Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majembe Ligi Kuu Bara ndani ya AFCON 2025

LIGI AFCON Pict

Muktasari:

  • Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi shiriki katika mashindano hayo, bendera ya Ligi Kuu Bara itapeperushwa si tu na nyota wa Taifa Stars, bali hata wa mataifa mengine wanaocheza ligi yetu wakiziwakilisha nchi zao.

LIGI Kuu Bara kwa sasa imesimama kupisha Fainali za Mataifa Afrika (AFCON 2025) zitakazoanza Jumapili wiki hii nchini Morocco.

Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi shiriki katika mashindano hayo, bendera ya Ligi Kuu Bara itapeperushwa si tu na nyota wa Taifa Stars, bali hata wa mataifa mengine wanaocheza ligi yetu wakiziwakilisha nchi zao.

Mbali na nyota wanaocheza sasa Ligi Kuu Bara tutakaowashuhudia katika AFCON 2025, pia wapo waliowahi kupita nao watakuwa Morocco.

Stephane Aziz Ki aliyeitumikia Yanga kuanzia Julai 2022 hadi Juni 2025, hivi sasa yupo Wydad Athletic na atakuwa na kikosi cha Burkina Faso kilichopangwa kundi E na mataifa ya Algeria, Equatorial Guinea na Sudan.

Kennedy Musonda ambaye naye alikuwa Yanga kuanzia Januari 2023 hadi Julai 2025 alipohamia Hapoel Ramat Gan Givatayim ya Israel, naye ameitwa kuitumikia Zambia iliyopo kundi A na wenyeji Morocco, Mali na Comoros.

Musonda atakutana na Djigui Diarra ambaye walikuwa wote Yanga. Diarra bado yupo Yanga na anaenda AFCON akiwa na timu ya taifa ya Mali.

Nyota mwingine ni beki wa Cameroon, Che Fondoh Malone anayecheza USM Alger ya Algeria aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Simba.

Che Malone alikuwa Simba kwa misimu miwili kuanzia Julai 2023 hadi Julai 2025 alipojiunga nayo akitokea Coton Sport ya kwao Cameroon.

Katika AFCON 2025, Cameroon imepangwa kundi F na bingwa mtetezi Ivory Coast. Timu zingine ni Gabon na Msumbiji.

LIG 02

MALI

Djigui Diarra wa Yanga, ndiye kipa tegemeo wa Mali akiwa amelitumikia taifa hilo katika mechi mbalimbali zikiwemo za kufuzu AFCON 2025 na za kufuzu Kombe la Dunia 2026 na huku hawajafanikiwa.

Diarra ataipambania Mali yenye hesabu za kubeba AFCON kwa mara ya kwanza huku ikiwa imewahi kucheza fainali moja pekee mwaka 1972.

Ikiwa kundi A, Mali itafungua dimba dhidi ya Zambia, kisha wenyeji Morocco, itamaliza makundi dhidi ya Comoros.

LIG 01

NIGERIA

Taifa lenye mataji matatu ya AFCON iliyobeba mwaka 1980, 1994 na 2013, katika kikosi chake cha nyota 28, kuna mwamba mmoja anayetokea Ligi Kuu Bara, Amas Obasogie anayecheza nafasi ya golikipa pale Singida Black Stars.

Obasogie amekuwa akiitwa mara kwa mara katika kikosi cha Nigeria na hivi karibuni alikuwepo wakati wa mechi za kufuzu Kombe la Dunia, taifa hilo likishindwa kutoboa.

Nigeria ipo kundi C ambalo lina timu zingine za Tunisia, Uganda na Tanzania.

Hapa Obasogie anakwenda kukutana na nyota wengi wa Ligi Kuu Bara, ukiachana na wale wanaounda kikosi cha Taifa Stars, pia kuna Khalid Aucho anayecheza naye Singida Black Stars na Steven Mukwala wa Simba, hawa wanaiwakilisha Uganda.

LIG 03

UGANDA

Kucheza fainali mara moja mwaka 1978, ndiyo mafanikio makubwa ya Uganda katika AFCON. Hii ikiwa ni mara ya nane inakwenda kushiriki mashindano hayo, Ligi Kuu Bara itawakilishwa na nyota wawili wa kikosi hicho, kiungo Khalid Aucho anayecheza Singida Black Stars na mshambuliaji Steven Mukwala wa Simba.

Kumbuka Uganda imepangwa kundi C na Tanzania, Nigeria na Tunisia.

LIG 04

ZIMBABWE

Mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube anakwenda kuiwakilisha Ligi Kuu BAra akiwa na kikosi cha Zimbabwe kilichopangwa kundi B na Misri, Afrika Kusini na Angola.

Zimbabwe hii ni mara ya sita inakwenda kushiriki AFCON, inasaka nafasi ya kuvuka kwenda 16 bora kwa mara ya kwanza baada ya nyakati zote kuishia makundi katika miaka ya 2004, 2006, 2017, 2019 na 2021.

LIG 05

TANZANIA

Kuna nyota 19 wanaocheza Ligi Kuu Bara wameitwa kuitumikia Taifa Stars. Nyota hao wanaoungana na wengine tisa kutoka ligi zingine kuunda kikosi cha wachezaji 28 wenye jukumu la kuipa heshima bendera ya Tanzania.

Mbali na nyota hao 19 kutoka klabu mbalimbali za Ligi Kuu Bara, pia kocha mkuu, Miguel Gamondi naye anaingia katika orodha ya watu wanaokwenda AFCON kutoka ligi hiyo. Gamondi ni kocha mkuu wa Singida Black Stars akiwa pia kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars.

Wachezaji wa Taifa Stars wanaocheza Ligi Kuu Bara wanaokwenda AFCON 2025 ni Yakoub Suleiman, Shomari Kapombe, Wilson Nangu, Morice Abraham, Kibu Denis na Seleman Mwalimu (wote Simba). Bakari Mwamnyeto, Mohamed Hussein, Dickson Job na Ibrahim Abdullah (wote Yanga). Hussein Masalanga, Nickson Kibabage na Habibu Iddi (wote Singida Black Stars). Zuberi Foba, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Feisal Salum na Iddi Selemani (wote Azam). Pia kuna Kelvin Nashon wa Pamba Jiji.