Makocha watungiwe kanuni za kusimamia maoni wanayotoa
Muktasari:
Imekuwa ni kawaida kwa wapenzi wa soka na wakati mwingine hata vyombo vya habari hapa kwetu kuwa na mitazamo na tafsiri tofauti kutokana na matukio yanayotokea katika soka letu hapa Bongo na yale yanayotokea Ulaya hata kama yanafanana kwa kila namna.
ASSALAAM aleiykhum wasomaji na wanamichezo wenzangu kwa jumla. Leo Jumamosi ikiwa ni siku ya ufunguzi za msimu wa Ligi Kuu ya Vodaco michezo kadhaa itachezwa katika viwanja mbalimbali na nyingine itachezwa kesho.
Imekuwa ni kawaida kwa wapenzi wa soka na wakati mwingine hata vyombo vya habari hapa kwetu kuwa na mitazamo na tafsiri tofauti kutokana na matukio yanayotokea katika soka letu hapa Bongo na yale yanayotokea Ulaya hata kama yanafanana kwa kila namna.
Mfano, kuna wakati mashabiki wa Manchester United waliopo Bongo wanakubali na kuelewa somo kirahisi kabisa pale Robin Van Persie anapopoteza nafasi ya wazi ya kufunga na wachambuzi au watangazaji kusema ni bahati mbaya.
Lakini tukio hilohilo linapotokea kwa Uhuru Suleman wa Simba au Oscar Joshua wa Yanga mashabiki haohao hawataki kukubali kuwa jibu lilitolewa kwa Van Persie linaweza kuwa sahihi kwa Uhuru au Joshua.
Kama Van Persie anaweza kukosea, basi hata kina Joshua nao wanaweza kukosea.
Nje ya uwanja pia kumekuwa na mengi ambayo wenzetu waliotutangulia wamekuwa wakiyafanya kwa faiada ya mchezo wa soka, nasi tunaweza kuyaiga kwani kuiga mambo mazuri si dhambi.
Mfano, sote tunafahamu mchango wa Uingereza katika baadhi ya sheria na kanuni zinazosimamia soka sehemu mbalimbali duniani na hata katika Shirikisho la Soka la kimataifa.
Waingereza wamekwenda mbali zaidi katika kulinda maisha ya wachezaji baada ya msimu huu kuweka kanuni inayompa daktari mamlaka ya kuamua kama mchezaji anaweza kuendelea na mchezo au la pale anapopata maumivu sehemu ya kichwani.
Kanuni hii inahanikizwa na tukio lilitokea katika fainali za Kombe la Dunia za Brazil ambapo katika pambano kati ya England na Uruguay .
Mchezaji wa Uruguay aliumia kichwani na kisha kung’ang’ania kuendelea na mchezo akiwa katika hali ya kutokujitambua (unconsciousness).
Inaweza kuwa ni vigumu kwetu ‘kukopi na ku-pesti’ kanuni hiyo kwa sasa kutokana na kutokuwa na mfumo ulio tayari wa kulisimamia hilo.
Mfano sote tunawaona makocha wa klabu za Ligi Kuu England walivyowekewa sheria inayowaongoza kutoa maoni baada ya mechi kumalizika.
Hali hiyo imeondoa shutuma kwa waamuzi kutoka kwa makocha kutoa kauli ambazo zinaweza kuhatarisha maisha yao.
Hapa nyumbani tumeshuhudia makocha wa timu za Ligi Kuu wakiwashutumu waamuzi kwenye vyombo vya habari baada ya mechi na kudai uchezeshaji wao ndio uliosabibisha timu zao kufungwa .
Makocha hao huwa wanashindwa kuzungumza kitaalamu sababu za timu zao kufanya vibaya.
Binafsi ningefurahi kama kanuni kama hii ingeanza kutumika kwa makocha ambao hawana kitu cha ufundi cha kuwaambia waandishi na kushusha lawama hata kama wachezaji wao ndio waliopoteza nafasi nyingi.
Nimalize kwa kuiomba Bodi ya Ligi ambayo najua ilitoa elimu ya haki na wajibu wa viongozi wa klabu za Ligi Kuu lakini pia wafikirie uwepo wa kanuni itakayowaongoza makocha kutoa maoni.