Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ligi Kuu England inavyorudi na utamu wake

EPL Pict

Muktasari:

  • Kipute hicho kitapigwa kesho Jumatano huku namba zikionyesha kwamba hiyo itakuwa mechi yao ya 66 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mara 65 ilizokutana, Arsenal ilishinda 26, mara 18 nyumbani na nane ugenini, wakati Spurs imeshinda 15, mara 13 nyumbani na mbili ugenini huku mechi 24 ziliisha kwa sare. Safari hii itakuwaje? Ni suala la kusubiri kipigwe hiyo kesho.

LONDON, ENGLAND: MCHAKAMCHAKA wa Ligi Kuu England utaendelea tena wiki hii, ambapo macho na masikio ya wengi yatakuwa huko kwenye kipute cha dabi ya London Kaskazini, wakati ambapo Arsenal itakuwa nyumbani Emirates kukabiliana na mahasimu wakuu, Tottenham Hotspur.

Kipute hicho kitapigwa kesho Jumatano huku namba zikionyesha kwamba hiyo itakuwa mechi yao ya 66 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mara 65 ilizokutana, Arsenal ilishinda 26, mara 18 nyumbani na nane ugenini, wakati Spurs imeshinda 15, mara 13 nyumbani na mbili ugenini huku mechi 24 ziliisha kwa sare. Safari hii itakuwaje? Ni suala la kusubiri kipigwe hiyo kesho.

Hata hivyo, kwa siku hiyo ya kesho, kutakuwa na mechi za kibabe sana ambapo Everton ikiwa na kocha wake mpya, David Moyes itakuwa nyumbani Goodison Park kucheza na Aston Villa ya mkali wa Kihispaniola, Unai Emery. Makocha hao wawili wanafahamiana vyema baada ya kukutana mara nyingi, huku Leicester City itakuwa nyumbani King Power kukabiliana na Crystal Palace.

Newcastle United itakuwa nyumbani St James’ Park kucheza na Wolves katika moja ya mechi zinazotazamiwa kuwa na upinzani mkali, huku macho ya wengi yataelekezwa kwa straika Alexander Isak kama atafunga tena kama ambavyo amekuwa tishio kwa sasa na kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu England.

Usiku wa leo Jumanne, mashabiki wa ligi hiyo watakutana na uhondo matata kabisa, ambapo Manchester City itakuwa ugenini kukipiga na Brentford kwenye Uwanja wa Gtech Community. Hiyo itakuwa mechi ya nane kwa miamba hiyo kumenyana kwenye Ligi Kuu England, ambapo mara saba zilizopita, Man City imeshinda tano, mara tatu ilipocheza nyumbani na mbili ugenini, huku Brentford imeshinda mbili, moja nyumbani na nyingine ugenini. Kinachovutia timu hizo hazijawahi kutoka sare kwenye mechi za Ligi Kuu England.

Lakini, balaa zaidi kwa usiku wa leo litakuwa huko The City Ground wakati Nottingham Forest ikiwa kwenye ubora wa kutosha itaikaribisha Liverpool, ambayo pia imekuwa moto msimu huu. Itakuwaje? Ni suala la kungoja.

Takwimu zinasoma kwamba mara 15 ambazo miamba hiyo imekutana kwenye Ligi Kuu England, sare ni nne, huku Liverpool ikishinda saba, mara sita nyumbani na moja ugenini, huku Forest ikishinda nne, tatu ilipocheza nyumbani na moja ugenini. Kazi ipo.

West Ham United yenyewe itakuwa nyumbani kucheza na Fulham, ambayo imekuwa moto sana msimu huu, huku Chelsea itajimwaga uwanjani Stamford Bridge kucheza na Bournemouth katika mechi nyingine inayotazamiwa kuwa na utamu wa kutosha ndani ya uwanja.

Mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England itaendelea hadi keshokutwa Alhamisi, ambapo Ipswich Town itakipiga na Brighton, kabla ya Manchester United kupepetana na Southampton.

Mashabiki wa ligi hiyo wanasubiri kwa hamu kuona namna msimamo utakavyobadilika kutokana na mechi za wiki hii, hasa pale kwenye kilele cha msimamo huo kama kutakuwa na uongezo la pengo la pointi au kama litapungua.

Hata hivyo, wakati ukisubiri hilo, ushawahi kujiuliza kwenye msimamo wa muda wote wa Ligi Kuu England ni timu gani inashika usukani na ipi inaburuza mkia? Kwenye msimamo wa muda wote wa Ligi Kuu England, Luton Town ndiyo timu inayoburuza mkia ambapo ilivuna pointi 26 katika mechi 38.

ManUnited ndiyo vinara wa msimamo wa muda wote. Lakini, unafahamu imecheza mechi ngapi na kuvuna pointi ngapi?

Kutokana na hilo, Mwanaspoti linakuletea msimamo wa muda wote wa Ligi Kuu England unaohusu timu za Big Six tu unavyosoma ili kufahamu mbabe ni nani na kibonde ni yupi. Kula chuma hicho!

EP 01

Man United – mechi 1248, pointi 2524, mabao 2323

Man United imekuwa ikisuasua kwenye Ligi Kuu England msimu huu, ikishuka nafasi kwenye 10 la chini katika msimamo, hivyo wanapambana kuweka mambo sawa. Lakini, kwenye ishu ya msimamo wa muda wote wa Ligi Kuu England, miamba hiyo ya Old Trafford inashika namba moja, ikivuna pointi 2,524 katika mechi 1,248 ilizocheza. Katika mechi hizo, Man United imeshinda 750, sare 274 na vichapo 224 huku ikifunga mabao 2323 na kufungwa mabao 1195, hivyo imebaki na +1128 ya tofauuti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

EP 02

Arsenal – mechi 1248, pointi 2354, mabao 2235

Chama la Arsenal kwa sasa lipo chini ya kocha Mikel Arteta, ambaye kwa misimu miwili ya hivi karibuni aliifanya timu hiyo kuwa tishio na kuwa ya kiushindani kwenye mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England. Kwa misimu miwili iliyopita, Arsenal imemaliza kwenye nafasi ya pili na hata sasa ipo kwenye nafasi ya pili, pointi sita nyuma ya vinara Liverpool.

Lakini, Arsenal inaonekana kuwa na mapenzi na nafasi ya pili, kwani hata kwenye msimamo wa muda wote wa Ligi Kuu England, miamba hiyo imecheza mechi 1248 na kuvuna pointi 2354.

Kwenye mechi hizo, imeshinda 684, imetoka sare 302 na vichapo 262, huku ikifunga mabao 2235 na kufungwa 1238 na kuwa na +997 ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.


Liverpool – mechi 1247, pointi 2304, mabao 2229

Mdachi Arne Slot ameonekana kuanza na mguu mzuri kwenye maisha yake huko Liverpool baada ya kuiongoza vyema timu hiyo ya Anfield na kuongoza msimamo wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi sita licha ya kucheza mechi moja pungufu.

Hayo ni makali ya Liverpool kwa msimu huu, ambayo imekusanya pointi 46 katika mechi 19.

Lakini, kwenye msimamo wa muda wote wa Ligi Kuu England, Liverpool kwenye ile orodha ya Big Six inashika nafasi ya tatu, baada ya kucheza mechi 1247 na kukusanya pointi 2304.

Katika mechi hizo, Liverpool imeshinda 666, sare 306 na vipigo 275, huku ikifunga mabao 2229 na kufungwa 1254 na kuwa na +975 ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

EP 03

Chelsea – mechi 1248, pointi 2281, mabao 2127

Enzo Maresca alianza kwa moto kwenye benchi la ufundi katika kikosi cha Chelsea na kuifanya timu hiyo kuwa tishio msimu huu na kuonekana kama ipo kwenye mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England kabla ya mambo kutibuka kwa siku za hivi karibuni.

Chelsea imeporomoka kwa kasi kutoka nafasi ya pili hadi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu, lakini pia ikishika nafasi ya nne kwenye msimamo wa muda wote wa mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England baada ya kuvuna pointi 2281 katika mechi 1248 ilizocheza.

Katika mechi hizo, The Blues imeshinda 657, imetoka sare 310 na kuchapwa 281 huku ikifunga mabao 2127 na kufungwa 1259, hivyo ikibaki na +868 ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na kuifanya Chelsea kukamilisha ile Top Four ya muda wote kwenye Ligi Kuu England, kwamba kama ingekuwa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, basi msimamo ungekuwa hivyo.


Tottenham – mechi 1248, pointi 1937, mabao 1930

Tottenham Hotspur ukiitafuta kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa msimu huu, inashika nafasi ya 12 baada ya kukusanya pointi 24 katika mechi 20.

Si rekodi tamu sana na ndio maana hata kocha wao alikuwa kwenye kitimoto, akidaiwa kuwa kwenye hatari ya kufutwa kazi. Lakini, kwenye msimamo wa muda wote wa Ligi Kuu England, kwa vigogo wa Big Six, Spurs inashika nafasi ya tano, ipo juu ya Man City baada ya kuvuna pointi 1937 katika mechi 1248.

Katika mechi hizo, Spurs imeshuhudia ushindi mara 547, ikitoka sare 296 na kupoteza mechi 405 huku ikiwa imefunga mabao 1930 na kufungwa 1592, huku ikiwa na +338 ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na hivyo kujiweka kwenye orodha ya timu ambazo zimefanya vizuri kwenye msimamo wa muda wote wa Ligi Kuu England.


Man City – mechi 1058, pointi 1843, mabao 1884

Habari ndiyo hiyo, usishangae. Man City imekuwa tishio kwa misimu ya hivi karibuni kwenye Ligi Kuu England tangu ilipokuwa chini ya kocha Pep Guardiola, lakini mavitu ya timu hiyo ya huko nyuma kwenye ligi hiyo, mambo hayakuwa poa kabisa na ndiyo maana kwenye msimamo wa muda wote wa Ligi Kuu England kwa upande wa vigogo wa Big Six, Man City ndiyo inayoshika mkia baada ya kukusanya pointi 1843 katika mechi 1058.

Na hilo linatokana na timu hiyo kuwahi kushuka daraja. Katika mechi hizo, Man City imeshinda 539, sare 226 na vichapo 293, huku ikifunga mabao 1884 na kufungwa 1162 na kuwa na +722 ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Kwa msimu huu, Man City mambo yake pia si mazuri, ikishika nafasi ya sita kwenye msimamo baada ya kuvuna pointi 34 katika mechi 20.

Kocha Guardiola anakuna kichwa kuona namna gani atapindua meza na kutetea taji la ubingwa wa ligi hiyo, ambalo amelibeba mara nne mfululizo.