Kutoka Manara hadi Samatta

Muktasari:

WAKATI taifa likijiandaa kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru Desemba 9, Watanzania wameshuhudia mambo mengi yaliyojitokeza, hususan wazawa wanavyopambana kucheza nje ya nchi.

WAKATI taifa likijiandaa kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru Desemba 9, Watanzania wameshuhudia mambo mengi yaliyojitokeza, hususan wazawa wanavyopambana kucheza nje ya nchi.

Wimbi la Watanzania kwenda kucheza nje ya nchi halipo kwenye soka tu hasa la wanaume kama wengi wanavyofikiria, lipo hata kwenye mpira wa kikapu, utabisha nini wakati kina Abdallah Ramadhan ‘Dullah’ na Hasheem Thabeet, Upande wa mabondia kuna Omary Kimweri, wanasoka wa kike kama Sophia Mwasikili, Eshter Chabruma ‘Lunyamila’ na sasa Mwanahamis Omary ‘Gaucho’ anayekipiga Morocco.

Hata kwenye upande wa makocha Tanzania imeshuhudia ndani ya Miaka 60 ya Uhuru, baadhi yao wakienda nje na kuleta heshima kubwa kwa taifa. Danny Korosso, kocha anayekumbukwa kwa soka la kitabu lililochezwa na Ushirika Moshi ni mmoja wa makocha awali kabisa kwenda nje ya nchi, alienda Botswana.

Sunday Kayuni anaheshima kubwa ndani ya Kenya hususani klabu ya AFC Leopards kutokana na kuibebesha taji la mwisho la Ligi Kuu ya Kenya, miaka ya mwisho ya 1990 na baada ya hapo wanahangaika kusaka ubingwa bila mafanikio. Pia kuna Twalib Hilal, Seleman Nyambui, Mohammed Badru na wengine walioenda kufundisha nje ya nchi kupitia soka na riadha.

Ukiachana na michezo, hata kwenye burudani nako kuna wasanii mbalimbali wa Kitanzania waliotumia vipaji vyao kwenda nje ya nchi na baadhi yao hadi leo wanaendeleza kuitangaza nchi kimataifa.

Freshi Jumbe Mkuu na wenzake hadi leo wapo Japan. Pia kuna mtunzi na mwimbaji mahiri nchini aliyepita katika bendi mbalimbali ikiwamo DDC Mlimani Park ‘Wana Sikinde’, Amina Ngaluma ‘Japaness’, ambaye yeye na mumewe Rashid Sumuni walifanya kazi wakiwa na bendi ya Jambo Survivors nchini Thailand, Mashariki ya Mbali barani Asia.

Japaness alikumbwa na mauti akiwa nchini humo Mei 2014 na kuja kuzikwa nchini. Mpiga solo mahiri wa zamani wa Vijana Jazz, Shaaban Yohana ‘Wanted’ aliyekuwa Botswana kabla ya kukumbwa na mauti mwaka 2017 na wengineo ni kuonyesha namna gani kwenda nje ya nchi kusaka maisha kwa kutumia vipaji haikuwa kwenye soka au michezo mingine tu.

Hata hivyo, katika kusherehekea Miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania Bara) tunaangalia namna safari ya nyota wa Tanzania katika kucheza soka nje ya nchi na namna upepo ulivyo sasa na sauti za wadau juu ya kitu gani kinachokwamisha baadhi yao kushindwa kuchangamka kama walivyofunguliwa njia na nyota wa zamani wa kimataifa wa Yanga, Pan Africans na Taifa Stars, Kitwana Manara na nduguze Sunday Manara ‘Computer’ na Kassim Manara.


Kitwana Manara ‘Popat’

Kama hamjui, Kibwana Manara ndiye aliyekuwa Mtanzania wa kwanza kucheza soka la kulipwa, akisajiliwa miaka ya 1960 klabu ya Feisal FC ya Mombasa baada ya kung’ara timu ya taifa ya Tanganyika, akiwa kama kipa.

Kitwana anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyedumu timu ya taifa ya Tanzania kwa muda mrefu, akiichezea kwa miaka 16 kutoka 1960-1976, lakini akichezea timu mbili tofauti katika nafasi mbili tofauti.

Alisajiliwa Cosmopolitan kama kipa na baadaye TPC Moshi na kuichezea Stars kabla ya kwenda Mombasa na aliporejea nchini na kusajiliwa Yanga mwaka 1965 alikuwa namba 9 tishio, lakini katika timu ya taifa ndiye aliyekuwa kipa namba moja, yaani ‘Tanzania One’ enzi hizo.

Jamaa alisifika kwa kufunga mabao ya kichwa enzi akicheza kama mshambuliaji, huku kwenye ukipa alisifika kwa kudaka kutokana na kuwa na umbile kubwa na uwezo mkubwa wa kuruka juu.

Inaelezwa ndiye mshambuliaji aliyetajwa kuwa na mabao mengi nchini (ingawa idadi yake haitajwi) ikielezwa amemzidi Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyekuwa Yanga aliyemaliza msimu mmoja na mabao 26 mwaka 1999 na kufuatiwa na Abdallah Juma aliyekuwa Mtibwa Sugar aliyefunga 25 mwaka 2004.

Inaelezwa aliwahi kutakiwa kucheza soka Ulaya, lakini alichomoa na kufungua milango kwa wadogo zake, Sunday Manara ‘Cumputer’ na Kassim Manara waliocheza barani humo katika nchi za Uholanzi na Austria.


Sunday Manara ‘Computer’

Sunday Manara, baba mzazi wa Msemaji wa zamani wa Simba aliyehamia Yanga kwa sasa, Haji Manara ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza kabisa nchini kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya baada ya kupatikana kwa Uhuru unaotimiza miaka 60 kwa sasa.

Umahiri wake enzi akikipiga kilimfanya abatizwe jina la Computer, hata kabla chombo hicho kilichorahisisha teknolojia ya mawasiliano hakijatua nchini kwa kiwango kikubwa alichokuwa nacho akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji.

Mara baada ya kung’ara na Yanga na baadaye kupita Pan Africans, alitimka nje ya nchi na kwenda Uholanzi kujiunga na Heracles Almelo ya Uholanzi mwaka 1977 hadi 1978.

Baada ya Manara kucheza Ulaya jkwa kujiunga moja kwa moja, ilipita muda mrefu kabla ya Renatus Njohole, Haruna Moshi ‘Boban’, Henry Joseph na wengine kadhaa kuibuka, lakini bado mkongwe huyo anashikilia rekodi yake, japo Mbwana Samatta aliandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kwa sasa kucheza Ligi Kuu England.

Mwaka 1979, Manara alitimkia New York Eagles ya Marekani alilokuwa akicheza ligi moja na gwiji wa soka duniani Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’ ambaye alikuwa akiichezea timu ya New York Cosmos.

Alidumu ndani ya timu hiyo kwa mwaka mmoja na kuamua kundoka na kujiunga na klabu yaSV St. Veit ya Austria na baadae kutua katika timu ya Al-Nasr ya Dubai na mwaka 1984 alipoamua kurejea nyumbani Tanzania baada ya kustaafu.


Nadir Haroub ‘Canavaro’

Beki huyu ambaye alijiunga na Yanga mwaka 2006 akitokea Malindi FC ya Zanzibar, aliwahi kuonja ladha ya soka la kulipwa baada ya mwaka 2009, Yanga kumtoa kwa mkopo Vancouver Whitecaps ya Canada iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Marekani.

Nahodha huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars aliichezea Vancouver Whitecaps kwa miezi sita na mwaka 2010 akarejea nchini kuendelea kuichezea Yanga.


Athuman Machupa

Mmoja ya washambuliaji hatari waliowahi kuichezea Simba na timu ya Taifa ya Tanzania’ Taifa Stars’.

Simba ilimsajili Machuppa mwaka 1998 akitokea Malindi ya Zanzibar na kuichezea klabu hiyo kwa misimu nane mpaka pale alipoamua kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Denmark mwaka 2007.

Alicheza Denmark kwa msimu mmoja na baadae akaenda kucheza soka la kulipwa Sweden hadi anastaafu.

Alipostaafu hakurudi Tanzania na kuamua kundelea kuishi nchini humo na kisha kumchukua na mkewe na mpaka leo wanaishi nchini huko.

Shekhan Rashid ni kiungo wa zamani wa Simba aliyesajiliwa na klabu hiyo mwaka 2001 na kuichezea kwa misimu mitatu hadi 2004 alipoamua kwenda Uarabuni kucheza soka la kulipwa, kisha mwaka 2005 akarejea nchini na kujiunga na Mtibwa Sugar kisha Moro United kabla ya kupumzika kwa muda soka mwaka 2007 baada ya kupata majeraha ya kifundo cha mguu.

Mwaka 2009 akajiunga na Azam aliyoichezea kwa msimu mmoja na kupumzika baada ya kutofurahia soka kutokana na jeraha la kifundo cha mguu na ndipo mwaka 2011 akafanya uamuzi wa kutimkia Sweden kucheza soka la kulipwa na anaishi huko hadi leo.

Nahodha zamani wa Taifa Stars, Henry Joseph naye aliwahi kucheza soka la kulipwa nje ya nchi katika klabu ya Kongsvinger ya Norway kuanzia mwaka 2009 hadi 2013.

Nizar Khalfan naye alikuwa mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar na Yanga na aliwahi kucheza soka la kulipwa katika klabu mbalimbali.

Mwaka 2007 alijiunga na Al Tadamon ya Kuwait na mwaka uliofuata akasajiliwa Tadamon Sour ya Lebanon na baadae mwaka 2009 akarejea nchini na kujiunga na Moro United.

Alichezea Moro United nusu msimu na mwaka huo 2009 akasajiliwa na Vancouver Whitecaps ya Canada aliyoichezea hadi mwaka 2011.


Danny Mrwanda

Mshambuliaji huyu wa zamani wa AFC Arusha, Simba, Yanga na Taifa Stars, ni miongoni mwa nyota waliotimka nje ya nchi na kucheza kwa muda mrefu, akianzia kucheza in Kuwait katika klabu ya Al Tadamon kisha akatimkia Vietnam kukipiga Đong Tâm Long An na Ða Nong kabla ya kurejea nyumbani kucheza na mara ya mwisho.


Mbwana Samatta

Ni mmoja ya wachezaji walioinufaisha sana Simba kwani nusu msimu aliocheza Simba kuanzia mwaka 2010 hadi 2011 ulimtosha Samatta kuuthibitishia ulimwengu ana kipaji kikubwa cha kusakata soka na kupata dili nono la kujiunga na TP Mazembe ya DR Congo.

Mazembe walilazimika kuilipa Simba kiasi cha Dola 82,681.90 sawa zaidi ya Sh191 milioni ili kupata saini yake na mwaka 2015 aliwapa ubingwa wa Afrika. Baada ya hapo gari la Samatta liliwaka, akatimkia KRC Genk ya Ubelgiji mwaka 2016 alikoichezea hadi mwaka jana na kisha kusajiliwa na Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu England.

Hata hivyo, mwaka jana klabu hiyo ya Aston Villa ilimtoa kwa mkopo Fenerbahce ya Uturuki ambayo nayo imemtoa kwa mkopo Antwerp ya Ubelgiji.


Mrisho Ngassa

Winga huyu machachari wa zamani wa Yanga mwenye rekodi ya kuwa mchezaji aliyeifungia mabao mengi timu ya taifa ya Tanzania (25), mwaka 2015 alipata dili la mkwanja mrefu kwenda Free State Stars ya Afrika Kusini.

Wakati huo Ngassa alikuwa Yanga na kununuliwa na wasauzi hao kwa kitita cha Dola 155,907.4 sawa zaidi ya Sh361 milioni.

Aliichezea Free State kwa msimu mmoja na kisha mwaka 2016 akatimkia Fanja FC ya Oman kabla ya mwaka 2017 kurejea nchini.


Simon Msuva

Difaa El Jadida ya Morocco ilitoa kiasi cha Dola 80,325 zaidi ya Sh186 milioni kwa Yanga ili kunasa saini ya winga Simon Msuva mwaka 2017.

Akiwa Jadida Msuva aliuwasha moto kinoma na kuwashawishi vigogo wa nchi hiyo Wydad Athletic Club mwaka jana kumsaini kwa pesa ndefu na hadi sasa anawatumikia mabingwa hao wa Morocco.


Thomas Ulimwengu

Hii ni awamu ya pili kwa Thomas Ulimwengu kuichezea miamba ya soka la Afrika na DR Congo, TP Mazembe, mara yake ya kwanza alikuwa na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta.

Mwaka 2011 ndipo Ulimwengu alipopata nafasi ya kujiunga na TP Mazembe na kuichezea klabu hiyo kwa miaka mitano kisha aliamua kutimkia zake, Sweden alikojiunga na AFC Eskilstun lakini majeraha yalikatisha ndoto yake ya kucheza soka barani Ulaya.

Ilimbidi kukaa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu na baada ya kupona akatajwa kujiunga na Sloboda Tuzla lakini taratibu za kufanya kazi nchini humo zilikuwa kikwazo kwake hivyo ikambidi arejee Afrika na kuamua kuzichezea Al-Hilal Club ya Sudan na JS Saoura ya Algeria kabla ya kurejea zake DR Congo.


Ally Msengi

Ni Mtanzania pekee ambaye kwa sasa anacheza Ligi Kuu Afrika Kusini akiwa na Stellenbosch. Msengi,19, alipata nafasi hiyo mwaka jana, 2020 baada ya kufanya majaribio kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo ambacho kilikuwa kikijiandaa na msimu mpya.

Licha ya udogo wake, Msengi amekuwa ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa wakipata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayonolewa na Steve Barker na mara kadhaa kocha huyo amekuwa akimsifia kiungo huyo wa Kitanzania.


Novatus Dismas

Alhamisi ya Septemba 2, 2021 kwenye uwanja wa TP Mazembe, Lubumbashi ndipo alipopewa nafasi ya kuvaa kwa mara ya kwanza jezi ya Taifa Stars na kufanya yake mbele ya tajiri, Moise Katumbi huko DR Congo na mashabiki hawakuwa sehemu ya mchezo huo ambao ulikuwa wa kuwania nafasi ya Kombe la Dunia Qatar 2022.

Licha ya kwamba ulikuwa ni mchezo wake wa kwanza kuitumikia Taifa Stars, Novatus Dismas, 19, alimudu kushindana na viungo wa kimataifa wa DR Congo kama vile Samuel Moutoussamy anayekipiga Nantes ya Ligi Kuu Ufaransa ‘Ligue 1’ na Chancel Mbemba anayeichezea FC Porto ya Ureno.

Novatus alicheza kwa dakika 57 kabla ya nafasi yake kuingia Mudathir Yahya. Kile alichokifanya kwenye mchezo wake wa kwanza ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, kilimfanya Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen kumpa shavu kwenye mchezo wa pili wa kuwania nafasi ya kwenda Qatar, ilikuwa ni mchezo dhidi ya Madagascar kwa Mkapa.

Kiungo huyo mkabaji wa Maccabi Tel Aviv ya Israel, aliitumia vyema nafasi hiyo kwa kuisaidia Taifa Stars kuvuna pointi tatu kwa kuibuka na ushindi wa maba 3-2, alikuwa miongoni mwa wafungaji wa mabao ya Tanzania kwenye mchezo huo uliochezwa bila ya uwepo wa mashabiki ikiwa ni matakwa ya Shirikisho la Soka Afrika.

Baada ya Entag El Harby kushuka daraja huko Misri, Himid Mao ‘Ninja’ ni kama amebadili gia akiwa angani kwa kubaki Ligi Kuu nchini humo baada ya kukamilika kwa uhamisho wake wa kujiunga na Ghazl El Mahalla siku chache zilizopita kwa makataba wa miaka mitatu.

Ghazl El Mahalla itakuwa klabu ya nne kwa Himid kuichezea huko Misri na alianza maisha yake ya soka la kulipwa 2018 kwa kukipiga akiwa na Petrojet ambayo aliichezea kwa msimu mmoja na iliposhuka daraja akatimka zake.

Baada ya kuondoka Petrojet, Himid alijiunga na Enppi SC kama ambavyo ilikuwa pindi akiichezea timu yake ya kwanza mambo yalivyoenda kombo kutokana na kiwango kizuri alichokuwa akikionyesha akiwa na klabu hiyo wala hakushuka daraja. Wakati Enppi SC ikishuka daraja, kiungo huyo wa zamani wa Azam FC, alipata shavu la kujiunga na Entag El Harby ambayo miongoni mwa timu saba ambazo zimeshinda ubingwa wa Ligi Kuu ya Misri, ikiwa imeshinda mara moja, katika msimu wa 1972-73.

Mbali na hao, lakini ipo orodha ndefu ya wachezaji wa Kitanzania waliowahi kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kwa mafanikio makubwa, akiwamo Renatus Njohole, Shaaban Nditi, Twalib Hilal, Zamoyoni Mogellah, Juma Pondamali, Idd Pazi ‘Father’, Ivo Mapunda, Lubigisa Lubigisa, Erasto Nyoni, Jackson Chove, Kassim Seleman ‘Selembe’, Mohammed Banka, David Naftar, Thomas Mourice, Jamhur Kihwelo, Ally Yusuf ‘Tigana’, Mtwa Kihwelo, Said Mwamba ‘Kizota’, Seleman Matola, Mussa Mgosi, Nsa Job, Shadrack Nsajigwa, Ahmed Amasha, Hassan Afif na wengine walicheza katika mataifa mbalimbali yakiwamo ya Arabuni, Afrika, Ulaya na Mashariki na Mbali.

Pia wamo nyota wengine chipukizi kwa sasa wanakiwasha nje ya nchi na kuitangaza Tanzania kama Adolf Bitegeko (Volsungur, Iceland), Morice Abraham (Spartak Subotica, Serbia), Bernard Kamungo (North Texas, Marekani), Yohana Mkomola (Vorskla, Ukraine), Habib Kyombo (TS Sporting, Afrika Kusini), Ibrahim Joshua na Kalos Kirenge (Tusker, Kenya) na wengine kibao na kuionyesha Tanzania ina vipaji vya soka vya kutosha.


WASIKIE WADAU

Athuman Machuppa anasema uoga ndio unasababisha wachezaji wengi wa Tanzania kushindwa kwenda nje kucheza soka la kulipwa huku wengine akipata nafasi wakikata tamaa mapema.

“Wengi wanalewa sifa za hapa nchini, akishaandikwa kwenye magazeti na kusifiwa wanaona wamemaliza. Angalau kwa sasa wanapambana kutoka lakini wengi wanaangalia hapa nilipo hivyo inakuwa ngumu kusogea mbele. Lakini pia wanapotoka nje wapambane zaidi wasikate tamaa mapema na kurejea nyumbani lazima wawe wavumilivu na moyo wa kusaka mafanikio zaidi.

“Jambo lingine linalosababisha wachezaji wengi wasitoke nje kucheza soka la kulipwa ni klabu kuwabania. Inatakia klabu ziwe na malengo na kuwasaidia wachezaji ili wengi watoke ili timu yetu ya tafa inufaike pia,” anasema.

Naye aliyekuwa Kocha wa Gwambina na Mtibwa Sugar, Mohammed Badru ambaye amefanya kazi ya kunoa vituo mbalimbali vya soka nchini England, anasema kitendo cha Tanzania kuwa na wachezaji wengi ambao wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi kinaweza siku moja kuwa faida kwa taifa.

“Inawezekana leo tusione faida yake maana tunaye Samatta pekee ambaye amecheza soka kwenye ngazi ya juu ya mpira Ulaya lakini nawahakikishia kuwa tukiwa na wachezaji wengi mfano sita wakawa wanacheza Ligi Kuu England, wengine Ufaransa, Ureno tunaweza kuwa tishio,” anasema Badru aliyepo Azam U17 kwa sasa na kuongeza;

“Kazi mwalimu itakuwa ndogo ni kutengeneza mpango wa namna ya kucheza tu kwa sababu kila mchezaji atakuwa tayari, kuna siku niliona mazoezi ya timu ya taifa mwalimu anaelekeza kucheza kwa nafasi, nilishangaa sana. Japo kasi yetu sio kubwa ya wachezaji kutokana na wakitoka umri nao unakuwa umesogea lakini ipo siku tunaweza kufika,” anasema kocha huyo.