KWAKO KASHAHA: Simba, Namungo wameipa heshima Tanzania

HATUA ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika inaendelea na sasa raundi mbili zimeshachezwa na upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, hatua ya mchujo imekamilika rasmi na sasa inangoja hatua ya makundi.

Upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, wawakilishi wa Tanzania, Simba, Jumanne iliyopita walicheza dhidi ya Al Ahly na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Luis Miquissone.

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, wawakilishi wengine wa Tanzania, Namungo FC wamefanikiwa kutinga pia hatua ya makundi baada ya kuitupa nje Primiero De Agosto ya Angola walipoibuka na ushindi wa jumla wa mabao 7-5 licha ya kupoteza 3-1 katika mechi ya marudiano iliyochewa kwenye Uwanja wa Azam Complex, juzi Alhamisi.

Kwa ujumla kwanza tumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba timu zetu mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika zimefanya vizuri, lakini pia zimecheza katika ari ya juu ya ushindani, kitu ambacho kimechangia zipate matokeo chanya hapa nyumbani.

Ukiondoa changamoto zilizowakuta Namungo, lakini haikuwakatisha tamaa na haikuwavunja moyo. Nadhani walijipanga vizuri kisaikolojia na viongozi wao hatimaye wakaja kucheza michezo yote nyumbani na wamefanikiwa.

Pamoja na kwamba wamepoteza mechi ya marudiano, lakini nafikiri kazi nzuri ilikuwa ni katika mchezo wa kwanza imewafanya wavuke. Kwa hiyo naweza kusema timu zote za Tanzania ziko kwenye kiwango kizuri, sehemu nzuri na zimefanya kazi nzuri ya kulinda heshima yao, mashabiki wao na nchi kwa ujumla wake.

Nianze kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ulichezwa kati ya Simba na Al Ahly. Kwa ujumla naweza kusema ilikuwa ni mechi moja nzuri. Binafsi yangu mimi sijashuhudia kiwango cha Simba, takribani miaka saba au nane hivi kulinganisha na mpira waliocheza juzi dhidi ya Al Ahly.

Walicheza mpira ambao naweza kusema technically ulikuwa umebalansi katika maeneo yote. Utayari ulikuwa wa kutosha. Uwezo wa mchezaji mmojammoja ulikuwa juu, commitment level kwa kila mchezaji ilikuwa ni ya juu mno lakini discipline ya mchezo kwa maana ya mbinu za kiufundi ilikuwa ya kutosha sana na ndio maana mtu ambaye kwa kufuata profile au kwenye makaratasi usingeweza kujua kwamba wale ni Al Ahly licha ya ukubwa wao kwenye parameters (vigezo) mbalimbali kwenye soka la Afrika

Kwa mtazamo wa haraka labda ungefikiria Simba ingekuwa ni underdog mbele ya Al Ahly ukizingatia wametoka kucheza Kombe la Dunia la Klabu wakiwa wameshika nafasi ya tatu, ni mabingwa watetezi wakiwa na kikosi bora, wameboresha benchi la ufundi lakini pia ni timu ambayo ina wachezaji waliosajiliwa kwa thamani ya juu.

Sasa on paper unaweza kufikiri kwamba Al Ahly walikuwa na zaidi ya asilimia 70 kushinda, lakini kilichotokea uwanjani kilikuwa kinyume kuonyesha kuwa Simba walijiandaa vizuri na mentally na physically walikuwa tayari kucheza na mabingwa wa Afrika.

Mchezo uwanjani kuanzia dakika ya kwanza hadi ya 90 vipindi vyote viwili, kulikuwa na concentration (umakini) ya juu mno, wachezaji walikuwa maximum concentrated (makini zaidi) kwa sababu kulikuwa na makosa ambayo yalikuwa yanajitokeza lakini walikuwa wepesi kuyasahihisha haraka iwezekanavyo

Lakini pili, mfumo wa mwalimu ulionekana kuwabeba mno kwani aliweka holding midfielders wawili ambao waliwasaidia sana Chama na Miquissone waliokuwa mbele na wakawasaidia sana Pascal Wawa na Joash Onyango kucheza wakiwa huru mno licha ya kwamba backline ya Simba ilitimiza majukumu yake inavyotakiwa kwa hiyo kila mmoja alitimiza wajibu wake vizuri kwa maana ya shared values kwenye mpira lakini pia tunasema complimentary skills (ujuzi wa kuongezea) kwamba pale inapooneka mmoja amekosea mwingine anaingia kwa haraka kufuta makosa yake lakini waliambukizana uwezo wa kiufundi na kimbinu na isingeweza kuonekana mchezaji gani yuko dhaifu kwa hiyo kulikuwa na flow ya mpira ulioonekana kutembea.

Lakini pia tumpongeze key player (mchezaji bora) wa Simba aliyecheza katika nafasi ya ushambuliaji kwa sababu alikuwa ana uwezo wa kukaa na mipira lakini kubwa lingine nililoliona, Simba walikuwa na variation (tofauti)katika kushambulia. Walikuwa wanekwenda deep kwenye penati boksi lakini safari hii wlaikuwa wanapiga mashuti mengi nje ya boksi. Na lile goli lililofungwa, lilikuwa ni amost nje ya penalti boksi maana ilikuwa kwenye ile mark ya penati boksi.

Mechi ya marudiano ya Namungo ilikuwa ni nzuri yenye hadhi ya kimataifa ingawa ilitawaliwa zaidi na De Agosto ambayo ni timu kubwa na yenye wachezaji wazuri.

Kimsingi nazipongeza Simba na Namungo kwa kufanya vziuri na naamini hii itasaidia kuinua mpira wetu.