Kwa Yanga hii unapigwa nje na ndani

Kwa Yanga hii unapigwa nje na ndani

USAJILI wa vifaa vitano vipya vya kigeni, Joyce Lomalisa, Aziz Ki Stephane, Bernard Morrison, Lazarous Kambole na Gael Bigirimana unaipa Yanga vikosi viwili vya kibabe ambavyo vinaweza kuifanya ishiriki vyema mashindano ya kimataifa na yale ya ndani bila presha.

Lakini kana kwamba haitoshi, benchi la ufundi la Yanga lina wigo mpana wa uteuzi wa mfumo wowote na staili ya kiuchezaji katika michezo mbalimbali kutokana na uwepo wa kundi kubwa la wachezaji ambao wana sifa tofauti za kiuchezaji na kiufundi.


Mifumo mitano ya kibabe

Msimu uliopita, Yanga ilikuwa ikipendelea sana kutumia mfumo wa 4-2-3-1 na mara kadhaa ilibadilika na kutumia ule wa 4-4-2 lakini usajili ambao wameufanya hivi sasa imewaongezea wachezaji ambao wanaweza kuwafanya wategemee pia mifumo ya 4-3-3 na 3-5-2 ama 3-4-3.

Eneo la kiungo ndilo ambalo Yanga inaonekana kuwa na utajiri mkubwa wa wachezaji jambo ambalo kiuhalisia litaliumiza kichwa benchi la ufundi la timu hiyo katika kuamua nani apewe nafasi ya kucheza kikosini baina yao.

Katika eneo la kiungo, Yanga ina Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Aziz Ki, Khalid Aucho, Yannick Bangala, Zawadi Mauya, Farid Musa na Gael Bigirimana.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi akiamua kuanza na viungo wawili wa ulinzi ambao watajikita na ulinzi tu, anaweza kuanza na Bangala, Aucho, Mauya au Bigirimana lakini kama anataka kuanza na kundi kubwa la viungo washambuliaji anaweza kuwatumia Farid, Sure Boy, Fei Toto na Aziz KI.

Upande wa washambuliaji pia, Nabi ana Fiston Mayele, Heritier Makambo, Kambole, Yusuf Athuman na Crispin Ngushi ambao yeyote kati ya hao anaweza kumudu mfumo wowote ule ikiwa Yanga itaamua kuanza na washambuliaji wawili wa kati, mmoja au watatu au kuhitaji wengine washambulie kutokea pembeni.


Vita ya ushindani

Kusajiliwa kwa Lomalisa kunamuweka katika wakati mgumu Kibwana Shomari kupata nafasi ya kutosha mbele yake upande wa beki wa kushoto ambayo amekuwa akipangwa katika idadi kubwa ya mechi msimu huu.

Uzoefu wa Lomalisa aliyewahi kuichezea timu ya Taifa ya DR Congo na uwezo wake wa kuzuia pamoja na kusaidia mashambulizi, vinaweza kumpa changamoto Kibwana ambaye amekuwa bora zaidi katika kuzuia.

Mawinga Bernard Morrison na Aziz Ki, huenda wakachukua nafasi za Ducapel Moloko na Dickson Ambundo ikiwa wawili hao watashindwa kukaza buti kwani wana wana uzoefu wa mechi hasa za kimataifa lakini pia wana uwezo mkubwa wa kuamua mechi kutokana na uwezo wao binafsi wa kupiga chenga, kutengeneza nafasi na kufunga mabao.

Kambole anatishia nafasi ya Feisal Salum iwapo Yanga itaanzisha washambuliaji wawili wa kati kwa pamoja.


Vikosi

Kikosi cha wachezaji 11 ambacho Yanga inakifikiria kwa mechi za kimataifa kitaundwa na kipa Djigui Diarra huku mabeki wakiwa ni Djuma Shabani, Joyce Lomalisa, Dickson Job na Bakari Mwamnyeto.

Kwenye nafasi ya kiungo kutakuwa na Bangala na Bigirimana huku mawinga wakiwa ni Ki Aziz na Feisal Salum

Upande wa ushambuliaji, Yanga inaweza kuwachezesha pamoja Kambole na Mayele jambo linaloweza kuifanya ipate idadi kubwa ya mabao tofauti na sasa ambapo mzigo mzito unaonekana kuwa kwa Mayele.

Nyota hao 11 watakaokuwa wanaanza, watakuwa na usaidizi wa wengine 11 ambao nao wanaweza kutengeneza kikosi chao kikawa tishio pia.

Wakali hao ni kipa Abuutwalib Msheri, mabeki Farid Musa, Kibwana Shomari, Ibrahim Bacca na Abdallah Shaibu, huku viungo wakiwa ni Zawadi Mauya na Salum Abubakar.

Mawinga ni Bernard Morrison na Dickson Ambundo wakati washambuliaji ni Heritier Makambo na Ngushi.