LUKINDO: Winga alitua Ligi Kuu, akimpigia saluti Maxi

Muktasari:
- Mchezaji huyo aliwahi kuichezea Ligi Kuu akiwa na Mbao FC akishuka nayo msimu wa 2019/2020 kabla ya kutimkia Mbeya City ambako alitumia muda mwingi nje ya uwanja akiuguza majeraha ya goti kabla ya kutemwa na kurejea Ligi ya Championship akiwa na Pamba Jiji na baadae Biashara United
BAADA ya msoto wa miaka miwili akijitafuta katika Ligi ya Championship, hatimaye msimu uliomalizika wa ligi hiyo winga Herbert Lukindo amejipata kwa kuonyesha kiwango kikubwa na kuzivutia timu kadhaa na kama zali amejikuta akirejea katika Ligi Kuu Bara kwa msimu mpya utakaoanza mwezi ujao.
Mchezaji huyo aliwahi kuichezea Ligi Kuu akiwa na Mbao FC akishuka nayo msimu wa 2019/2020 kabla ya kutimkia Mbeya City ambako alitumia muda mwingi nje ya uwanja akiuguza majeraha ya goti kabla ya kutemwa na kurejea Ligi ya Championship akiwa na Pamba Jiji na baadae Biashara United.
Akiwa na Biashara iliyomaliza nafasi ya nne na kucheza play-of dhidi ya Tabora United, nyota huyo aliupiga mwingi kwani katika mechi 31 alifunga mabao 11 na asisti sita, huku akikumbukwa kwa bao la penalti katika mchezo wa play-off kuwania kupanda daraja dhidi ya Tabora United na kuzusha vurugu kubwa kabla ya tmu hiyo kung'olewa Ali Hassan Mwinyi kwa kufungwa mabao 2-0, kiwango alichoonyesha kimembeba.
Timu ya KenGold iliyopanda daraja kama Pamba Jiji imemnyakua na mwamba huyo msimu ujao atakinukisha huko.
KIWANGO KIMEMBEBA
Msimu uliopita wa Ligi ya Championship ulikuwa bora kwa winga huyo mshambuliaji wa Biashara United akifunga mabao 11 na assisti sita katika mechi 31, ambapo anaamini ubora huo ndiyo umezivutia timu nyingi ikiwemo Ken Gold ambayo imemsajili na kumrejesha Ligi Kuu.
“Siri ya ubora niliokuwa nao ni kujituma na kusikiliza nini walimu wanataka kifanyike ndiyo kimepelekea kuwa na msimu bora kwangu na hata kwa timu tumepambana kadri ya uwezo wetu hadi kufika pale,”
“Siku hizi Ligi ya Championship inaonyeshwa kwenye televisheni, hii imerahisisha watu kufuatiliaa mchezaj au timu kwahiyo inakua rahisi kupata timu kama umefanya vizur zaidi,” anasema Lukindo
"Siri ya Biashara Utd kufanya vizuri msimu uliopita kwenye Championship ni uongozi na benchi la ufundi walisajili wachezaji wazuri na wapambanaji, pia timu ilikuwa na upendo sana kwahiyo ilikua rahisi kufanya kazi kwa pamoja.”
KWANINI KENGOLD?
Lukindo anarejea Ligi Kuu baada ya kukosekana kwa takribani misimu mitatu tangu aliposhuka daraja na Mbao FC mwaka 2020, baada ya kusaini KenGold, huku akifunguka sababu za kutua kwa wachimba dhahabu hao wa Mbeya.
“Ni kweli timu nyingi zilituma ofa kunihitaji lakini niliichagua Ken Gold kwa sababu ukiachana na maslahi KenGold walikuwa na nia kubwa ya mimi kuja kucheza hapa tangu tukiwa Ligi ya Championship, ndiYo maana mapema tu walihitaji mimi kutua hapa,” anasema Lukindo.
BAO LA UTATA
Moja ya matukio ya kusisimua kwenye soka la Tanzania msimu huu ni tukio la bao la utata la penalti katika mchezo wa mtoano (playoff) kuwania kwenda Ligi Kuu kati ya Biashara United dhidi ya Tabora United kwenye Uwanja wa Karume, Musoma.
Katika tukio hilo, mshambuliaji wa Biashara United, Herbert Lukindo alifunga penalti ambayo ilitoboa nyavu na kuzua vurugu wachezaji wa Tabora United wakidai siyo bao kwani mpira umetoka nje, ambapo Lukindo anazungumzia tukio hilo.
“Kiukweli ile penalti inabaki kwenye kumbukumbu zangu siku zote mpigaji lazima uangalie mpira hadi mwisho kwahiyo mimi nilikua na uhakika kuwa lile ni goli ndiyo maana nilishangilia,” anasema Lukindo
MZIKI WA MAXI
Licha ya uwepo wa wachezaji wengi wazawa na wa kimataifa wanaosakata kabumbu nchini, Lukindo anavutiwa na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Max Nzengeli raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Wachezaji wapo wengi wanaonivutia uchezaji wao ila Max Nzengeli jamaa ni mpambanaji sana na anajua mpira,” anasema Lukindo.
Kuhusu kurudi Ligi Kuu na namna alivyojiandaa na kuwa na mwendelezo wa kiwango bora, Lukindo anasema “Miaka miwili nimecheza Championship nadhani nimejivunza mengi sana kwahiyo nimerudi Ligi Kuu kupambana kuendeleza nilipoishia naamini nitafanya vizuri zaidi.”
Lukindo anasema tabia ya baadhi ya timu zinazopanda kutoka Championship kuachana na sehemu kubwa ya wachezaji wake ni jambo ambalo linategemeana na namna walivyoishi nao na mahitaji yao, hivyo hawezi kuwalaumu.
“Hili ni swali gumu sana kulijibu maana huwez jua waliishi vipi na hao wachezaji kwahiyo kuna sababu nyingi nadhani zinazopelekea wao kufanya hayo maamuzi,” anasema
PENALTI YAMLIZA
Lukindo anasema tukio ambalo lilimnyima usingizi msimu uliopita ni kukosa penalti kwenye mchezo muhimu wa kutafuta nafasi ya kupanda Ligi Kuu dhidi ya Pan African na kupelekea timu hiyo kutoka kwenye mbio za kupanda daraja.
“Yapo matukio mengi ila la kukosa penalti mechi na Pan African iliniuma sana maana tulikua nyuma 2-1 na dakika za jioni kabisa kwa sababu sijawahi kukosa penalti kwahiyo watu wote walijua nafunga, hii ilikua mbaya sana kwangu kiukweli,” anasema.
Akizungumzia pacha aliyecheza naye Biashara, Boban Zurintusa, raia wa Uganda (mabao 21) katika safu ya ushambuliaji iliyotisha Ligi ya Championship, Lukindo anasema “Nafikiri ilikua nzuri sana siyo mimi tu na Boban yeyote unaecheza nae Biashara mtashirikiana vizuri ndiyo maana karibu wachezaji wote walifunga mabao,”
ALIKOPITA/TAKWIMU
Mshambuliaji huyo ameanzia safari yake ya soka jijini Tanga katika kituo cha Eagle Rangers Sport Academy, JKT Mgambo, Ndanda, Mbao FC,Mbeya City, Pamba, Biashara United na sasa Ken Gold.
“Nikiwa Mbao nilitengezeza sana magoli kuliko kufunga nilitoa assisti tisa na magoli matatu, Mbeya City niliumia goti sikupata sana nafasi ya kucheza nilifunga magoli mawili, nikaja Pamba nilifunga magoli sita na assisti nne, msimu huu nikiwa Biashara nimefunga magoli 11 na assisti sita,” anasema Lukindo