Prime
Makocha: Kuna timu hukodi timu za vijana mitaani - RIPOTI MAALUM 4

Muktasari:
- Kocha mzoefu wa kuibua vipaji kwa vijana wadogo anasema changamoto kubwa ya kutokuwa na maendeleo stahiki ni namna timu zinazoshiriki Ligi Kuu kujikita zaidi kuzipa kuvipa vipaumbele vikosi vinavyoshiriki ligi, huku akikiri kwamba zipo klabu zinazotumia timu za vijana kwa kukodi mitaani badala ya kuzisimamia.
KATIKA sehemu iliyopita ya mfululizo wa makala za leseni za klabu upande wa timu za vijana, wadau wamezungumza mambo mbalimbali ikiwamo changamoto zinazosumbua... Endelea na mahojiano haya
Kocha mzoefu wa kuibua vipaji kwa vijana wadogo anayefanya kazi kwenye kituo cha Magnet, Wane Mkisi anasema changamoto kubwa ya kutokuwa na maendeleo stahiki ni namna timu zinazoshiriki Ligi Kuu kujikita zaidi kuzipa kuvipa vipaumbele vikosi vinavyoshiriki ligi, huku akikiri kwamba zipo klabu zinazotumia timu za vijana kwa kukodi mitaani badala ya kuzisimamia.
“Tatizo linakuja moja, timu nyingi zimejielekeza kwenye timu kubwa zinazocheza Ligi Kuu. Wanafanya hivyo kwa kuwa matokeo yake ndio yanayoonekana haraka. Tatizo lingine linakuja klabu zinaona ni gharama kuendesha soka la vijana,” anasema.

“Timu nyingi zinazocheza Ligi Kuu hazina hata hivyo vikosi chini ya miaka 20 na 17. Ukizichunguza kwa umakini zipo timu zinachukua timu za mtaani. Watazichukua zitacheza mashindano (ligi ya vijana ya TFF) kwa jina la timu za Ligi Kuu, haya mambo yapo. Unaweza kukutana na timu ya vijana kwa umri huo, lakini ukakuta wachezaji wana umri mpaka miaka 25 na 27 tena ambao wameshacheza mpaka ligi.”
“Tuondoe siasa tuache kutaka mafanikio ya haraka bila kutoa jasho. Tutengeneze mpango mzuri wa usimamizi wa kuzalisha vijana tuwe na idara za ufundi ambazo zitatengeneza programu sahihi ya kwenda kuzalisha vijana ambao wanajua namna ya kuzalisha kupitia mpango wa soka la vijana.”
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola ambaye pia amewahi kusimamia jukumu la kuzalisha vijana ndani ya klabu hiyo anasema hakuna uhalisia wa kukuza na kuzalisha vijana kwa klabu za Ligi Kuu, huku akiitaka TFF kuhakikisha inaaanzisha mashindano zaidi ya vijana yatakayochezwa kwa muda mrefu badala ya yanayofanyika kwa wiki chache.

“Kinachoendelea kuhusu hii leseni ya klabu ni kama klabu zinataka kuonekana zinafuata tu, ila uhalisia mambo bado sana yako nyuma. Kitu cha kwanza kinachotuangusha ni kukosa mashindano maalumu kwa ajili ya hawa vijana. Unaona kama kuna timu ya vijana chini ya miaka 17, lakini zipo timu zinamiliki hizo timu, ila wala sio zao ni za mitaani tu,” anasema Matola.
“TFF inatakiwa kutengeneza mashindano ya muda mrefu kama ilivyo Ligi Kuu, hata haya ya chini ya miaka 20 yenyewe hayakidhi vigezo yanachezwa kwa wiki mbili. Wito wangu ni TFF ishirikiane na serikali kutafuta wadhamini watakaojikita kudhamini soka la vijana ili lipate nguvu kama ilivyo Ligi Kuu. Kwa mambo yanavyoendelea sasa ni vigumu kuona matunda tunayoyatarajia.
“Sasa hivi imekuja sheria kwamba kila timu inayocheza ligi ihakikishe inawapa nafasi vijana kutoka timu ya vijana, lakini fuatilieni ni timu gani imewatumia hao vijana. Hawatumiki kwa sababu hawapo tayari kushindana huku juu, kwa kuwa huku chini walipotoka hawajapikwa vizuri. Watawekwa pale (benchi) watakuwa watazamaji tu na sio kushindana.”
Kocha mwingine aliyebobea kwenye soka la vijana, Kassim Liyogope anasema changamoto kubwa ni klabu kutokuwa tayari kuwekeza kwa vijana, huku akipinga suala la ukosefu wa fedha kuwa kikwazo.

“Tatizo kubwa naloliona ni kutokuwa tayari kwa sababu ukizungumzia uchumi timu nyingi zinao,” anasema Liyogope.
“Kwa hiyo ukiniambia timu zimeshindwa kutekeleza mpango wa soka la vijana kwa kukosa fedha hilo sikubaliani nalo. Kwa kuwa kila klabu ina makao makuu halafu ina uwanja wa nyumbani palepale inapofanyia mazoezi timu yao kubwa panaweza kutumiwa na timu ndogo. Kitu muhimu ni kuwa na makocha sahihi wenye taaluma ya kutekeleza inavyohitajika.”
Said Tully aliyewahi kuhudumu kwenye kamati ya soka la vijana TFF, anasema wasimamizi wakuu wa kanuni wanatakiwa kukomaa na klabu kubwa za Simba na Yanga ambazo hazina sababu ya kushindwa kuwekeza soka la vijana, huku akiwataja baadhi ya viongozi kukosa sifa na mapenzi ya dhati ya kuendeleza soka badala yake wamejikita kusaka mafanikio binafsi.
“Kilichopo ni suala la kifedha ukiangalia namna hata hizo timu za juu zinavyoendeshwa kuna mambo unaona hayajakamilika. Nachoona watu wengi waliokuja kuongoza hizi klabu hawana mapenzi sana ya maendeleo ya mpira. Wanakuja kwa sababu soka ni ajira mtu anapata riziki maisha yanakwenda. Mkazo mkubwa imekuwa ni namna gani atapata fedha na kama sio fedha, basi atapata sifa,” anasema.

“Asilimia 80 kati ya 100 ya watu wanaopenda mpira wanapenda Simba na Yanga, inayobaki 20 ndio unaweza kuwapata wanaopenda soka. Sasa hapo ukizigusa hizi klabu kubwa utasikia kelele. Mimi nasema mfano unatakiwa kupatikana kupitia hizi klabu kubwa. Kama wangeanza na hizi, basi kwenda klabu za chini ingekuwa rahisi. Sasa kama zimeshindikana hizi klabu kubwa huwezi kuzibana hizi ndogo.”
Kuhusu hoja ya kukosa mashindano kwa timu za vijana Tully anaipinga akisema: “Sikubaliani nayo, tunapohitaji mashindano hatutakiwi kuangalia matokeo, tunatakiwa kuangalia kijana anajengwaje. Mashindano yapo mengi sana, mimi bado nitabaki na hizi klabu kubwa ambazo naamini zinaweza kuandaa mashindano mafupi na zikaalika timu za vijana mbalimbali kutoka Uganda ambao ukizialika tu zitakuja hata kwa basi kucheza na wenzao au hata zenyewe kwenda Uganda au hata Kenya.”
Kocha Bahati Mgunda wa Kituo cha Symbio kinachofundisha vijana kuanzia miaka 10, anasema timu za vijana zinahitaji muda na uvumilivu ndio maana ni vigumu kuona klabu zinakuwa na programu hizo, kwani wachezaji wengi wanakuwa shuleni.
Mgunda anasema mambo hayo yanatakiwa kuanzia shuleni japokuwa kuna Umiseta, lakini haichukui muda mrefu kama inavyotakiwa.

“Kupata wachezaji bora lazima tuanzie shuleni - kuanzia chini kabisa huko kuwe na mwendelezo wa mashindano ambayo watakuwa wakiyafanya kwa muda mrefu sio mwaka kwa mwaka. Tunakua sana kisoka, kuna hamasa na mambo mengi, lakini huku chini tunasahau ambao ndio wanakuwa wachezaji wa baadaye,” anasema.
WAZAZI HAWA HAPA
Mboka Francis, mzazi wa Johan Cruyff Mboka (7), anasema wakati mwanawe anaanza shule walimu walikiona kipaji na kumshauri amlee kimichezo ili afikie malengo na sasa mabadiliko anayaona baada ya mafunzo.
Naye Kathbet Koola, mzazi wa Sean Kathbet anasema tangu mtoto wake aanze kujifunza kuhusu mpira wa miguu kituoni kipaji chake kimeongezeka tofauti na awali.