Prime
Kona za Arsenal na unafiki wa mzungu
HABARI za mjini ni nyingi. Kuanzia uvamizi wa wana wa Israel na Marekani katika ardhi ya Iran. Lini dunia itaacha vita? Hatutajua. Lakini pale katika ardhi ya Mfalme Charles Uingereza. Kona za Arsenal pia ni habari ya mjini. Zinakera na kufurahisha.
Maadui wa Arsenal wanachukia kona zao. Wakati huo huo Arsenal na wafuasi wa timu nyingine pamoja na wachambuzi hawaoni tatizo. Na kuna kina Paul Scholes na Ruud Gullit ambao wanadhani kuna tatizo. Idadi ya watu wanaokerwa na kona za Arsenal wameonekana kuwa wengi zaidi.
Kinachoshangaza ni hawa hawa wanaokerwa na kona za Arsenal ndio hawa hawa ambao wamekuwa wakiisema Arsenal kwa miaka mingi imekuwa ikicheza soka la kuvutia kwa miaka mingi bila ya mataji. Arsenal wamesemwa tangu wakati ule wa Arsene Wenger wakati alipopoteza makali yake. Timu bado ilicheza soka la kuvutia lisilo na mataji. Lisilo na ushindi mwingi.
Wenger alipoondoka akaja Unai Emery ambaye hakuwa na makali sana. Ghafla akaja Mikel Arteta ambaye aliirudisha Arsenal katika soka la kuvutia. Tatizo na Arteta naye amecheza soka la kuvutia lakini ametwaa taji moja tu la FA.
Hili nalo lilikuwa tatizo kubwa kwa wachambuzi. Kwamba unachezaje mpira wa kuvutia bila ya mataji? Arteta alipoteza mataji mbele ya Pep Guardiola na kisha Arne Slot. Dunia ikamcheka.
Msimu uliopita na msimu huu Arteta amejitafutia mbinu nyingine ya kutwaa mataji ili mradi mashabiki wa Arsenal wafurahie. Arsenal imeajiri mtaalamu wa mipira ya faulo (set-pieces) anayeitwa Nico Jover. Ni mfaransa huyu.
Katika mkataba wake na Arsenal kuna kipengele ambacho kinaonyesha kuna bonasi zake anazipata kama Arsenal wakifunga mabao ya mipira hiyo. Jamaa inaonekana anafanya kazi yake kwa ufasaha.
Kuna namna ambayo Arsenal wanaitaka na kuweka genge lao nyuma ya ukuta wa timu pinzani. Wanaelekezana mbinu za namna ya kujichanganya kwa adui wakati Declan Rice au Bukayo Saka wakiwa wanakaribia kupiga faulo.
Mara kadhaa tumeshuhudia wakifunga mipira hiyo. Kwa sasa kona za Arsenal au mipira ya faulo ya Arsenal inayopigwa kando ya uwanja inaonekana kuwa na hatari kama penalti tu. Kuna wazungu wanachukia.
Wazungu wale wale ambao walikuwa wanaicheka Arsenal kwa kucheza soka la kuvutia bila ya mataji. Arsenal wamejitafutia mbinu za kufunga mabao ya aina yoyote ile ili mradi watwae mataji. Wazungu hawataki.
Lakini hapo hapo kumbuka kwamba bado Arsenal ina idadi kubwa ya mabao ya kawaida kuliko haya ya faulo. Hata hivyo huwa yanakumbukwa zaidi mabao ya mipira ya kutengwa kwa sababu yanawapa shida zaidi.
Hapa kuna mambo mawili. Kwanza kabisa kuna timu nyingi ambazo zinakabia chini zaidi (low block) zikicheza na Arsenal. Hizi hazisemwi kwamba zinaharibu mpira kwa sababu zinacheza kwa kujihami zaidi. Hazisemwi. Na ambacho hawaelewi ni kutokana na kukabia chini zaidi ndiyo maana zinatoa mipira mingi ya kona ambayo Arsenal wanaitumia vizuri.
Tatizo hapo tunasahau Arsenal wanafika langoni mwa adui mara nyingi tu kwa kucheza mpira mzuri. Tatizo ni pale zinapokuja kona na kufunga watu huwa wanasahau Arsenal wamepata kona kwa kucheza soka zuri la kushambulia.
Pili watu wanasahau kuna timu nyingi zinafunga mabao haya ya mipira ya kutengwa. Juzi tu Rodri kawafunga Nottingham Forest bao la pili kwa mpira wa kichwa pale pale katika sita ya adui kwa staili ile ile ya Arsenal. Tatizo Manchester City hawana Nico Jover wao.
Hawawezi kurudia jambo hilo mara nyingi wakati Arsenal wanaweza. Niambieni timu nyingine ambayo isingependa kufanya kama Arsenal kama ingejipatia nafasi ya kuwa na mtaalamu kama Nico Jover.
Waingereza wana timu zao mbili wanazipenda zaidi. Manchester United na Liverpool. Ni timu ambazo wanaamini zinalinda tamaduni za Muingereza. Kama mabao haya yangekuwa yanafungwa na Manchester United au Liverpool ungesikia wakiliweka neno 'art' na kupamba.
Kwamba kinachofanyika ni ubunifu wa hali ya juu. Lakini mabao kama haya yakifungwa na Arsenal ndio huwa inasemwa wanaharibu mpira.
Yangekuwa yanafungwa na Manchester City au Chelsea ingesemwa hivi hivi tu wanaharibu mpira. Jaribu kuangalia mpira ambao Pep Guardiola ameupeleka Manchester City kama umesifiwa sana kama inavyostahili. Hapana. Tena kuna makocha Waingereza kama Sam Allardyce alisikika akidai Pep anaharibu mpira wao.
Wenyewe walishazoea kasi na krosi lakini Pep akaja kuweka mpira chini na bado akalaumiwa. Pep ndio ametuletea mpira ambao mabeki wa kati ndio wanamuanzishia kipa wao mpira.
Zilikuwepo nyakati ambazo Stoke City walikuwa wanafunga mabao mengi ya mipira ya kurushwa iliyokuwa inarushwa na staa wao mtaalamu wa kurusha mipira, Rory Delap lakini hatukusikia kelele hizi.
Akina Bolton wamefunga sana kwa mipira ya kona lakini hatukusikia kelele hizi. Tatizo inaonekana Arsenal wamekuwa wataalamu zaidi katika hizi kona na hapo ndipo kelele zinapokuja.
Wazungu hawa hawa ndiyo waliotuambia kama kuna uwezo wa kushinda huku unacheza vibaya basi fanya hivyo. Wenyewe na kiingereza chao wanaita 'winning ugly'. Arsenal wamejaribu kushinda mataji kwa soka lenye mvuto lakini mambo yameonekana kuwa mazito.
Sasa hivi wanashinda kwa njia tofauti tofauti lakini bado wazungu wanalalamika. Hapo ndipo unafiki wa mzungu unapokuja hadharani. Hata Michael Owen amelisema hivi majuzi baada ya Arsenal kuifunga Brighton and Hove.
Pia katika miaka ya karibuni wachezaji wa Arsenal walikuwa wanakejeliwa kwamba ni walaini. Kuna msemo uliokuwa unawananga wa 'London softies'. Akina Patrice Evra, Troy Deeney na wengineo wengi walidai ilikuwa rahisi kucheza na Arsenal kwa sababu ilikuwa na wachezaji laini na walikuwa wanacheza mpira laini.
Hii ilikuwa baada ya kuondoka kwa kina Patrick Vieira na wababe wenzake kisha zikafuata zama za akina Cesc Fabregas.
Leo Arsenal ina wababe wengi wanaocheza soka la kibabe wakiongozwa na akina Gabriel Magalhaes lakini wazungu hao hao wanalalamika. Ndivyo unafiki wao unapojitokeza wakati walikuwa wanawasifu sana Stoke City kwa mpira wa kibabe kiasi kwamba kila mchezaji mzuri aliyehamia Uingereza alikuwa anaulizwa "unaweza kucheza Jumatatu usiku katika mvua dhidi ya Stoke City ugenini?" Leo yote hayo yamesahaulika.
Binafsi naamini Arsenal wanacheza mpira mzuri kuliko ule ambao ulikuwa unawapa mataji Chelsea ya Jose Mourinho. Ule wa pasi moja ndefu kwa Didier Drogba kisha anatumia juhudi zake binafsi kufunga. Kama akiwa katika wakati mgumu anamsubiri Franck Lampard aje ampasie afunge shuti afunge. Yote haya yanasahaulika kwa sababu Arsenal wanafunga kona za kibabe.
Kitu kikubwa zaidi kwa Arsenal ni kuchukua mataji. Timu zinakumbukwa kwa kubeba mataji na sio kucheza mpira mzuri au mbaya. Ndiyo maana Arsenal wenyewe wamekuwa wahanga wa kukejeliwa kwa kucheza mpira mzuri usio na mataji.
Kinachokumbukwa zaidi ni ubingwa na siyo aina ya mchezo uliokuwa unatumika. Sir Alex Ferguson anakumbukwa kwa kutwaa mataji mengi kuliko Arsene Wenger ingawa Wenger alikuwa anacheza mpira kuliko Sir Alex.
Fainali ya ligi ya mabingwa mwaka 1999 inakumbukwa kwa Manchester United kutwaa ubingwa wa dakika za mwisho dhidi ya Bayern Munich. Hakuna anayekumbuka sana mabao yenyewe ya Ted Sheringham na Ole Gunnar Solskjaer yalikuja kwa mipira ya kutengwa ambao leo Arsenal wanalalamikiwa. Huu ni ukweli mchungu. Nadhani hata Sir Alex hawezi kuwa katika upande wa wale ambao wanaishutumu Arsenal kwa mipira ya kona.