Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lupekenya: Kutoka Ligi Kuu Bara hadi daraja la kwanza Zanzibar

Muktasari:

  • Lupekenya sio jina geni kwa mashabiki wanaofuatilia Ligi Kuu Bara, kwani nyota huyo alijiunga na Coastal Union msimu wa 2022-2023, baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa na kikosi cha KMKM FC cha visiwani Zanzibar msimu wake wa 2021-2022.

MAISHA yana milima na mabonde, lakini, kila changamoto unayopitia leo inakujenga uwe na nguvu na hekima ya kufikia kesho yako bora zaidi, hivyo ndivyo ilivyo sasa kwa aliyekuwa mshambuliaji nyota wa Coastal Union, Optatus Yustine Lupekenya.

Lupekenya sio jina geni kwa mashabiki wanaofuatilia Ligi Kuu Bara, kwani nyota huyo alijiunga na Coastal Union msimu wa 2022-2023, baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa na kikosi cha KMKM FC cha visiwani Zanzibar msimu wake wa 2021-2022.

Msimu wa 2021-2022 Lupekenya aliifungia KMKM mabao 19 katika Ligi Kuu ya Zanzibar akishika nafasi ya pili nyuma ya mfungaji bora wa KVZ, Maabad Maulid aliyefunga 21 ambao wote pamoja waliungana tena katika kikosi cha Coastal Union.

Lupekenya alijiunga na Coastal Union msimu huo wa 2021-2022 sambamba na kiungo Greyson Gerald Gwalala aliyekuwa pia anaichezea KMKM ambaye hadi leo na Maabad bado wanaendelea kukitumikia kikosi hicho cha ‘Wagosi wa Kaya’ kutoka Tanga.

Gwalala na Maabad wamekuwa ni muhimili mkubwa kwa kikosi hicho cha Coastal Union katika eneo la kiungo na ushambuliaji tangu walipojiunga nayo msimu wa 2021-2022, japo kwa Lupekenya ameamua kuanza upya baada ya changamoto za hapa na pale.

Maisha ya Lupekenya Coastal Union hayakuwa mazuri kwani licha ya kusaini mkataba wa miaka miwili, ila aliutumikia mmoja tu kisha kurejea Zanzibar ambapo kwa sasa anaichezea Raskazone inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja.

Kutokana na matumaini makubwa aliyokuwa amebeba nyota huyo tangu akiwa Ligi Kuu ya Zanzibar hadi Ligi Kuu, Mwanaspoti limemtafuta na kupiga naye stori ambapo amefunguka mambo mengi na malengo yake kwa sasa ya kurejea katika kiwango bora.


FURSA YA KUKUZA SOKA

Nyota huyo anasema kusajiliwa na Coastal Union ilikuwa ni fursa nzuri kwake ya kukuza soka zaidi nje ya mipaka ya Ligi ya Zanzibar jambo ambalo kwa mchezaji yeyote hutamani kuona likitokea hususani unapoenda sehemu iliyopiga hatua kubwa.

“Unapoenda sehemu ambayo ligi yake ni kubwa na ina wachezaji wazuri hata wewe mwenyewe unaona kuna mafanikio unapata niliona bahati kwangu na kuamini ni muda wa kuzidi kuonyesha kiwango changu, japo, bahati mbaya sikufanikiwa,” anasema.

Lupekenya anasema sababu iliyochangia kushindwa kuonekana zaidi katika Ligi Kuu Bara ni kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, jambo ambalo ukiwa mchezaji ni ngumu kukabiliana nalo hasa ukiwa umebeba pia matarajio makubwa.

BARA SIO MCHEZO

Nyota huyo anasema Ligi Kuu Bara inahitaji sana matumizi ya nguvu na akili ndani ya uwanja, jambo ambalo ni tofauti na Ligi ya Zanzibar, ambayo licha ya kufanana kwa baadhi ya mambo, ila kuna utofauti kwa namna ya uchezaji kwa wachezaji.

“Ligi ya Zanzibar ni ngumu sana kwa sababu ya ushindani uliopo, ila ni tofauti kidogo na Tanzania Bara kwa sababu huko unakutana na wachezaji wanaotoka sehemu mbalimbali, sasa ukiachana na matumizi ya nguvu, ila unajifunza pia,” anasema.

Lupekenya anasema Ligi zote hazina pia tofauti kubwa, isipokuwa mojawapo ya vitu ambavyo vimeifanya Bara kukua zaidi ni kutokana na muingiliano wa wachezaji wengi kutoka mataifa mbalimbali, jambo ambalo linaongeza ushindani mkubwa na mvuto.

MSAADA WA MAKOCHA

Wakati wa kipindi kigumu mshambuliaji huyo anasema alikuwa anapata msaada mkubwa kutoka kwa wachezaji wenzake kwa ajili ya kumjenga kiakili, ingawa mabadiliko ya mara kwa mara ndani ya kikosi cha Coastal Union nayo yalikuwa ni changamoto.

“Kuna baadhi ya makocha waliokuwa wananijenga kwa maana ya kiakili na kimwili ili kuhakikisha nafanya vizuri, japo kwa wengine ilikuwa ni tofauti kidogo, kwangu nilichukulia ni kawaida na changamoto kama zilivyo pia changamoto zingine.”

Mshambuliaji huyo anasema mchezaji anapopitia nyakati ngumu ni muhimu kwa benchi la ufundi kukaa naye chini na kuangalia changamoto anazopitia, kwa sababu kwa kufanya hivyo itakuwa ni chachu ya kumtengeneza vizuri kwa maana ya kisaikolojia.


AVURUGWA KISAIKOLOJIA

Anasema kushindwa kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara kulimuathiri kisaikolojia kwa sababu aliona malengo yake na kile alichokikusudia kukifanya kinaenda tofauti, hivyo alipitia kipindi kigumu japo kwa sasa anapambana kurejea tena upya.

“Dhamira yangu ilikuwa kutoka Zanzibar na kuja Bara, nashukuru kipindi kile nilifanikiwa, ingawa malengo yangu baada ya kufika yalikuwa ni tofauti, nimekubaliana na yote yaliyotokea mwanzoni na nimeamua kuanza tena upya,” anasema Lupekenya.

Lupekenya anasema haamini kama alifeli katika Ligi Kuu Bara, isipokuwa mazingira tofauti na aliyotokea ilikuwa ni moja ya changamoto zilizotokea ambazo ni za kawaida kwa mchezaji yeyote kwa sababu wapo wengi tu ambao imeshawatokea mwanzo.

“Kufanya vizuri sehemu moja haina maana unapoenda unaweza ukafanya vilevile, unahitaji muda wa kuzoea mazingira tofauti na uliyotoka, kwa sababu hata wachezaji unaoenda kukutana nao kwenye timu husika wana falsafa zao za kiuchezaji pia.”


KUTOKATA TAMAA

Mojawapo ya jambo kubwa na la muhimu kwa nyota huyo alilojifunza kwa kipindi cha mwaka mmoja aliocheza Ligi Kuu Bara ni kutokata tamaa kwa kila alichopitia, kwani mitihani mbalimbali inayotokea kwa binadamu ni sehemu ya kujifunza maishani.

“Licha ya kutotimiza malengo yangu ila, nilichojifunza ni kutokata tamaa, niliamini bado nina nafasi ya kufanya vizuri hata kama nikiwa sehemu nyingine, ukiwa mchezaji au mtu yeyote usichoke kuamini kile unachokiamini,” anasema Lupekenya.

Nyota huyo anasema katika maisha kila kitu kinatokea kwa sababu na mipango pia ya Mwenyezi Mungu, hivyo unapokata tamaa maana yake umeamua kuonyesha unyonge wako, jambo ambalo kwake hawezi kulipa kipaumbele bali ni fursa ya kupambana zaidi.


GOTI LAMTIBULIA

Nyota huyo anasema baada ya kurejea Zanzibar na kujiunga na Mlandege, malengo yake yalikuwa ni kufanya vizuri ili iwe nafasi nyingine kwake ya kuonekana na kupata shavu la kuja Tanzania Bara kupambana, japo majeraha ya goti yalimuharibia.

“Wakati napambana kurejea katika kiwango changu, nilipata majeraha ya goti yaliyoniweka nje kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, jambo hilo liliniathiri sana kiakili kwani, nilikaa kwa muda mrefu bila ya timu ya Ligi Kuu,” anasema Lupekenya.

Nyota huyo anasema sababu iliyochangia kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu ni kutokana na kucheza mechi huku akiwa amechomwa sindano za kutuliza maumivu, ingawa kwa sasa amejifunza na anapambania kurejesha kiwango chake.

“Majeraha hayo yaliniathiri sana kuanzia kiakili na hata kisaikolojia kwa sababu nilikuwa naona ndoto zangu za kucheza mpira zimeisha, nilichokifanya ni kujipa matumaini na nashukuru pia nimeanza kuona mwanga uliopo mbele yangu,” anasema.

MTAZAMO CHANYA

Licha ya nyota huyo kwa sasa kuichezea Raskazone FC, inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja, ila kwake sio jambo la kujutia katika maisha yake, kwa sababu kwa hali aliyopita hasa ya majeraha ilikuwa ni lazima kuanza tena upya.

“Niliona kuanza moja ni sehemu ya kujifunza, nimejiunga nayo kwa lengo la kuzidi kuimarisha kiwango changu hasa baada ya kukaa nje kwa muda mrefu, nawashauri na wengine wasikate tamaa kwa sababu changamoto zipo kwa ajili ya kujifunza pia.”

Nyota huyo anasema malengo yake kwa sasa ni kuipambania timu hiyo ya Raskazone ipande Ligi Kuu ya Zanzibar kisha baada ya hapo ndipo atakapojua mustakabali wake ikiwa ataendelea kuichezea kwa msimu ujao au atatafuta changamoto pia mpya.

“Malengo na akili yangu kiujumla nimeyaweka hapa Raskazone FC napambana kwa ajili ya kuipandisha Ligi Kuu ya Zanzibar, ili iwe fursa nyingine ya mashabiki zangu kuniona katika madaraja ya juu kama ambavyo walivyonizoea,” anasema Lupekenya.