Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ligi Kuu yamoto… Wazawa, wageni wapangiwa vikosi

HAPO Pict

Muktasari:

  • Katika eneo la chini, wageni wa ligi hiyo, KenGold wanaendelea kuburuza mkia wakiwa na pointi 16, wakizibeba timu zote wakifuatiwa juu yake ya Tanzania Prisons yenye pointi 18 na Kagera Sugar ikiwa nafasi ya 14 kwa pointi 19 katika janga la kushuka daraja.

LIGI Kuu Bara imesimama baada ya jana kupigwa mechi ya kiporo kati ya Simba na Dodoma Jiji, ili kupisha kalenda ya mechi za kimataifa kwa timu za taifa zinazochuana kusaka tiketi ya kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026.

Kabla ya mechi ya jana, tayari zilishapigwa mechi 180 na kufungwa jumla ya mabao 400, huku nyota wa kigeni 57 wakifunga mabao 175 ikiwa ni wastani wa mabao matatu kwa kila mechi, ilihali wazawa 201 wamefunga mabao 213, sawa na kufunga mabao mawili katika kila mchezo. Lakini kuna mabao mengine 13 ambayo wachezaji wamejiweka wenyewe nyavuni katika harakati za kuokoa.

Wakati ligi ikienda mapumzikoni hadi Aprili Mosi, watetezi Yanga wapo kileleni wakikusanya pointi 58 kupitia mechi 22, ilihali Simba iko nafasi ya pili, huku Azam ikishika nafasi ya tatu na pointi 48 kwa mechi 23, sawa na michezo iliyocheza Singida iliyopo nafasi ya nne kwa alama 44.

Katika eneo la chini, wageni wa ligi hiyo, KenGold wanaendelea kuburuza mkia wakiwa na pointi 16, wakizibeba timu zote wakifuatiwa juu yake ya Tanzania Prisons yenye pointi 18 na Kagera Sugar ikiwa nafasi ya 14 kwa pointi 19 katika janga la kushuka daraja.

Ligi imesimama kukiwa pia na mchuano mkali wa wafungaji mabao ambapo kabla ya mechi ya jana, Clement Mzize wa Yanga alikuwa mzawa pekee anayechuana na nyota wa wageni, Prince Dune (Yanga) na Jean Charles Ahoua (Simba) kileleni katika orodha ya wafungaji kila mmoja akiwa na 10.

HAP 01

Mkenya Elvis Rupia wa Singida Black Stars anafuata nyuma yao akiwa mabao tisa, huku orodha ndefu ikimfuata nyuma yake kwa waliofunga mabao kati ya manane na saba ikiwa na sura mseto kwa wazawa na wageni.

Kwa ujumla Ligi imesaliwa na jumla ya mechi 59 ili kukamilisha raundi saba zilizosalia, ikiwamo pambano la Dabi ya Kariakoo lililoshindikana kufanyika Machi 8 na ndipo itakapofahamika bingwa wa msimu huu na washindi wengine wawili wataoungana na bingwa wa Kombe la Shirikisho kushiriki michuano ya kimataifa ya CAF kwa msimu ujao, huku mbili za mwisho zikishuka daraja moja kwa moja.

Hata hivyo, wakati ligi ikisimama, kuna mastaa waliofanya vyema katika mechi 181 za raundi 23 zilizopita kutokana na viwango walivyoonyesha na kuzibeba timu wanazozitumika katika ligi hiyo, sambamba na makocha walioziongoza timu zao kufanya vyema hadi wakati huu.

Kwa namna makocha na wachezaji walivyojipambanua, Mwanaspoti limekuletea vikosi vitatu tofauti kupitia mechi zilizochezwa ambavyo vinaundwa na baadhi ya wachezaji waliofunika hadi sasa katika ligi hiyo, kimoja cha wazawa, kingine cha nyota wa kigeni na kingine chenye mseto wa nyota hao.

HAP 02

Yaani kama itatokea ikaandaliwa mechi moja kali basi vikosi hivyo vinaweza kushuka uwanjani na kuonyeshana kazi kwa maana ya kikosi cha wazawa na kile cha wageni na huenda pakachimbika kwa aina ya wachezaji wanaoviunda na makocha watakaosimamia.


WAZAWA

Kikosi chao kinaundwa na kipa Yakoub Suleiman anayekipiga (JKT Tanzania) aliyeisaidia timu hiyo kushika nafasi ya sita ikiwa ndio timu inayoongozwa na kocha mzawa ambayo imefanya vizuri hadi sasa na pia ikiruhusu mabao machache zaidi kulinganisha na timu nyingine nje ya Simba, Yanga na Azam FC.

JKT imefungwa mabao 17 ikishika nafasi ya nne nyuma ya timu zilizoruhusu mabao machache baada ya Simba (8), Yanga (9) na Azam (12), huku kipa huyo akiwa na clean sheet nane kama alizonazo Yona Amos wa Pamba ambaye anaingia katika kikosi hiki kama kipa wa akiba.

Mabeki wa pembeni wa kikosi hicho ni Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wote wa Simba ambao wamekuwa na kiwango bora kwa muda mrefu na msimu huu wameendeleza moto wao, licha ya kuwepo kwa mabeki wengine wa pembeni wanaochuana nao.

Kabla ya mechi za jana, Kapombe alikuwa na mabao matatu na asisti tatu, wakati Tshabalala alikuwa na bao moja na asisti tatu.

Mabeki wa kati ni Ibrahim Bacca na Dickson Job ambao wameifanya Yanga kuwa na ukuta imara na ulioiwezesha kukaa kileleni kwa muda mrefu ikifungwa mabao tisa tu hadi sasa nyuma ya Simba, mbali na kulinda lakini Bacca ameifungia Yanga mabao manne, akiwa mmoja ya nyota wenye mabao mengi.

HAP 03

Viungo wa kikosi hiki ni Yusuf Kagoma wa Simba na Seleman Rashid Bwenzi wa KenGold aliyeingia dirisha dogo na hadi sasa ameonyesha uwezo mkubwa wa kuibeba timu hiyo akiifungia mabao matano katika mechi saba.

Kagoma aliyesajiliwa msimu huu kutoka Singida Fountain Gate amekuwa mmoja wa viungo imara katika uzuiaji na kuifanya Simba iwe na utulivu kiasi cha kuwafanya mabeki wa timu hiyo na kipa Moussa Camara kuwa na utulivu na kuwa moja ya timu isiyopitika kirahisi katika Ligi Kuu Bara.

Kiungo mwingine anayeingia katika kikosi hicho ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye amekuwa na muendelezo mzuri tangu msimu uliopita alipomaliza kama mfungaji wa pili na mabao 19 na asisti saba. Kwa sasa kiungo mshambuliaji huyo aliyeifanya Azam kuwa tishio amefunga mabao manne na asisti 11 akiwa ndiye kinara wa pasi za mwisho zilizozaa mabao katika ligi.

Washambuliaji wa kikosi hiki ni Offen Chikola wa Tabora United, Clement Mzize wa Yanga na Paul Peter wa Dodoma Jiji ambao wameonyesha uwezo mkubwa katika kufunga mabao hadi sasa katika ligi hiyo wakichuana na nyota wa kigeni. Mzize ana mabao 10 na asisti tatu, wakati Chikola ana mabao saba akiibeba Tabora inayoshika nafasi ya tano kwa sasa katika msimamo ikiwa na pointi 37 kupitia mechi 23, ilihali Paul Peter ameiwezesha Dodoma kuwa timu isiyotabirika akifunga mabao sita.

HAP 04

Kocha wa kikosi hiki ni Ahmad Ally anayeinoa JKT Tanzania, akiwa ni kocha aliyeifanya JKT kuwa moja timu zilizopo Sita Bora, lakini akiwa ni kocha mzawa aliyeiongoza kukusanya pointi 30 kupitia mechi 23, ikifunga mabao 18 na kufungwa 17 ikiwa ni moja ya timu yenye ukuta mgumu baada ya vigogo Simba, Yanga, Azam zilizopo Tatu Bora.


KIKOSI CHA WAZAWA

Yakoub Suleiman (JKT TZ), Shomari Kapombe (Simba), Mohammed Hussein (Simba), Ibrahim Bacca (Yanga), Dickson Job (Yanga), Yusuf Kagoma (Simba), Offen Chikola (Tabora Utd), Seleman Rashid ‘Bwenzi’ (KenGold), Clement Mzize (Yanga) Feisal Salum ‘Fei Toto’ (Azam) na Paul Peter (Dodoma Jiji)

AKIBA: Yona Amos (Pamba), Israel Mwenda (Yanga), Pascal Msindo (Azam), Abdulrazak Hamza (Simba), Adolf Mtasingwa (Azam), Oscar Paul (KMC), Nassor Saadun (Azam) na Joshua Ibrahim (KenGold)

KOCHA: Ahmad Ally


MZIKI WA WAGENI

Katika orodha ya kikosi cha nyota wa kigeni kuna mziki mnene kwani Mwanaspoti imefanya kazi ya ziada kuchuja wachezaji, kutokana na ukweli asilimia kubwa ya wageni wamefanya vizuri hadi sasa wakiwa na wastani wa kufunga mabao 3 kwa kila mechi moja ya Ligi, huku maeneo mengine wakitisha zaidi.

Ukiacha eneo la ushambuliaji lenye wanaume wa shoka wanaojua kutupia, lakini hata idara ya makipa na mabeki, wageni wamekimbiza mbali na eneo la kiungo ambao kuna mafundi wanaojua boli na kukifanya kikosi hicho kutisha zaidi na kama ikitokea kupimana ubavu na wazawa kazi itakuwapo.

Katika kikosi hicho cha mapro wa kigeni, langoni anasimama, Moussa Camara anayeongoza kwa kuruhusu mabao machache (manane), huku akiwa na clean sheet 15 ambazo ni sawa na zile zilizowekwa msimu uliopita na aliyekuwa kipa bora, Ley Matampi aliyekuwa Coastal Union. Camara ameweka clean sheet hizo kupitia mechi 20, akiwa amesaliwa na mechi nane zinazoweza kumuongeza idadi zaidi licha ya sasa kuelezwa ni majeruhi na kuzikosa mechi mbili zilizopita ikiwamo ya Coastal Union na ile ya jana dhidi ya Dodoma Jiji.

HAP 05

Mabeki wa pembeni wa timu hiyo wanasimama Andy Bikoko wa Tabora United aliyeifanya timu hiyo kuwa na ukuta imara, kwani ni timu ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu, lakini kwa iliyoruhusu mabao machache ikifungwa 19 katika mechi 23. Bikoko ana mawili na asisti moja hadi sasa na anasaidiana na Chadrack Boka wa Yanga ambaye amefunga bao moja na asisti mbili vilevile na amekuwa mmoja ya wachezaji wenye kasi na kutengeneza mashambulizi mbali na kujilinda vyema.

Mabeki wa kati wanasimama Anthony Tra Bi Tra wa Singida BS ambaye ameifanya timu hiyo kuwa imara ikiganda nafasi ya nne hadi sasa katika msimamo. Beki huyo kutoka Ivory Coast amefunga mabao mawili na kuasisti mawili, akiwa ni beki anayecheza kwa utulivu wa hali ya juu akitumia akili.

Urefu wake umekuwa msaada kwa timu katika kuokoa mipira ya juu, mbali na uwezo wa kutoa pasi na kutengeneza mashambulizi kwa haraka kwenda kwa adui, na beki huyo anasaidiana na Che Malone Fondoh wa Simba ambaye ametengeneza ukuta mgumu Msimbazi akishirikiana na mabeki wenzake.

Mcameroon huyo licha ya kutajwa kuwa majeruhi kwa sasa, lakini ni mmoja ya mabeki wa kati walioonyesha kiwango cha hali ya juu, kwa wepesi alionao katika kujilinda na kusaidia mashambulizi mbali na kufunga mabao kwani ana mawili hadi sasa.

Viungo wa timu hiyo ni Josephat Arthur Bada wa Singida BS, Pacome Zouzoua wa Yanga na Jean Charles Ahoua wa Simba ambao namba zao katika Ligi Kuu zinatisha kwa sasa wakati ligi ikienda mapumziko.

Bada amehusika katika mabao tisa akifunga matatu na kuasisti sita, wakati Pacome amehusika katika mabao 14 akifunga saba na asisti saba, wakati Ahoua (kabla ya mechi ya jana, alikuwa) amehusika katika mabao 16 akifunga 10 na kuasisti sita akiwa mchezaji wa pili kuhusika na mabao mengi nyuma ya Prince Dube wa Yanga aliyehusika na mabao 17, akiwa ndiye kinara kabla ya jana.

Washambuliaji katika kikosi hicho cha Mwanaspoti ni Dube, Jonathan Sowah wa Singida BS na Gibril Sillah wa Azam FC, ambao namba zao pia zinatisha katika ligi ya msimu huu. Dube aliyetua Yanga msimu huu kutoka Azam amekuwa nguzo imara ya Yanga katika ushambuliaji, akifunga mabao 10 bila ya penalti yoyote mbali na kuasisti saba, wakati Sowah aliyeingia dirisha dogo hadi sasa katika mechi saba amefunga mabao saba, ikiwa na maana kila mechi amefunga, akiwa ni mshambuliaji hatari zaidi ndani ya 18.

Sillah anayeshambulia kutoka pembeni naye ana balaa lake, kwani amefunga mabao saba na kuasisti mara mbili na kuifanya Azam kutamba ikiganda nafasi ya tatu hadi sasa.

Timu hii itakuwa chini ya kocha Fadlu Davids wa Simba ambaye amekuwa na rekodi nzuri akiwa na kikosi hicho kilichopo katika mbio za ubingwa ikichuana na watetezi, Yanga wanaosaka taji la msimu wa nne mfululizo. Kabla ya mechi ya jana, Fadlu aliiongoza Simba kucheza mechi 21 na kushinda 17, sare tatu na kupoteza moja tu, huku ikikusanya pointi 54 na kufunga mabao 46 na kufungwa manane.

Kama jana imeendeleza ubabe kwa Dodoma Jiji itakuwa na maana imecheza mechi 22 na kushinda 18 na kupunguza pengo la pointyi dhidi ya Yanga kutoka nne hadi moja, hapo ni mbali na kiporo cha Dabi, jambo linalomfanya awafunike makocha wengine wa kigeni waliopo kwa vile yeye alianza na timu tangu mwanzo wa msimu huu.


KIKOSI CHA WAGENI

Moussa Camara (Simba), Andy Bikoko (Tabora Utd), Chadrack Boka (Yanga), Anthony Tra Bi (Singida BS), Fondoh Che Malone (Simba), Josephat Arthur (Singida BS), Prince Dube (Yanga), Pacome Zouzoua (Yanga), Jonathan Sowah (Singida BS), Jean Charles Ahoua (Simba) na Gibril Sillah (Azam).


AKIBA: Diarra Djigui (Yanga), Ibrahim Imoro (Singida BS), Yeison Fuentes (Azam), Khalid Aucho (Yanga), Mathew Momanyi (Pamba), Elvis Rupia (Singida BS), Stephane Aziz Ki (Yanga), Peter Lwasa (Kagera Sugar)

KOCHA: Fadlu Davids


KIKOSI CHA JUMLA

Ukiacha vikosi hivyo vinavyoundwa na wachezaji wazawa na wageni, Mwanaspoti imekiunda kikosi bora cha Ligi Kuu hadi sasa chenye sura mseto kutoka kwenye vikosi hivyo viwili ambavyo vitakuwa chini ya kocha Fadlu.

Kikosi hicho kinaundwa na kipa Camara aliyewafunika makipa wote katika Ligi hadi sasa kwa uimara wake langoni akiwamo Kipa Bora wa Kombe la Shirikisho msimu uliopita na aliyekuwa Kipa Bora kwa misimu miwili mfululizo katika misimu mitatu, Diarra Djigui wa Yanga.

Ukuta wa kikosi hicho kwa asilimia kubwa unaundwa na wazawa ambao ni Kapombe na Tshabalala kwa pembeni, huku Job akisimama na Tra BI Tra, wakati eneo la viungo kuna mafundi Bada, Pacome na Ahoua, huku washambuliaji wakiwa ni Mzize, Dube na Sowah.


KIKOSI BORA KILIVYO

Moussa Camara (Simba), Shomary Kapombe(Simba), Mohammed Hussein (Simba), Antony Tra Bi (Singida BS), Dickson Job (Yanga), Josephat Arthur Bada (Singida BS), Clement Mzize (Yanga), Pacome Zouzoua (Yanga), Jonathan Sowah(Singida BS), Jean Charles Ahoua (Simba) na Prince Dube (Yanga).


AKIBA: Diarra Djigui (Yanga), Andy Bikoko (Singida BS), Ibrahim Bacca (Yanga), Khalid Aucho (Yanga), Yusuf Kagoma (Simba), Feisal Salum (Azam), Elvis Rupia (Singida BS), Stephane Aziz KI (Yanga).

KOCHA: Fadlu Davids