Morocco yaongoza mbio za ubingwa AFCON 2025
Muktasari:
- Ikumbukwe kuwa, Ivory Coast ndiyo bingwa mtetezi wa AFCON, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Nigeria kwenye fainali ya mashindano ya mwisho yaliyofanyika mwaka 2024 nchini Ivory Coast.
Kompyuta mahiri ya takwimu ya Opta Supercomputer, imetoa utabiri wa mataifa yenye nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, mashindano yatakayoanza wikiendi hii Desemba 21, 2025 nchini Morocco na kumalizika Januari 18, 2026.
Kwa mujibu wa Opta, Morocco, ambayo ni mwenyeji wa mashindano hayo, imepewa nafasi kubwa zaidi ya kutwaa taji la AFCON 2025, wakiwa na asilimia 19.1.
Nafasi ya pili inashikiliwa na Misri iliyopewa asilimia 12.4 ya kushinda kombe hilo. Inafutiwa kwa ukaribu na Senegal yenye asilimia 12.3 ya nafasi ya kutwaa ubingwa.
Katika nafasi ya nne ni Algeria, yenye asilimia 12, huku Nigeria ikikamilisha tano bora kwa kupata asilimia 7.3 ya uwezekano wa kushinda taji la mashindano hayo mwaka huu.
Mataifa mengine yaliyopo kwenye orodha ya Opta baada ya Nigeria ni Tunisia, Ivory Coast (mabingwa watetezi), Mali, Cameroon na Afrika Kusini.
Ikumbukwe kuwa, Ivory Coast ndiyo bingwa mtetezi wa AFCON, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Nigeria kwenye fainali ya mashindano ya mwisho yaliyofanyika mwaka 2024 nchini Ivory Coast.