Majeraha yasiyopona hatari kubwa kwa wachezaji wanaotumika sana
Muktasari:
- Mechi hizo zilizokuwa za kuvutia sana, kutokana na kuhusisha timu za taifa kutoka mabara yote, ambazo zimesheheni mastaa wakulipwa wanaocheza ligi kubwa, ikiwamo za bara Ulaya.
MWISHONI mwa wiki mbili zilizopita mpaka wiki hii, ligi mbalimbali duniani zilisimama ili kuwaruhusu wachezaji kushiriki mechi za kirafiki za kimataifa za FIFA.
Mechi hizo zilizokuwa za kuvutia sana, kutokana na kuhusisha timu za taifa kutoka mabara yote, ambazo zimesheheni mastaa wakulipwa wanaocheza ligi kubwa, ikiwamo za bara Ulaya.
Timu za Africa nazo hazikuwa nyuma, ikiwamo timu ya Taifa ya Tanzania, ambayo iliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Macau. Huku mechi ya kuvutia ilikuwa Argentina na Zambia Waafrika wakichapwa 5-0.
Katika mechi hizo jicho la kitabibu liliona namna wachezaji walio katika viwango vya juu wanaocheza ligi zenye ushindani mkubwa wakiendelea kupewa nafasi zaidi katika timu za taifa.
Lakini katika kufanya hivyo baadhi ya wachezaji ni kama vile kwao imekuwa mzigo na hii ni kwa sababu wanaingia katika kipengele cha wachezaji wanaotumika sana bila kupumzishwa, hivyo kuwa katika hatari ya kupata majeraha.
Ingawa mwili wa mchezaji una utimamu na ustahimilivu wa juu, na ukiwa umekomaa kuweza kucheza muda mrefu bila kujeruhiwa au kuchoka, bado wapo baadhi waliokumbana na majeraha.
Mfano ni staa wa Barcelona, Mbrazili Raphinha ambaye aliamua kujitoa kuichezea Brazil kwenye mechi hizo za kirafiki kutokana na majeraha ya misuli ya nyuma ya paja.
Mshambuliaji huyo atakuwa nje kwa wiki tano na anatarajiwa kurudi kucheza mchezo wa EL Clásico dhidi ya Real Madrid utakaochezwa mwezi Mei. Kuumia kwake ni pigo kwa klabu na timu yake ya taifa ambayo jana iliichapa Croatia mabao 3-1.
Siyo huyo tu aliyejitoa ili kujihami, bali pia mastaa kadhaa wa Arsenal walioamua kujitoa kutokana na majeraha ambayo hayajapona vizuri.
Leo tupate ufahamu kuhusu majeraha yasiyopona vizuri na madhara ya kuwa benchi muda mrefu kwa wachezaji wa soka wanaotumika sana.
HATARI KUCHEZA NA MAJERAHA YASIYOPONA
Haishangazi kwamba katika timu za taifa mwanasoka anapokuwa anategemewa ama kuamua kudanganya kupona na kucheza au akalazimishwa kucheza akiwa ametumia dawa za maumivu.
Mchezaji naye ni binadamu; hushawishika kudanganya ili apangwe kucheza kikosi cha kwanza, jambo ambalo humpatia bonasi ikiwamo ile anayopewa endapo atafunga au kuibuka ushindi.
Kwa kawaida kiashiria kikubwa cha mchezaji kuwa hajapona vyema ni kuhisi maumivu katika eneo la jeraha au kushindwa kutumia kiungo hicho vizuri.
Kucheza mchezo ukiwa na maumivu sio sahihi kiafya kwani kunaongeza ukubwa wa tatizo. Jeraha linapotoneshwa mara kwa mara ni chanzo cha kujijeruhi upya na hivyo kuchelewa kupona. Maumivu kwa mchezaji aliye majeruhi ni ishara kuwa jeraha bado halijapona vizuri, ingawa nje ya mwili anaweza kuonekana kuwa yuko timamu.
Maumivu yanaweza kuwa ya kawaida, ya kati au makali. Yanaweza kuwa ni majeraha ya mfupa, misuli, mishipa ya fahamu, na tishu nyingine za mwilini.
Panapotokea jeraha, mwili hujibu mapigo kwa kutuma “askari mwili” kwa ajili ya kukarabati eneo hilo. Mlipuko wa kinga ya mwili ndio chanzo cha mtu kuhisi maumivu, kufagika, kuvimba, kupata joto, na kubadilika rangi ya ngozi. Hali hii ndio kitabibu huitwa inflammation.
Wanamichezo ambao wako nje ya uwanja kwa kuwa majeruhi, hudhani kuwa maumivu yanapopungua au wamepona na wako fiti kuanza kucheza, pasipo kufahamu kuwa jeraha bado halijapona kikamilifu.
Mara nyingine, misuli ya mwili ya mwanamichezo inapotumika sana huambatana na vimichubuko vya ndani ambavyo uwepo wa maumivu ni kama ombi la mwili kuhitaji kupumzika ili kupona kabisa.
Unapobainika na wataalamu wa tiba za michezo kuwa una majeraha ya mfupa na nyuzi ngumu, yaani tendon na ligaments, fahamu kuwa itachukua muda kupona kabisa na kurudi mchezoni.
Mchezaji anahitajika kujifahamu na kujidhibiti binafsi kuhusu maumivu, ikiwamo kujua yanachokozwa na mambo gani; je yanaanza wakati wa mwanzo, katikati au mwishoni baada ya mchezo au mazoezi? Ni vyema pia kufahamu kama maumivu yanauma unapominywa au yanakuwepo yenyewe; je yanasambaa au yanaibukia sehemu nyingine? Kila tabia ya maumivu ya mwili hutoa picha ya chanzo chake na ukubwa wake.
Wataalamu wa tiba za afya za michezo huweza kugundua na kutibu maumivu, kuyatathimini madhara yake kiujumla, huku wakitambua mjongeo wa mwili ambao unaweza kuchochea tatizo hilo kuendana na jeraha lilipo.
Baadhi ya makocha, viongozi, na mashabiki ndio kawaida ya kushinikiza wachezaji walio na majeraha na maumivu, kuwapa dawa za maumivu na kuwalazimisha kushiriki mchezo huku wakijua wazi kuwa hawako imara.
Vilevile, hata kampuni kubwa zenye mikataba minono ni washinikizaji wa wachezaji wanaotangaza biashara zao kuchezeshwa, huku wakiwa hawajapona vizuri.
Ikumbukwe, kuchoma sindano na kunywa dawa za maumivu kunakwenda kuondoa maumivu na kukupa utulivu kwa muda tu, na si kukarabati jeraha na kuliponesha kabisa.
Hata pale anapopona mfupa, misuli au tishu zilizojeruhiwa kwa mara nyingine hatari ya kujeruhiwa mara kwa mara ni kubwa, kwani tishu hizo zinapungua uimara wa kuhimili michezo na mazoezi.
Ni vizuri kuepuka kumchezesha mchezaji au kucheza akiwa na maumivu au majeruhi, kwani ni sawa na kutanua ukubwa wa jeraha na hivyo kumgharimu kukaa nje muda mrefu akiuguza jeraha kubwa.
Ikumbukwe kuwa uwepo wa maumivu unachangia viungo vya mwili kutofanya kazi vizuri. Hivyo, anapocheza uwanjani huonekano hawako timamu kimwili na kisaikolojia.
MADHARA KUTOCHEZA MUDA MREFU
Ni kweli kama mchezaji hajachezeshwa siku nyingi anaweza kuwa mzigo uwanjani na hii ni kutokana na ukweli kuwa kukaa muda mrefu nje kunachangia wepesi wa mchezaji kupungua. Inahitajika kufuata hatua za uponaji za kitabibu kwa mchezaji aliye benchi, kutokana na kuwa majeruhi muda mrefu, ili kuepukana na madhara ya kukaa nje muda mrefu bila kucheza. Kwa kawaida, mwili wa binadamu unapokaa muda mrefu bila kufanya kazi, misuli huweza kupata tatizo la mkazo, hivyo kuwafanya wachezaji wakose wepesi na kucheza chini ya kiwango.
Vilevile wachezaji wasipocheza muda mrefu, na kwa kipindi walichokuwa wamejitenga, wanaweza kupata tatizo la uzito mkubwa kutokana na ulaji holela wa vyakula. Inahitajika umakini mkubwa kwa jopo la wataalam wa tiba kumtathimini kwa kina mchezaji aliyekaa muda mrefu benchi kutokana na kuugua majeraha ya muda mrefu. Mapendekezo yao ndio yanatumika na benchi la ufundi kuamua kumtumia mchezaji aliyekaa sana benchi.