Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maisha yanaendelea bila ya Fei Toto dabi ya Soweto

JICHO Pict


SAHAU kuhusu Dabi ya jana pale Unguja. Juzi nilikwenda kutazama Dabi ya Soweto. Moja kati ya dabi maarufu Afrika. Kaizer Chiefs dhidi ya Orlando Pirates. Majirani ambao wanaishi Soweto kama ambavyo kuna majirani wanaishi Kariakoo na jana walikuwa wanacheza katika ardhi ya Mzee Karume.


Ndugu yetu Cedric Kaze alichezea mabao 3-0. Ilikuwa haki kwa sababu Kaizer wapo ovyo. Pale kileleni wapo Orlando Pirates kwa sasa wakiwa na pointi zao 41, huku Mamelodi wakishika nafasi ya pili wakiwa na pointi 38.


Hata hivyo, walikuwa na mechi pungufu na jana walikuwa wanatazamiwa kucheza pambano leo jingine ambalo lingewafanya wafike kileleni kwa mara nyingine tena. Mamelodi wameutawala mpira wa Afrika Kusini na wametwaa mataji ya ligi mfululizo hadi wamechoka.

Juzi nikakumbuka afadhali na sisi siku hizi tumempumzisha Fei Toto. Alikuwa hapumui mida kama hii msimu uliopita. Wakubwa walikuwa wamemkalia kooni. Waandishi walikuwa wamemkalia kooni.

Wachambuzi walikuwa wamemkalia kooni. Kila mtu alikuwa amemkalia kooni kwa maana ya kutaka kumwona Fei akirudi zake Kariakoo kucheza Simba au Yanga.

Wakati huo vichwa vya habari vilikuwa hivi hapa. ‘Fei na Simba kila kitu safi’. ‘Yanga wamalizana na mama yake Fei Toto’. Mwingine angeandika ‘Ni suala la muda tu Fei kucheza na Pacome’. Mwingine angesema ‘Mo Dewji avunja benki, Fei njia nyeupe Msimbazi’.

Kuna viongozi wa hizi klabu ambao bila ya heshima walikuwa wakimuongelea Fei hadharani wakati kwa mujibu wa sheria za FIFA hairuhusiwi kufanya hivyo kwa watu wanaohusika moja kwa moja na klabu.

Wazungu wana lugha yao huwa wanasema ‘tapping’. Kwamba umemlaghai mchezaji mwenye mkataba halali na klabu yake. Sisi huku huwa tunajifanyia mambo kwa kiswahili tu.

Mwishowe kabisa familia ya Bakhresa ikaona ujinga ikaingilia kati. Familia akasaini mkataba mpya wa kuichezea Azam hadi baada ya miaka mitatu ijayo. Mdomo wetu wa kushindwa kuamini Fei anaweza kucheza timu nyingine nje ya Simba na Yanga ukaishia hapo.

 Na kwa namna tunavyoijua familia ya Bakhresa na utajiri wake ni bora mashabiki, watangazaji na wachambuzi wangekaa kimya tu. Kwa kufanya walichokuwa wanafanya wakawa wamewapandisha hasira kina Abuubakar Bakhresa wakampa Fei ofa nono.

Nilimkumbuka Fei juzi huku nikikumbuka namna ambavyo Wasauzi wamekubali mchezaji kama Fei kucheza Mamelodi. Ni suala la pesa tu kuongea. Mamelodi amekuja kusimama katikati ya utawala wa Kaizer Chiefs na Orlando Pirates kwa kutumia noti za tajiri Patrice Motsepe ambaye pia ni Rais wa CAF. Hakuna wanachoweza kufanya kwa sasa labda kama Motsepe ataondoa pesa zake Mamelodi.

Kuna mambo mawili hapa. Kwanza ni kwa nini hatuamini Azam FC inaweza kuwa Mamelodi yetu? Kwa nini hatuamini Fei anaweza kucheza kwa kutulia tu Azam akaipa mafanikio? Kwa nini hatuamini kama Fei hawezi kucheza Azam wakati huo huo tunaamini kwamba Pacome Zouzoua anaweza kucheza Yanga au Simba. Kwa nini hatuamini hata Pacome mwenyewe anaweza kwenda kucheza Azam.

Wasauzi wamebadilika katika hisia hizi. Lakini kitu cha pili ni kwamba Azam wenyewe wamechangia kwa kiasi kikubwa watu kuamini katika hili. Kila siku watu wamekuwa wakijiuliza Azam inakwama wapi kusimama katikati ya Yanga na Simba?

Inawezekana mazingira yetu ni magumu kuliko yale ya Afrika Kusini. Kwamba Simba na Yanga ni wakubwa zaidi nchini kuliko hata ilivyokuwa kwa Kaizer Chiefs na Orlando Pirates katika nchi yao.

Kama hilo ni sawa, vipi kuhusu mechi za kimataifa? Pyramids ya Misri walionekana kama vile wanafanyiwa figisu katika soka lao, lakini wakadhihirisha kwamba ni kweli wanafanyiwa figisu nyumbani baada ya kutwaa ubingwa wa Afrika.

Rafiki zangu Azam katika michuano ya kimataifa huwa wanasuasua kama wanavyosua hapa nyumbani.

Kitu cha kushangaza ni Azam wanapata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wa Simba na Yanga pindi wanapocheza mechi hizo.

Ushahidi ni pale nilipokuwa Mwanza nikitazama pambano la Azam na Wydad Casablanca lililokuwa linachezwa Morocco. Mashabiki katika baa walikuwa wanaishangilia Azam. Wote hawa walikuwa mashabiki wa Simba na Yanga.

Faida nyingine ambayo Azam wanaweza kuwa nayo ni kama wakiwa wanapambana na timu moja kati ya hizi katika msimamo wa ligi.

Kwamba unapambana na Yanga halafu Simba unamuacha mbali. Lazima Simba watakusapoti uchukue ubingwa mbele ya Yanga. Ni hivyo hivyo kama unapambana na Simba, huku Yanga akiwa ameachwa mbali.

Hata hivyo, ni nadra sana kwa nafasi hii kutokea kwa Azam. Kabla ligi haijafika nusu ya msimu tayari Yanga na Simba wanapambana pale juu.

Kwa mfano sasa hivi Kaizer Chiefs ameachwa pointi 11 na mtani wake Orlando. Wakati huo huo jana Mamelodi alitarajiwa kushinda na kuongoza ligi kwa tofauti ya mabao dhidi ya Orlando Pirates.

Kama mazingira haya yangekuwa Tanzania Azam angepata sapoti kutoka kwa mkubwa mmoja lakini kwa hali hii ya kila siku Yanga kufukuzana na Simba mapema tu huwa inafanya wakose sapoti kutoka kwa mfani mmoja.

Ni hilo ndilo ambalo linawafanya watu waamini kwamba Fei anastahili kucheza timu moja kubwa kati ya Yanga au Simba. Ni hilo ndilo ambalo lilimfanya Mrisho Ngassa arudi zake Simba kisha Yanga baada kutimkia Azam nyakati zile. Labda pia ndio jambo lililomfanya Prince Dube atimkie zake Yanga baada ya kuweka mgomo baridi pale Chamazi.

Inawezekana pia kuna mkono wa kina Abuubakar Bakhresa inabidi ufike lakini bado haujafika. Huku dabi inachezwa huku wachezaji wengi bora wakiwa Mamelodi. Hakuna anayeona kitu cha ajabu.

Labda Azam watie pesa nyingi zaidi na kuchukua wachezaji wa maana zaidi ili tuamini mchezaji kama Fei anastahili kucheza katika timu yao.

Kama tunawadhulumu katika ligi basi wanaweza kutia pesa nyingi wakafanya mambo makubwa katika michuano ya CAF kiasi kwamba tutaamini kuwa mchezaji kama Fei Toto anaweza kucheza kwao.

Kwa hali ilivyo sasa inaonekana hata Pascal Msindo hatuamini anaweza kucheza Azam. Kitu kinachochekesha sana.

Inawezekana mazingira yetu ni magumu lakini huku Afrika Kusini hali ni shwari kabisa kwa Mamelodi. Wakubwa wamepiga magoti. Mamelodi kachukua ubingwa wa Afrika Kusini mara saba mfululizo.

Kudhihirisha hapa nyumbani hawabahatishi hawa wakubwa amechukua ubingwa wa Afrika mara moja na ameshindwa katika fainali mara tatu. ‘Fei Toto’ wa huku akitakiwa na Mamelodi haionekani kama anakwenda katika timu ambayo inafeli. Ni tofauti na Fei Toto wetu.

Wakati juzi ilikuwa dabi yao huku na Orlando Pirates akimchakaza mtani wake mabao 3-0, ikumbukwe wiki mbili tu zilizopita mbabe huyu bwana Orlando alikuwa amechakazwa mabao 3-1 na Mamelodi katika uwanja wake wa nyumbani.  Haya ndiyo maisha ambayo Azam walipaswa kuishi hapo nyumbani.