Prime
Kompyuta yafichua jambo zito kichapo cha Arsenal kwa Man City

Muktasari:
- Arsenal ilicheza kwa kiwango bora kwelikweli ikiifundisha adabu Man City kwa kuwachapa mabao 5-1 katika mechi ya kibabe kabisa iliyofanyika uwanjani Emirates, juzi Jumapili.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imeshusha kipigo kizito kwa Manchester City, matokeo hayo wala hayasaidii chochote kwenye mchakamchaka wao wa kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, kwa mujibu wa kompyuta maalumu.
Arsenal ilicheza kwa kiwango bora kwelikweli ikiifundisha adabu Man City kwa kuwachapa mabao 5-1 katika mechi ya kibabe kabisa iliyofanyika uwanjani Emirates, juzi Jumapili.
Straika Erling Haaland aliisawazishia Man City baada ya Arsenal kutangulia kwa bao la mapema la Martin Odegaard, lakini kiungo Thomas Partey akairudisha The Gunners kwenye uongozi kinda makinda Myles Lewis-Skelly na Ethan Nwaneri kabla na baada ya bao la Kai Havertz.
Lakini, mambo yote hayo yalikuwa furaha kubwa kwa wachezaji wa Arsenal hasa beki wao Gabriel kwenye vita yake na straika Haaland, ambaye alionekana kusema kitu usoni kwa mshambuliaji huyo baada ya kuongoza 1-0 kabla ya Lewis-Skelly kumdhihaki pia fowadi huyo wa kimataifa wa Norway baada ya kufunga na kushangilia kwa staili ambayo imekuwa ikifanywa na staa huyo wa Pep Guardiola anapofunga.
Haaland aliwajibu mashabiki wa Arsenal baada ya kuwaonyesha nembo ya dhahabu ya Ligi Kuu England iliyopo kwenye jezi yake kabla ya baba yake mzazi, Alfie naye kuliingilia jambo hilo na kuishambulia Arsenal kwenye mtandao wa X.
Ushindi huo uliwapa mashabiki wa Arsenal matumaini ya kushindania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu na kwa sasa ipo nyuma kwa pointi sita dhidi ya vinara Liverpool, ambao bado wana mechi mmoja mkononi dhidi ya mahasimu wao wa Merseyside, Everton - ambao uliahirishwa.
Lakini, kompyuta huyo maalumu imetabiri Liverpool ya Kocha Arne Slot ndiyo itakayonyakua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Kompyuta huyo ilitumia akili mnemba kukokotoa jinsi Liverpool itakavyomaliza ligi ikiwa pointi tisa juu ya Arsenal ya Arteta katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England ambazo zitakuwa mbio za farasi wawili.
Utabiri wa kompyuta ni kwamba Liverpool itashinda mechi 29, itatoka sare sita na kupoteza mechi tatu, hivyo itamaliza msimu ikiwa na pointi 93, sita nyuma ya zile ambazo ziliwapa ubingwa wa taji hilo katika msimu wa 2019-2020 ilipokuwa chini ya kocha Mjerumani, Jurgen Klopp.
Wakati huo, Arsenal imetabiriwa itapoteza mechi mbili zaidi na itamaliza ligi kwenye nafasi ya pili kwa msimu wa tatu mfululizo.
Akili mnemba imetabiri Nottingham Forest itamaliza ligi ya msimu huu kwenye nafasi ya tatu ikiwa imekusanya pointi 74, ikiwa ni pointi 10 nyuma ya Arsenal. Utabiri huo umekuja baada ya Forest kuishushia Brighton kipigo cha mabao 7-0 Jumamosi iliyopita na straika Chris Wood alifikisha mabao 17 baada ya kufunga hat-trick.
Mabingwa mara saba, Man City, ambao msimu huu wamekuwa wakipambana na hali yapo, itamaliza ligi ndani ya Top Four kwa utabiri wa kompyuta hiyo na itafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Hilo litakuwa pigo kubwa kabisa kwa Man City ya kocha Pep Guardiola katika kipindi cha miaka tisa ya kocha huyo akiwa na wababe hao wa Etihad. Lakini, mahasimu wao Manchester United ambao wamekuwa na kiwango kibovu, ikiwamo cha kuchapwa 2-0 na Crystal Palace uwanjani Old Trafford juzi Jumapili, kompyuta inadai itamaliza ligi kwenye nafasi 12 baada ya kuweka rekodi ya hovyo kwenye uwanja wao wa nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya miaka 132. Nafasi hiyo itakuwa ya chini zaidi kuwahi kumaliza tangu Ligi Kuu England ilipoanza mwaka 1992.
Wakati huo, Bournemouth na Newcastle United zitaipiku Chelsea kwenye vita ya kufuzu Europa League, hiyo ina maana The Blues italazimika kwenda kucheza kwenye Conference League kwa msimu wa pili mfululizo.
Fulham itamaliza ligi kwenye nafasi ya nane, wakati Aston Villa itakuwa ya tisa, huku zote zikitabiriwa kumaliza na pointi 61, huu ya Brentford itakayomaliza na pointi 50 na Brighton pointi 48. Tottenham Hotspur iliyomaliza nafasi ya tano msimu uliopita, msimu huu majeruhi wamekuwa wengi kwenye kikosi chao, hivyo watamaliza wakiwa kwenye nafasi ya 16, pointi moja nyuma ya Everton.
Lakini, kuna habari njema kwa mashabiki wa Leicester City, kwa sababu kompyuta utabiri wake ni Wolves, Ipswich na Southampton ndizo timu zitakazoshuka daraja. Southampton itamaliza ligi na pointi 18, hivyo itaizidi Derby kwenye kundi la aibu, ambayo yenyewe ilivuna pointi chache zaidi wakati inashuka daraja katika msimu wa 2007-08, iliposhuka baada ya kukusanya pointi 11 katika mechi 38.