Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Malaika ajivunia mafanikio yake Ipswich Town

Muktasari:

  • Ingawa amezaliwa Marangu na kukulia England, lakini moyo na akili yake iko Tanzania. Anasema kila anapopata nafasi ya kucheza huonyesha kiwango kikubwa na kuwathibitishia kuwa mtoto mwenye asili ya Kiafrika anaweza kushindana katika kiwango cha juu.

KUNA msemo unaosema kipaji hakina mipaka, na hilo linaonekana kwa kiungo mwenye asili ya Tanzania, Malaika Meena anayekipiga Ipswish Town, ambaye anaendelea kuandika historia katika soka la wanawake nchini Uingereza.

Ingawa amezaliwa Marangu na kukulia England, lakini moyo na akili yake iko Tanzania. Anasema kila anapopata nafasi ya kucheza huonyesha kiwango kikubwa na kuwathibitishia kuwa mtoto mwenye asili ya Kiafrika anaweza kushindana katika kiwango cha juu.

Wiki hii Mwanaspoti ilifanya mahojiano na kiungo Malaika anayecheza Ipswich Town inayoshiriki Ligi Kuu England kwa Wanawake.


IPSWICH IMEMKOMAZA ZAIDI

Baada ya kucheza kwa mkopo katika kikosi cha Ipswich Town akitokea Bristol City, Malaika anasema amepata somo kubwa ambalo limembadilisha ndani na nje ya uwanja.

Anasema timu hiyo ilipitia changamoto nyingi, lakini mazingira hayo yalimfundisha kupambana, kutokata tamaa na kuelewa kwamba kila mechi ni vita ya kutafuta pointi tatu.

"Nimecheza ngazi ya shule, mashindano ya vijana nilikuwa kama sehemu ya kunikuza kisoka, lakini baada ya kufika hapa nimepata kitu tofauti kwa sababu tunacheza mechi za ushindani," anasema Malaika.

Kwa mujibu wake, kufanya kazi chini ya kocha David Wright kumemjengea kujiamini na kumsaidia kukua kama mchezaji mwenye uwezo wa kubeba majukumu makubwa katikati ya uwanja.


ASILI YA TANZANIA

Malaika anasema moja ya vitu vinavyomfanya ajisikie mwenye bahati ni kuwa na mizizi ya Kitanzania.

Anaeleza kuwa malezi aliyoyapata kutoka kwa familia yake yamemfundisha kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu watu na kutokukata tamaa hata pale mambo yanapokuwa magumu.

Anasema anatamani vijana wa Tanzania waamini kuwa mafanikio hayachagui unapotoka bali yanategemea namna unavyojituma na kuamini ndoto zako.

"Naamini hilo limenisaidia kunishepu kuwa mwanamke jasiri kama ninavyoonekana sasa, kwahiyo najivunia kuwa Mtanzania kwani hilo limenisaidia."


ARSENAL NA CHELSEA ZILIMJENGA

Katika safari yake ya soka kiungo huyo aliwahi kupita katika akademi za klabu mbili kubwa duniani, Arsenal na Chelsea za wanawake.

Anasema huko alijifunza kwamba mafanikio hayaji kwa bahati nidhamu ndiyo msingi wa kila kitu.

Anaongeza kuwa maisha ya mchezaji si mazoezi pekee bali yanahusisha lishe bora, usingizi wa kutosha, matumizi sahihi ya muda na kujitunza kila siku.

"Somo kubwa nililojifunza ni kwamba mchezaji anafanya vizuri zaidi pale anapofurahia safari yake na kuendelea kujifunza kila siku," anasema.


ANAJIONA KAMA POGBA NA VIERA

Malaika anajielezea kama kiungo wa box-to-box anayependa kushambulia na pia kusaidia ulinzi.

Anasema tangu akiwa mdogo alipenda kuwaangalia Paul Pogba na Patrick Viera, na kupitia uchezaji wao alijifunza namna ya kutawala eneo la kiungo kwa utulivu na kujiamini.

Anaamini bado ana nafasi kubwa ya kuendelea kukua na kuongeza mchango wa mabao pamoja na pasi za mwisho kwa timu yake.

Moja ya mechi anayoikumbuka zaidi msimu uliopita ni dhidi ya Sunderland, ambapo alicheza dakika zote 90 na kuibuka Mchezaji Bora wa Mechi.

"Nilicheza vizuri ingawa nilikosa mabao mengi na siko hiyo kulikuwa na watu wengi kutoka Tanzania akiwemo baba yangu mzazi kwahiyo hiyo ndio mechi ambayo ipo kwenye kumbukumbu zangu," anasema Malaika


MAREKANI NA UINGEREZA ZINA TOFAUTI

Mbali na kucheza England, Malaika pia amewahi kucheza soka la vyuo nchini Marekani akiwa na Wake Forest.

Anasema soka la Marekani liko vizuri kwenye kumiliki mpira na kujenga mashambulizi kwa utulivu, wakati soka la England lina kasi kubwa, nguvu nyingi na mabadiliko ya haraka kutoka kwenye eneo la ulinzi kwenda kushambulia.

"Napenda sana nilipoanza maisha yangu chuoni ndani ya miaka minne tulikuwa na timu nzuri, lakini kuna tofauti kubwa kati ya uzoefu unaoupata chuoni na ukiwa kwenye timu, " anasema Malaika

Anasema uzoefu huo umemfanya awe mchezaji anayeelewa mifumo tofauti ya mechi.


KUHUSU KURUDISHA KWA JAMII

Licha ya shughuli zake za soka, Malaika anaendelea kusaidia watoto wa Tanzania kupitia mpango wa kukusanya vifaa vya michezo kutoka England na kuvisambaza kwa watoto wenye uhitaji.

Anasema tangu akiwa mdogo aliguswa kuona watoto wengi wakipenda mpira, lakini walikosa vifaa vya kuchezea.

Kwa kushirikiana na baba yake na marafiki zake, wamefanikiwa kukusanya maelfu ya vifaa na kuvituma Tanzania.

"Wakati nakuja Tanzania nikiwa mdogo niliona watoto wengi wenye vipaji wakicheza mpira lakini wengi hawana vifaa kwahiyo nikaona kuna namna ya kuwasaidia ninapopata vifaa basi navituma nyumbani ili angalau watoto wafurahi."

Lengo lake ni kuanzisha taasisi rasmi ya misaada ili kuwafikia watoto wengi zaidi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Zanzibar, Mwanza na sehemu nyingine za nchi.

Anasema kinachomfurahisha zaidi ni kuona tabasamu na shukrani za watoto wanaopokea vifaa hivyo.


NDOTO ZAKE

Malaika anasema malengo yake makubwa ni kucheza kwa mafanikio katika Ligi Kuu ya Wanawake England na kuwa mmoja wa viungo bora wenye mchango mkubwa wa mabao na pasi za mabao.

Lakini zaidi ya mafanikio binafsi, anatamani kuona vijana wengi wa Tanzania wakiamini uwezo wao na kuthubutu kuanzisha safari za kutimiza ndoto zao.

UJUMBE WAKE KWA VIJANA

"Usisubiri hadi uwe maarufu au uwe na kila kitu. Anza na kile ulichonacho. Ukifanya kazi kwa moyo na malengo mazuri, watu wengi watakuunga mkono kuliko unavyofikiria."