuhamia Manchester United mwaka 2018, kiwango chake kilishuka sana na hakufikia matarajio ya wengi.

Mshambuliaji Fernando Torres alipokuwa Liverpool alikuwa miongoni mwa washambuliaji hatari zaidi, lakini alipotua Chelsea mwaka 2011, alipoteza makali yake na kushindwa kufunga mabao kwa wingi kama alivyofanya awali.

CHA 02

Mfano mwingine ni Kaka alitwaa tuzo ya Ballon d'Or mwaka 2007 akiwa AC Milan lakini baada ya kujiunga na Real Madrid alikumbana na changamoto ya majeraha na ushindani mkali ndani ya timu hiyo yaliyomfanya kiwango chake kushuka.

Hiyo ni baadhi tu ya mifano ya wachezaji wa kimataifa waliowahi kupitia changamoto ya kushuka kiwango baada ya kutoka timu moja na kwenda nyingine wakitarajiwa kufanya makubwa.

Mwanaspoti limekuchambulia mambo matatu yanayomfanya Chama asugue benchi Yanga akionekana mchezaji wa kawaida wakati alipotoka Simba alikuwa mchezaji tegemeo na supastaa.


NAFASI KIKOSINI

Tangu Chama atambulishwe jangwani msimu huu, Yanga imefundishwa na makocha watatu yaani Miguel Gamondi aliyetimuliwa kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo akidumu msimu mmoja na nusu, akafuata Sead Ramovic ambaye nae hakukaa sana akaondoka zake CR Belouzdad na huyu wa sasa Miloud Hamdi.

Makocha hao wote watatu ni kama hawampi nafasi ya kutosha kuonyesha uwezo wake 'Mwamba wa Lusaka' ambaye alikuwa na kijiji chake wakati anacheza Simba.

Wakati yupo Simba hakuna kocha aliyemuweka benchi na hilo ilitokana na kiwango alichoonyesha, kiufupi makocha waliingia kwenye mfumo wa nyota huyo.

Januari 18, 2023 aliyewahi kuwa kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira 'Robertinho' aliwashtua mashabiki wa Simba baada ya kumtoa Chama dakika 33 na kumuingiza Pape Sakho kwenye mchezo wa Ligi kuu dhidi ya Mbeya City iliyoshuka daraja, wakiamini ndiye mchezaji anayeweza kubadilisha mchezo muda wowote.

CHA 03

Tangu hapo Robertinho akaendelea kumchezesha Chama kutokana na kelele zile za mashabiki ambao waliamini Chama angeendelea kuwepo uwanjani angefanya balaa lakini kwa sasa huoni kelele hizo tena za Mzambia huyo acheze.

Juzi kati kiungo Aziz KI alifunga ndoa na Hamisa Mobetto, alipomaliza sherehe siku ya pili yake, KI akaanza na kama kawaida Chama akaanzia benchi, ni kiasi gani nyota huyo ana kazi kubwa kutoka kwenye ufalme wake Simba hadi kusugua benchi akionekana mchezaji wa kawaida.

Hadi sasa Chama amecheza dakika 659 kati ya 1891 za ligi kuu akifunga mabao matatu na asisti tatu kwenye mechi 16.

Kwenye mechi hizo 16 za ligi kuu alizocheza Mwamba wa Lusaka nne pekee ndizo alianza na zilizosalia amekuwa akitokea benchi.

Kwa Gamondi, kiungo huyo alicheza mechi nyingi, yaani 10 na mbili pekee ndiyo alianza kwenye kikosi huku nane akiishia benchi akicheza dakika 477.

Alipoondoka Gamondi ilionekana sasa ni muda wa Chama kupata namba mbele ya Ramovic, lakini nae aliendelea kumuweka benchi akimpa mechi mbili tu kati ya sita akicheza kwa dakika 96.

Mambo ni kama yalionekana kuwa afadhali baada ya kuondoka kwa 'German Mashine' kwani mechi ya kwanza kwa Miloud alianza nae akicheza kwa dakika 46 dhidi ya JKT Tanzania, KMC 24 na juzi alipocheza dakika 21 na kufunga mabao mawili na asisti moja.


Chini ya Hamdi  

(Dk 21) v Mashujaa

(Dk24) v KMC

(Dk 46) v JKT


Chini ya Ramovic  

(Dk 28) v Kagera Sugar

(Dk 68) v KenGold


Chini ya Gamondi 

(Dk 82)v JKT Tanzania

(Dk 67) v Singida BS

(Dk 83) v KMC

(Dk 28) v Pamba Jiji

(Dk 08) v Simba

(Dk 32) v Tabora United

(Dk 35) v Coastal Union

(Dk 46) v Azam fc

(Dk 36) v Namungo assist ya Pacome

(Dk 26) v Kagera

(Dk 29) v KenGold

                 

TATIZO AZIZ KI

Kila ilipokaribia tamati ya mkataba wa Chama na Simba, Wananchi walipambana kuhakikisha wanapata saini ya nyota huyo lakini mambo hayakwenda sawa akaendelea kusalia Msimbazi.

Unaweza kusema Chama alijiunga na Yanga wakati ambao timu hiyo iko kwenye fomu nzuri kuanzia kwenye benchi la ufundi, wakisajili wachezaji wenye ubora jambo lililochangia kwa kiasi fulani.

Eneo analocheza Chama kuna Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Aziz KI ambao wamekuwa na kiwango bora tangu msimu uliopita wakitengeneza utatu wa hatari, pia ilimuongeza Duke Abuya ambaye nae amecheza mechi kadhaa akianza karibu kila kocha aliyepita na Jonathan Ikangalombo ambaye bado hajacheza mchezo wowote.

Kiungo huyo anaweza kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji ambayo ndiyo asilia na winga zote mbili maeneo ambayo yana wachezaji walionyesha kiwango bora wakiingia kwenye mifumo ya makocha.

Lakini tabu inaonekana ipo kwa Aziz KI ambaye ndiye anacheza eneo moja na Mzambia huyo akipewa nafasi ya kucheza mara kwa mara iwe kaonyesha kiwango bora au akicheza vibaya bado alianza kwenye kikosi hicho.

KI anapewa nafasi kubwa kutokana na kile alichokifanya msimu uliopita, akiibuka kinara wa ufungaji akiweka kambani mabao 21, Mchezaji bora (MVP) na kiungo bora alikuwa akichuana na kiungo wa Azam FC, Feisal Salum 'Feitoto'.

Kwa alichokifanya Aziz kuipa ubingwa timu hiyo wa ligi kuu na Kombe la FA na kucheza robo fainali ya CAF ikitolewa na Mamelodi Sundown kwa mikwaju ya penati, ilikuwa ngumu kwa kocha yeyote kumpa nafasi kubwa Chama ilhali alikuwa na Aziz aliyekuwa na msimu bora.

Hata alipoondoka Gamondi, timu ilipokuwa chini ya Ramovic naye alifanya kile kile kutokana na kuikuta timu katikati ya msimu, hivyo ilikuwa ngumu kufanya mabadiliko ya kumpa nafasi ya kuanza Chama.

Mwanzoni mwa msimu Aziz hakuanza vizuri kuanzia kwenye utengenezaji wa nafasi na kufunga lakini bado makocha walimtumia kwa sababu ni mchezaji tegemeo eneo hilo.

CHA 04

MAZINGIRA MAPYA                

Hii inaweza kuwa sababu mojawapo ya kiungo huyo fundi wa kupiga chenga kutowika sana akiwa na Yanga kwani ndio msimu wake kwa kwanza katika kikosi hicho kilichosheheni viungo kibao.

Kwa dakika alizocheza akiwa na timu mpya ya kufunga mabao matatu na asisti tatu sio takwimu mbaya kwa kiungo mshambuliaji ambaye kazi yake kubwa ni kutengeneza nafasi kwa washambuliaji.

Simba alicheza kwa takribani misimu saba tangu alipojiunga na wana robo fainali ya CAF hao msimu 2018/19 akitokea Power Dynamos ya nchini kwao Zambia.

Msimu wake wa kwanza alifunga mabao matano kwenye mechi nne alizocheza ikiwa bado mabao mawili kuyafikia yale ya msimu wa kwanza akiwa na mnyama.

Kiufupi alikuwa anaifahamu vyema Simba kutokana na uzoefu mkubwa alioupata hasa kwenye michuano ya ndani na kimataifa ambayo ilikuwa ni kama yake akifanya makubwa akiwa na Simba ambayo ilicheza robo fainali tano za CAF.

Rekodi zinaonyesha Chama yupo kwenye orodha ya wafungaji bora 10 wa muda wote wa mashindano hayo akifikisha jumla ya mabao 23 na kukaa nafasi ya saba. Anayeongoza ni staa wa zamani wa TP Mazembeya DR Congo, Tresor Mputu aliyefunga 39.

Hata hivyo, yanamfanya kuwa mchezaji pekee wa Ligi Kuu anayeongoza kwa mabao Ligi ya Mabingwa Afrika, mabao hayo yanamfanya kumpiku nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta aliyeweka kambani mabao 21.

Amefika Yanga ambayo aliyokuwa anakutana nayo kwenye mashindano ya ligi, kombe la FA na ngao ya jamii kiufupi ni mgeni kabisa tofauti na alipotoka.

Hata hivyo, bado rekodi zinambeba kiungo huyo ambaye baadhi ya mashabiki wanatamani kumuona Chama aliyekuwa anakipiga Simba ingawa sio rahisi kwa mchezaji kutoka timu moja akahamia nyingine na kukifanya kile alichoonyesha klabu aliyopita.


NINI AFANYE?

Kwa kinachoendelea tangu ajiunge na Yanga hadi sasa ni wazi nyota huyo sio chaguo la kwanza la kocha Miloud Hamdi ambaye nae ameendelea kumuamini Aziz KI.

Inaelezwa Chama alisaini mkataba wa mwaka mmoja unaotamatika mwishoni mwa msimu huu lakini kwa hali inavyoonekana na kile kinachosemwa hana furaha ndani ya Yanga anaweza kuonyeshwa mlango wa kutokea.

Hakuna anayekataa Chama alikuwa bora akiwa Simba lakini aliondoka unyamani na kujiunga na Yanga, kabla ya hapo pia aliwahi kuuzwa RS Berkane ya Morocco msimu 2021/22 mambo yalipokuwa magumu akarejea tena Tanzania.

Maisha ya soka lazima yaendelee na kama ataendelea kuwa benchi itakuwa ngumu kwake ingawa anaweza kumuaminisha kocha anaitaka nafasi ya kucheza.