Makosa 10 ya Urembo ngozi yako itazeeka haraka
Muktasari:
- Wengine wananunua kila bidhaa mpya inayotoka sokoni wakiamini ngozi nzuri inapatikana kwa kutumia vitu vingi, wengine wanalala na vipodozi usoni, hawanywi maji ya kutosha na jambo la kushangaza zaidi hawatumii hata kinga ya jua.
Kuna watu ukikutana nao utasikia wanasema, “Sijui kwa nini ngozi yangu imeanza kuchoka mapema,” lakini ukifuatilia maisha yao ya kila siku unagundua tatizo si umri bali ni namna wanavyoitunza ngozi.
Wengine wananunua kila bidhaa mpya inayotoka sokoni wakiamini ngozi nzuri inapatikana kwa kutumia vitu vingi, wengine wanalala na vipodozi usoni, hawanywi maji ya kutosha na jambo la kushangaza zaidi hawatumii hata kinga ya jua.
Ukweli ni kwamba ngozi haichoki kwa sababu ya miaka pekee, mara nyingi inachoshwa na sisi wenyewe. Tabia tunazoziita za urembo wakati mwingine ndizo zinazoharakisha mikunjo, kufanya ngozi ikauke na kupoteza ule mng’ao wa asili. Wakati watu wanahangaika kutafuta siri za kuonekana vijana muda mrefu, majibu mengine yapo kwenye mambo madogo tunayoyafanya kila siku bila kufikiria.
Haya ni makosa 10 ya urembo ambayo yanaweza kuharakisha kuzeeka kwa ngozi bila wengi kutambua:
1. KUTOKULALA VYA KUTOSHA
Usingizi ni muda ambao mwili hujirekebisha na kuhuisha seli zake. Ukikosa usingizi wa kutosha mara kwa mara, ngozi inaweza kuonekana imechoka, kupoteza mng’ao na hata kuanza kupata mistari midogo mapema (makunyanzi). Kulala kwa muda unaotosha husaidia ngozi kupata nafasi ya kujitengeneza upya.
2. KUTOTUMIA KINGA YA JUA (Sunscreen)
Miale ya jua ni moja ya sababu kubwa zinazochangia kuzeeka kwa ngozi. Watu wengi hutumia vipodozi lakini husahau hatua hii muhimu. Miale ya UV inaweza kusababisha madoa, mikunjo na kupunguza uimara wa ngozi. Hata ukiwa ndani au siku yenye mawingu, ngozi bado inaweza kuathirika.
3. KUTUMIA BIDHAA NYINGI
Si kila bidhaa inayotangazwa inafaa kuingia kwenye ratiba yako ya urembo. Kuchanganya bidhaa nyingi kunaweza kuifanya ngozi ichanganyikiwe, kukauka au kupata muwasho. Ngozi inapopoteza kinga yake ya asili huanza kuonyesha dalili za uchovu na kuzeeka mapema.
4. KUSAFISHA USO KUPITA KIASI
Usafi ni muhimu lakini kusafisha uso mara nyingi kupita kiasi kunaweza kuondoa mafuta ya asili yanayolinda ngozi. Ngozi inapokosa ulinzi huo huanza kukauka na kuwa dhaifu, usioshe uso na dodoki gumu.
5. KUTOKUNYWA MAJI
Maji yana mchango mkubwa katika afya ya ngozi. Upungufu wa maji mwilini unaweza kuifanya ngozi ionekane kavu, isiyo na uhai na kuongeza mwonekano wa mikunjo.
6. KULALA NA VIPODOZI USONI
Baada ya siku ndefu, wengine hulala bila kuondoa vipodozi. Hili linaweza kuziba vinyweleo na kufanya ngozi ishindwe kupumua vizuri. Hali hii inaweza kuathiri ubora wa ngozi.
7. KULA BILA KUIZINGATIA AFYA YA NGOZI
Ngozi inaathiriwa pia na kile tunachokula. Ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi au mafuta unaweza kuathiri mwonekano wa ngozi. Lishe yenye matunda, mboga na virutubisho mbalimbali huisaidia ngozi kubaki katika hali nzuri, vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi husababisha chunusi.
8. KUGUSA USO MARA KWA MARA
Tabia ya kushika uso bila sababu inaweza kuhamisha uchafu na mafuta kutoka mikononi kwenda usoni. Hii inaweza kuongeza muwasho na matatizo mengine ya ngozi.
9. KUTOTUNZA NGOZI YA MWILI MZIMA SIO USO PEKEE
Watu wengi hujikita kwenye uso pekee na kusahau maeneo mengine yanayoonyesha umri kwa haraka. Shingo na mikono pia vinahitaji utunzaji sawa na uso.
10. KUFUATA KILA TREND YA UREMBO
Kitu kinachomfaa mtu mwingine si lazima kikufae. Kutumia bidhaa au mbinu bila kuelewa mahitaji ya ngozi yako kunaweza kuleta madhara badala ya matokeo mazuri.
USHAURI
Urembo wa kweli hauanzi kwenye chupa ya bidhaa bali kwenye tabia za kila siku. Ngozi yenye afya si lazima iwe kamili, lakini mara nyingi huonekana vizuri pale inapopewa muda wa kupumzika, kulindwa na kutunzwa kwa usahihi. Kabla ya kuongeza bidhaa nyingine kwenye ratiba yako ya urembo, jiulize kwanza kama ngozi yako kweli inaihitaji.