Kocha mpya Dodoma apiga mkwara
Muktasari:
- Kocha huyo amejiunga na Dodoma akitokea Polisi Rwanda baada ya kudumu kwa miaka mitatu na kufanikisha mambo kadhaa, ikiwamo kutwaa ubingwa wa Kombe la Peace Cup 2024, Super Cup 2025, pamoja na kuisaidia timu hiyo kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupita miaka 10.
ALIYEWAHI kuwa kocha wa timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, Vincent Mashami aliyepewa mkataba wa mwaka mmoja wa kuinoa Dodoma Jiji, amepiga mkwara kwamba licha ya kujua ugumu uliopo mbele yake, lakini atapambana kuhakikisha timu hiyo inakuwa tishio kwa msimu wake wa kwanza.
Kocha huyo amejiunga na Dodoma akitokea Polisi Rwanda baada ya kudumu kwa miaka mitatu na kufanikisha mambo kadhaa, ikiwamo kutwaa ubingwa wa Kombe la Peace Cup 2024, Super Cup 2025, pamoja na kuisaidia timu hiyo kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupita miaka 10.
Mafanikio mengine ni kutwaa ubingwa wa Ligi na APR FC, kuiwezesha timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ kutinga robo fainali ya mashindano ya CHAN 2020, pia amewahi kuzifundisha Isonga na Busegera kwa vipindi tofauti.
Mashami anachukua nafasi ya Mecky Maxime aliyeinoa kwa msimu uliopita ambapo Dodoma ilimaliza nafasi ya 12 kati ya timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.
“Ninafurahi kufanya kazi na timu hii, naamini kila kitu kitakuwa sawa na Dodoma itakuwa ni kati ya timu tishio kwenye Ligi,” alisema.
Aliongeza kwa namna alivyopokewa na ushirikiano mkubwa aliopewa basi atahakikisha kila kitu kinakuwa sawa ndani na nje ya uwanja kwa maana ya kuwafurahisha mashabiki.
Katibu Mtendaji Mkuu wa Dodoma Jiji, Johnson Fortunatus alisema mchakato wa kumtafuta mwalimu haikuwa mwepesi, kazi ilikuwa ngumu kwa sababu waliangalia vitu vingi, ikiwamo mahitaji ya klabu na kuangalia mwalimu yupi mzuri.
“Baada ya kumtambulisha mwalimu sasa tutaanza maandalizi ya Ligi, timu itasafiri kwenda Arusha ambako tutaweka kambi ya wiki mbili ya mazoezi ya nguvu,” alisema Fortunatus.
Akizungumzia usajili alisema umekamilika kwa asilimia kubwa na kwamba wamebaki wachezaji watatu tu ambao wanafanya nao mazungumzo ili waweze kufunga zoezi la usajili kwa ajili ya mashindano ya msimu wa 2025-2026.