Kocha KenGold mtihani upo hapa!

Muktasari:
- Kocha huyo raia wa Serbia alitambulishwa Januari, 19, akiongeza nguvu kwenye benchi la ufundi akisaidiana na Omary Kapilima, Jumanne Challe na Uhuru Selaman watakaoamua kushuka au kubaki Ligi Kuu timu hiyo.
WAKATI Kocha mpya wa Ken Gold, Vladslav Heric akianza kazi katika timu hiyo akisaka rekodi ya kwanza nchini, anakabiliwa na mitihani kadhaa itakayompaisha au kumwangusha.
Kocha huyo raia wa Serbia alitambulishwa Januari, 19, akiongeza nguvu kwenye benchi la ufundi akisaidiana na Omary Kapilima, Jumanne Challe na Uhuru Selaman watakaoamua kushuka au kubaki Ligi Kuu timu hiyo.
Pamoja na matumaini ya wengi kutokana na usajili uliofanyika katika dirisha dogo, lakini kocha huyo huenda akajikuta katika wakati mgumu ambao utamfanya kung’ara au kukwama.

Ugeni wake nchini
Mserbia huyu licha ya kushuka Tanzania kwa mbwembwe nyingi, lakini ndiyo mara ya kwanza kufanya kazi nchini, hali ambayo inaweza kumpaisha iwapo atafanya vizuri.
Pia kutokana na ugeni wake, inaweza kumpa ugumu kwa kuwa hana historia yoyote ya soka la Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki licha ya kuishi Kusini mwa Afrika.
Pia anaweza akachukua muda zaidi kuisoma ligi hiyo na pengine kumpa wakati mgumu katika kufanikisha malengo yake.
Ugeni wa Ken Gold
Ken Gold ambayo awali ilijulikana kama Gipco FC (Geita), inashiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza, jambo lililoipa ugumu kutoboa haraka.
Imekumbana na upinzani mkali uliosababisha kushindwa kufanya vizuri huku pia usajili wa dirisha kubwa haukuwa wa kushangaza.
Aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Fikiri Elias aliamini huenda vijana wanaojitafuta wangesaidia na pengine timu kunufaika nao kibiashara, lakini hali imekuwa tofauti na sasa iko mkiani mwa msimamo wa ligi.
Katika michezo 16 ya ligi, imekusanya pointi sita na sasa presha ni kubwa ndani na nje ya uwanja katika vita ya kushuka daraja.

Hamasa na morali
Kutokana na magumu iliyopitia na matokeo yasiyoridhisha imesababisha kushuka kwa morali ya wachezaji na kukata tamaa, hivyo inampa Kocha Heric wakati mgumu wa kuwarejesha sawa kwa kuwaandaa kisaikolojia ili kuwahamasisha pia mashabiki.
Wakati akijiandaa kuipa matokeo, lazima kuwapo hali ya utulivu kikosini kuanzia kiakili na hiyo itasaidia kutengeneza kujiamini kwa wachezaji na kubadili upepo wa matokeo.
Kutokana na matokeo kutokuwa rafiki, hata mashabiki wameonekana kupungua uwanjani katika michezo ya timu hiyo, hivyo kwa sasa ni kusubiri matokeo ya Mserbia huyo kuona mabadiliko.
Utukutu wa wachezaji
Katika kikosi kilichosajiliwa dirisha dogo, Ken Gold imenasa saini za mastaa wengi waliowahi kuvuma ndani na nje ya nchi, hali ambayo imeonekana kurejesha matumaini kwa mashabiki.
Pamoja na matumaini ya wengi kuitabiria mazuri timu hiyo, lakini Mserbia huyo atapaswa kuwa ‘mbogo’ kuhakikisha utulivu unakuwapo kikosini.
Wachezaji kama Kelvin Yondan, Benard Morrison na Obrey Chirwa ni baadhi ya mastaa wenye uwezo lakini misimamo ya ndani na nje ya uwanja na kama hawataangaliwa zaidi, huenda ikaja stori mpya.
Morrison ambaye anafahamika kwa historia na rekodi zake kwa timu alizotoka ikiwamo Yanga na Simba, wengi wanasubiri kuona hatma yake katika kikosi hicho ukizingatia mazingira iliyopo.

Mazingira ya timu
Tofauti na timu nyingine za Ligi Kuu zenye makazi yao maeneo ya mijini na jijini, Ken Gold makazi yake ni wilayani Chunya nje ya Jiji la Mbeya.
Ikiwa jijini Mbeya ni sawa na ugenini kwa kuwa hata uwanja wa mazoezi haina na inategemea zaidi Isyesye unaotumiwa na Mbeya City kutokana na uwanja wao uliotegemewa kutokuwa tayari huko Kiwanja wilayani humo.
Hata hivyo, kocha huyo ‘mzungu’ na wachezaji wake hasa wa kigeni watapaswa kuwa wavumilivu kwa maisha iliyonayo timu hiyo ili kufanya kazi kwa juhudi na bidii ili kufikia malengo.

Kauli ya kocha
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kutambulishwa, Mserbia huyo anasema licha ya kuwa mara yake ya kwanza kufanya kazi nchini, anasaka rekodi ili kuendelea kuishi Tanzania.
Anakiri licha ya presha iliyopo kutokana na matokeo iliyonayo timu, lakini matarajio yake ni kuona anabadili upepo kuhakikisha wanafanya vizuri na kubaki salama Ligi Kuu.
Anabainisha katika mikakati yake si kutafuta nafasi tatu wala nne za juu, badala yake ni kuona wanabaki kwenye ligi na falsafa yake ni soka la ushindani na nidhamu.
“Sitatafuta ubingwa wala nafasi nne za juu, lengo ni kubaki Ligi Kuu na falsafa yangu ni soka la ushindani, kasi na nidhamu na naamini kwa ushirikiano na wenzangu tutafikia malengo.”
Kuhusu hali ya wachezaji baada ya kuanza mazoezi, kocha huyo anasema licha ya kuwa mapema, lakini ameona mabadiliko na anachoelekeza kwa wachezaji wanaonesha kuelewa na matarajio yake ni kufanya vizuri.
“Natengeneza muunganiko na utimamu, nakazia zaidi eneo la straika, beki na timu kwa jumla ili kabla ya mechi yetu dhidi ya Yanga, Februari 5 tuwe fiti na kupata matokeo mazuri,” anasema Mserbia huyo.
Timu alizofundisha
Kabla ya kutua nchini, Mserbia huyo mwenye maneno mengi amezitumikia Orlando Pirates, Chippa United, Martebarg United aliyokuwa chini ya kocha Fadlu Davids (Simba), Black Leopard na Welcome Football Academy ya Afrika Kusini.

Mastaa wafunguka
Nahodha wa timu hiyo, Mishamo Daud anasema baada ya kutokuwa na matokeo mazuri mzunguko wa kwanza, lakini uongozi na benchi la ufundi waliona walipokosea na kusahihisha.
Anasema mabadiliko ya wachezaji walioingia na kocha mpya wanaenda kubadili upepo na kuirejesha kwenye ramani mpya Ken Gold wakishirikiana na sisi waliotukuta kufikia malengo.
“Mashabiki warejeshe upya matumaini kwakuwa timu ni mpya, kila mmoja ana nia ya kuhakikisha timu inabaki salama Ligi Kuu msimu ujao, mzunguko wa pili utakuwa na mafanikio kwetu,” anasema straika huyo.