Prime
Mabadiliko Simba, Yanga yamedoda?
Muktasari:
- Na mara nyingi mabadiliko ambayo wanayoyaongoza wanataka waone mwisho wake ni yale ya bandia yanayofanywa kwa malengo fulani ama ya kuendelea kubaki madarakani kwa kuonyesha maendeleo yasiyo ya kweli ama maslahi mengine ya kisiasa.
NDIO, ni jambo la kawaida mabadiliko yoyote au mageuzi huchukua muda hadi yakamilike. La sivyo kuna uwezekano wa kuwa na mabadiliko bandia ambayo hayaakisi malengo yaliyokuwa yakielezwa awali.
Na mara nyingi mabadiliko ambayo wanayoyaongoza wanataka waone mwisho wake ni yale ya bandia yanayofanywa kwa malengo fulani ama ya kuendelea kubaki madarakani kwa kuonyesha maendeleo yasiyo ya kweli ama maslahi mengine ya kisiasa.
Pamoja na ukweli kwamba mabadiliko huchukua muda mrefu, bado kuna mambo yanayoweza kuwa yanachukuliwa kama hatua kuelekea malengo ya kweli kama kuna nia hasa ya kuitoa taasisi hatua moja na kwenda nyingine.
Na ishara hizo huwa na vipindi maalumu; kwamba baada ya miaka miwili kutakuwa na jambo fulani na baada ya miaka minne hatua fulani itakuwa imetimia hadi mabadiliko yakamilike.
Simba na Yanga, klabu kongwe za michezo nchini zilianza kwa kasi wimbo wa mabadiliko ya uendeshaji na umiliki ambao kwa sasa uko mikononi mwa wanachama.
Mabadiliko kama hayo yalishindikana miaka ya tisini wakati wafadhili watano wa Yanga, wakiongozwa na mfanyabiashara maarufu Abbas Gulamali walipojitoa kuifadhili klabu hiyo yenye makao yake makuu Jangwani jijini Dar es Salaam.
Yanga ilikuwa ikiwategemea wafadhili hao kwa kila kitu, kiasi kwamba ilionekana kwamba haikuwa inaweza kuingiza mapato yoyote ya kuilea timu ya soka kwa angalau siku moja.
Ilikuwa ni kama uamuzi wa wafadhili hao kujiondoa ni kutaka kushinikiza wanachama wamuondoe mwenyekiti Jabir Katundu na katibu wake mkuu, George Mpondela, ambao ilionekana walitofautiana katika uamuzi wao.
Lakini, Mpondela alimshika Katundu na kuweka msimamo kuwa wasingewanyenyekea wafadhili hao na kuibua hoja ya kuibadili klabu na kuwa kampuni ili iweze kujiendesha kifedha. Hatua hiyo ilihusu kubadili muundo wa umiliki na uendeshaji.
Hapo kukazuka mgawanyiko mkubwa wa wanachama baada ya wale waliokuwa wakitumiwa na wafadhili kupinga kwa nguvu uamuzi huo, huku kundi kubwa zaidi likiunga mkono Yanga kuwa kampuni.
Na ndipo yalipozuka makundi mawili ya Yanga Kampuni, lililotoka mageuzi na Yanga Asili, kundi lililotaka Yanga iendelee na mfumo wake wa wanachama kumiliki klabu, huku Mpondela akipachikwa jina la Castro kutokana na msimamo wake. Mpondela, akiungwa mkono na wafanyabiashara wazawa pamoja na kufunguliwa kwa kesi sehemu mbalimbali hadi mpango huo ulipokufa kabisa.
Ilishindikana kwa sababu mpango huo ulikuja kama mbadala wa mapema vikwazo ambavyo wangekumbana navyo.
Ingetegemewa wakati wa utulivu kama uliopo sasa hivi, mchakato wa mabadiliko ungeweza kuonekana na ishara kwamba klabu inapiga hatia zingekuwepo kwa klabu hiyo tangu ilipopitisha mabadiliko ya katiba miaka mitano iliyopita.
Lakini kikubwa kinachoonekana ni ubora na mafanikio ya timu ya soka ambayo ni sehemu ya shughuli za kimichezo za klabu hiyo, na mipango kabambe ya ujenzi wa miundombinu, hasa ujenzi wa uwanja mpya eneo ambalo ulikuwepo Uwanja wa Kaunda uliojengwa miaka ya sabini.
Lakini, ukihoji mabadiliko yamefikia wapi huwezi kupata jibu lililokamilika na utendaji na uendeshaji wa klabu hauonekani kutengeneza mazingira ambayo yangeinua macho ya hao wanaoweza kuwekeza fedha zao kwa kununua hisa kama sheria zinavyolazimisha kuwa idadi ya wawekezaji iwe kuanzia wawili.
Uwepo wa mdhamini unaonekana kama umekuwa mkubwa zaidi, kiasi kwamba ni kama vile klabu haiwezi kufanya lolote zaidi ya kampuni hiyo, ambayo kimsingi ni mdhamini wa vifaa na si sehemu ya waendeshaji na wamiliki.
Kwa kifupi, inaonekana kama mchakato wa mabadiliko umesimama na uongozi umejikita katika uendeshaji timu ya soka na miundombinu yake.
Hali ni kama hiyo kwa klabu ya Simba ambayo mchakato wake wa mabadiliko ulikumbana na vikwazo vya kisheria na kanuni za umiliki ambazo kama nilivyoeleza awali zinataka idadi ya wawekezaji inatakiwa iwe kuanzia wawili kwenda juu.
Mpango wa Simba ulianza kama kutekeleza matamanio ya mfanyabiashara Mohamed Dewji, aliyedokeza awali kuwa yupo tayari kuweka mezani Sh20 bilioni anunue hisa za klabu hiyo.
Kauli yake ikafuatiwa na uamuzi wa kubadili mfumo wa umiliki na baadaye kufanya tathmini.
Lakini ilipofikia kuanza utekelezaji, serikali ikaitaka ifuate kanuni hiyo ya umiliki na hivyo mchakato kukwama kwa takriban miaka nane kabla ya mabadiliko ya katiba kupitishwa mwaka huu, lakini yakiwa na vikwazo ambavyo vimesababisha mchakato usiendelee.
Nao kwa sasa ni kama mchakato umekwama na akili imehamia kwenye ubingwa zaidi, huku fedha ambazo Dewji alionyesha waandishi wa habari kuwa anakabidhi lakini zimeshaingizwa kwenye akaunti, zikiwa zimewekwa kwenye kile kinachodaiwa akaunti maalumu.
Hizi klabu zilitakiwa ziwe na kamati za mabadiliko ambazo kazi yake ingekuwa ni kusimamia mchakato wa mabadiliko na kutoa taarifa za maendeleo yake kila baada ya kipindi fulani.
Kuwaachia viongozi waendelee na shughuli za kila siku za klabu na hapohapo kuendesha mchakato haikuwa jambo jema kwa kuwa viongozi wanaweza kuona mabadiliko ni kuathiri matamanio yao na hivyo kutojisukuma kuendelea na mchakato.
Na kwa kuwa furaha ya wanachama ni ushindi uwanjani, juhudi kubwa zitaelekezwa huko ili yeyote anayejaribu kuhoji maendeleo ya mabadiliko aonekane anataka kuvuruga furaha ya wanachama ambayo inaonekana dhahiri uwanjani.
Si vibaya kama wanachama na viongozi wakaliona hili na kufanya marekebisho kidogo mchakato wa mabadiliko ili kuweka wasimamizi ambao watawajibika kutoa taarifa za maendeleo ya mageuzi yaliyopitishwa na wanachama.