LIVE KUTOKA MISRI: Ratiba ipo poa, lakini...

MOALLIN: Tunajenga timu mpya, furaha

AZAM FC bado ipo kambini mjini El Gouna, Misri na juzi usiku ilicheza mechi ya pili ya kujipima nguvu dhidi ya Grand na kushinda bao 1-0 lililowekwa kimiani na nyota mpya, Tape Edinho, lakini mapema mchana jijini Dar es Salaam Tanzania, Bodi ya Ligi (TPLB) ilitangaza ratiba ya Ligi Kuu.

Benchi la ufundi la Azam pamoja na uongozi na wachezaji waliopo kambini mjini El Gouna, Misri wameipokea kwa hisia tofauti ratiba hiyo ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2022-2023.

Ratiba inaonyesha baada ya mechi ya Ngao ya Jamii kabla ya ligi kuanza Agosti 15 na kumalizika Mei 27 mwakani na Kocha Mkuu Abdihamid Moallin, amesema uwiano wa mechi za nyumbani na ugenini umekaa vizuri hivyo kuzipa timu nafasi ya kujipanga vizuri nyumbani baada ya mechi ngumu za ugenini.

“Kucheza mechi nyingi za ugenini kwenye viwanja vigumu vya mikoani ni hatari sana hivyo kurudi nyumbani ni kuipa timu nafasi nzuri ya kurekebisha makosa yao katika mazingira yaliyozieleka.”

Nahodha Aggrey Morris amefurahishwa na muda wa kutoka mechi moja hadi nyingine akisema unawapa wachezaji muda mzuri wa kumpumzika na kukusanya nguvu kabla ya mchezo mwingine.

“Unajua ligi yetu ni ngumu sana. Kwa hiyo mechi zikiwa karibu karibu zinatuchosha sana wachezaji na kupunguza uwezo wetu halisi.”

Lakini Morris ambaye ni mmoja wa wachezaji wazoefu sana kwenye ligi yetu, anatoa wito kwa bodi ya ligi kuisimamia ratiba hiyo kwa maslahi ya mpira wetu.

Morris anasema ratiba inaonesha muda wa mchezo lakini hutokea mabadiliko ya ghafla ya muda wa mchezo na kuvuruga kila kitu.

“Kwa mfano sisi tunaathirika sana na mabadiliko ya ghafla ya muda wa mchezo. Utakuta mechi yetu ya saa moja usiku inabadilishwa ghafla kuwa ya saa nane, kama ilivyotutokea dhidi ya Alliance mwaka ule”.

Hapa Morris alikuwa anakumbushia mchezo wa Azam na Alliance msimu wa 2029/20 ambao ulipangwa kufanyika Machi 7, 2020, saa moja usiku uwanja wa Mkapa.

Lakini Saa 4 asubuhi wakapewa taarifa kwamba mechi yao imehamishiwa uwanja wa Uhuru na itafanyika saa nane mchana.

Mambo haya ya kubadilisha muda pia yalishawahi kimuingiza matatani Aggrey baada ya sare ya 2-2 dhidi ya JKT Tanzania, ambapo mchezo ulipangwa kufanyika saa 10 jioni lakini asubuhi ya siku ya mchezo ukahamishiwa saa moja usiku.

Katika mahojiano ya baada ya mchezo, Morris akasema ligi imekuwa kama mafungu ya samaki.

Kauli hii ilimuingiza matatani na mamlaka kiasi cha kushitakiwa kamati ya saa 72.

Mkuu wa idara ya habari ya Azam, Zaka Zakazi, anatilia shaka ratiba hiyo kuipanga Azam kupita njia moja na Simba SC.

“Msimu uliopita tulipita njia moja na KMC. Msimu wa nyuma yake kabisa ilikuwa Namungo. Msimu huu ni Simba.

Yaani sisi tukicheza na timu X, Simba wanacheza na timu Y, mechi ijayo sisi tutacheza na timu Y iliyocheza na Simba mechi iliyopita, na wao watacheza na timu X ambayo tulicheza nayo sisi.

Hii kitu itatupa ugumu sana kwa sababu tutakuwa tunakutana kila mji tunaoenda. Kwa mfano, siku ya ufunguzi wa ligi, sisi tutacheza na Kagera Sugar na wao watacheza na Geita.

Mechi zinafuata, sisi na Geita wao na Kagera Sugar. Halafu tutaenda kukutana Mbeya. Sisi tutacheza na Mbeya City, wao na Tazania Prisons. Halafu sisi na TZ Prisons na wao na Mbeya City.

Hii itakuwa msimu msimu...usiombe kupita njia moja na Simba na Yanga, utakuwa na wakati mgumu sana.

Ratiba ya Ligi Kuu kwa msimu wa 2022/23 imetolewa na Bodi ya Ligi Agosti 3 ikionesha Azam itaanzia nyumbani mechi mbili za kwanza, dhidi ya Kagera Sugar, Agosti 17 na dhidi ya Geita Gold Agosti 21.

Ifuatayo ni ratiba kamili ya Azam FC kwa mechi za duru la kwanza ya Ligi Kuu Bara.


Agosti 17

v Kagera Sugar - nyumbani

Agosti 21

v Geita Gold - nyumbani


Septemba 6

v Yanga - ugenini


Septemba 13

v Mbeya City - ugenini


Septemba 30

v TZ Prisons - ugenini


Oktoba 3

v Singida Big Stars - nyumbani


Oktoba 12

v Dodoma Jiji - nyumbani


Oktoba 22

v KMC - ugenini


Oktoba 27

v Simba - nyumbani


Oktoba 31

v Ihefu - nyumbani


Novemba 12

v Mtibwa Sugar - ugenini


Novemba 15

v Ruvu Shooting - nyumbani


Novemba 20

v Namungo - ugenini


Novemba 27

v Coastal Union - nyumbani


Disemba 5

v Polisi Tanzania - ugenini