Makocha wazawa na mitihani kwa wageni

Wednesday October 06 2021
makocha pic
By Daudi Elibahati

LIGI Kuu Bara imeanza kwa kishindo msimu wa 2021/22 ikiwa inashirikisha timu 16, tofauti na msimu uliopita uliokuwa na timu 18.

Katika timu hizo zinazoshiriki msimu huu ni tano tu zinazonolewa na makocha wazawa, huku zilizosalia zikiwa na wageni. Mwanaspoti linakuletea wazawa na jinsi watavyokutana na mtihani mzito kwenye mbio za ubingwa.

Hawa hapa ni makocha wazawa watakaokutana na mtihani mzito kwa wale kigeni kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.


MOROCCO - NAMUNGO

Kocha wa Numungo FC, Hemed Morocco ameleta ushindani kwa makocha wa kigeni kwani ameiwezesha timu hiyo kucheza michuano ya kimataifa msimu wa 2020/21, hivyo kutazamia kuendelea alipoishia kutokana na kuanza vyema ligi kwa ushindi wa mabao 2-0 na kutoa sare moja.

Advertisement

Msimu uliopita Morocco aliiwezesha Namungo kumaliza katika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 43 katika michezo 34. Kocha huyo aliwahi kufundisha Coastal Union, JKT Oljoro, Mbao FC, Zanzibar Heroes na Taifa Stars.


MALALE - POLISI TANZANIA

Mzawa mwingine aliyepo kwenye vita na makocha wa kigeni ni Malale Hamsini ambaye msimu uliopita timu ya Polisi Tanzania ikiwa mikononi mwake ilimaliza katika nafasi ya sita ikiwa na pointi 45. Aliwahi kuzifundisha timu za JKU, Ndanda FC na JKT Tanzania.


MKWASA - RUVU SHOOTING

Charles Mkwasa, kocha wa Ruvu Shooting anayefahamika kama ‘Master’ana leseni A ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) aliyoipata 2014. Yupo kwenye kinyang’anyiro cha makocha wazawa wanaopambana na wageni msimu huu akiwa na Ruvu Shooting ambayo msimu uliopita alimaliza nayo katika nafasi ya 11 na alama 41. Mkwasa pia kaifundisha Yanga na Taifa Stars.


MAYANGA - TANZANIA PRISONS

Kocha Salum Mayanga ni mzoefu na soka nchini. Mbali na Prisons aliwahi kuzifundisha timu za Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Taifa Stars. Kocha huyo ametua Tanzania Prisons akipokea mikoba ya Aldof Rishard anayeifundisha Mwadui FC inayoshiriki Ligi ya Championship. Prisons msimu uliopita ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya saba na alama 44, hivyo kocha huyo kuwa jicho lingine linalotazamwa kwa atakachofanya msimu huu..


MAKATA-DODOMA JIJI

Mbwana Makata wa Dodoma Jiji aliwahi kupita timu mbalimbali ikiwemo Alliance FC aliyoipandisha Ligi Kuu Bara ilikoshiriki msimu mmoja na kushuka daraja.Hivi sasa yupo Dodoma Jiji aliyoipandisha Ligi Kuu ikiwa tayari msimu huu imecheza mechi mbili za ligi ikipoteza moja dhidi ya Simba kwa bao 1-0, huku ile ya ufunguzi iliifunga Ruvu Shooting kwa bao 1-0. Msimu uliomalizika Dodoma Jiji ilimaliza katika nafasi ya nane na pointi 44.


SIMKOKO-KMC

John Simkoko ni kocha wa KMC anayesaidia na Habib Kondo. Timu hiyo imefanya usajili bora na makini msimu huu na kinachosubiriwa ni matokeo tu uwanjani.


WASIKIE WADAU

Kocha mkongwe na mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah ‘King’ Kibadeni anaamini wazawa wana uwezo wa kufanya vizuri zaidi na kuleta ushindani dhidi ya wageni.

“Siku zote huwa najivunia makocha wetu. Wana uwezo mkubwa wa kushindana nao (wageni), ila hawajaaminiwa na kupewa nafasi kama ilivyo kwa wageni,” anasema.

Kwa upande wake, Adolf Rishard, anasema: “Makocha wa kigeni wanabebwa na timu zenye bajeti kubwa, lakini hebu wape timu ndogo uone kama watakuwa na maajabu. (Pia) ni tamaduni ambazo zimejengeka kwenye klabu zetu kuwa ili upate mafanikio lazima uwe nao, jambo ambalo si kweli.”

Msemaji wa KMC, Christina Mwagala anasema: “Benchi letu lote likiongozwa na kocha mkuu, John Simkoko na msaidizi wake, Habib Kondo ni wazawa, hivyo inaonyesha wazi kuwa viongozi wana imani nao ndio maana ya kupewa nafasi hizo kuliko makocha wa kigeni.”

Advertisement