KINAPIGWA TENA: Ni wikiendi ya KO ya Mama Dar
Muktasari:
- Japo mapambano yanashuhudiwa na watu wachache wanaokwenda ukumbini, lakini haijazuia mapambano na kila wikiendi zinachapwa, kama itakavyokuwa Jumamosi, Oktoba 5, mwaka huu kwenye Ukumbi wa City Centre, Magomeni, Dar es Salaam, katika pambano la Knockout ya Mama lililoandaliwa na Mafia Boxing Promotion.
UHONDO wa ngumi unaweza ukadhani umesimama. Hapana. Licha ya sasa kutokuonyeshwa kwenye runinga kama awali baada ya Kampuni ya Azam Media kujitoa, lakini huko kitaa kinapigwa haswa.
Japo mapambano yanashuhudiwa na watu wachache wanaokwenda ukumbini, lakini haijazuia mapambano na kila wikiendi zinachapwa, kama itakavyokuwa Jumamosi, Oktoba 5, mwaka huu kwenye Ukumbi wa City Centre, Magomeni, Dar es Salaam, katika pambano la Knockout ya Mama lililoandaliwa na Mafia Boxing Promotion.
Wikiendi iliyopita katika Ukumbi wa Hipro, bondia Jesca Mfinanga alipanda ulingoni dhidi ya Ellen Simwaka wa Malawi katika na kupoteza kwa pointi, huku mchekeshaji aliyehamia kwenye ngumi za kulipwa Miraji Supakila ‘Mkali Wenu’ alishinda pambano lake.
Pambano lingine lililofanyika Makunduchi Villa, Kigamboni, Mwanaspoti lilishuhudia bondia Barnaba Alexander ‘muuza madafu wa Ikulu’ aliyetambulika zaidi kama Komando Madafu akipoteza kwa pointi dhidi Mohamed Omary.
Wikiendi ijayo, Mafia Boxing Promotion imeandaa pambano hilo ikiwa imesheheni mikanda mikubwa miwili itakayowaniwa katika pambano hilo na bondia Said Chino atapanda ulingoni kuwania mkanda wa ubingwa wa mabara wa IBA dhidi ya Lusanda Komanisi wa Afrika Kusini katika pambano kuu ‘main card’ ambalo litapigwa kwa raundi 10.
Pia, nahodha wa Mafia Boxing, Ibrahim Mafia atapanda ulingoni kuwania mkanda wa ubingwa wa Baraza la Ngumi Duniani, WBC Afrika dhidi ya Enock Tetteh wa Ghana, Mafia anakuwa bondia wa pili kuwania mkanda wa ubingwa wa huo ndani ya ardhi ya Tanzania baada ya bondia namba moja nchini, Fadhili Majiha.
Mwanaspoti linakuchambulia mabondia wote wanaotarajia kupanda ulingoni kwenye pambano hilo ambalo limepewa jina la Knockout ya Mama.
Said Chino vs Lusanda Komanisi
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Mtanzania, Said Chino ‘The Bull Dog’ kuwania mkanda wa kimataifa akiwa ndani ya Tanzania dhidi ya Lusanda Komanisi ‘School Boy’ wa Afrika Kusini.
Chino mwenye rekodi ya mapambano 36, sawa na raundi 183, ameshinda mapambano 22 na kati hayo, 15 ni kwa knockout na amepigwa mara 12 kati hizo tatu ni kwa knockout na sare mara mbili.
Bondia huyo ametoa ahadi ya kushinda pambano hilo katika mkutano maalumu na waandishi wa habari huku akimwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan kuja kuona uwezo wake wa kushinda kwa knockout ni asilimia 68.18.
Lakini kwa mpinzani wake kutoka Afrika Kusini, Lusanda Komanisi mwenye rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 35, sawa na raundi 164, ameshinda 27 kati ya hayo 22 ni kwa knockout huku akiwa amepigwa mara nane kati ya hizo tano ni kwa knockout na hajawahi kutoka sare.
Upande wa nafasi, Chino anakamata nafasi ya tano kati ya mabondia 102 wa uzani wa Light nchini na duniani akiwa wa 220 kati ya 2413 wakati mpinzani wake akiwa wa 160 kati ya 2413 na nchini kwao akiwa ni wa nne kati ya 43 wa uzani huu.
Komanisi na Chino watapanda ulingoni kwenye pambano la kuwania mkanda wa ubingwa wa mabara wa IBA katika uzani wa Light, raundi 12 na Komanisi uwezo wake wa kushinda kwa knockout ni asilimia 81.68, akimzidi Chino kwa asilimia 13.5 na wote wakiwa na hadhi ya nyota mbili.
Ibrahim Mafia vs Enock Tettey Tetteh
Ibrahim Mafia ndiye bondia ambaye amebeba jina la gym ya Mafia Boxing Gym na Mafia Boxing Promotion kutokana na kuwa ndiye bondia wa kwanza kusainiwa kwenye menejimenti hiyo inayomiliki gym ya kisasa pamoja na ukumbi wake kwa ajili ya mapambano ya mchezo huo City Centre uliopo Magomeni, Sokoni.
Mafia ni bondia namba moja kwenye uzani wake wa Super Bantam, akiwa na jumla ya mapambano 11 sawa na raundi 50 ikiwa kila raundi ina wastani wa dakika 210 ikiwa kila raundi imebeba dakika tatu.
Mafia atapanda ulingoni kwenye pambano la kuwania mkanda wa ubingwa wa WBC Afrika akiwa ameshinda mapambano 10, kati ya hayo saba ni kwa knockout na hadi sasa hajui uchungu wa kupigwa zaidi ya kutoka sare mara moja.
Bondia huyo anayetarajiwa kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa pili kuwania mkanda wa ubingwa huo ndani ya ardhi ya Tanzania na anakamata nafasi ya nne kwa sasa katika mabondia wote nchini kwenye ‘Pound for Pound’ ya mabondia bora.
Mafia mwenye hadhi ya nyota tatu, anakamata nafasi ya kwanza kwenye uzani wake kati ya mabondia 53 wakati duniani akiwa ni 34 kati ya 1361 huku akiwa na uwezo wa kushinda knockout kwa asilimia 70.
Mpinzani wake, Enoch Tetteh kutoka Ghana hadi sasa amecheza mapambano 12, sawa na raundi 78 ikiwa ni wastani wa dakika 234.
Bondia amefanikiwa kushinda mara 11 kati ya hizo tisa ikiwa ni knockout na ametoka sare mara moja pekee huku akiwa hajawahi kupigwa kama ilivyo kwa mpinzani wake.
Tetteh mwenye hadhi ya nyota mbili kwenye uzani wa super bantam anakamata nafasi ya tatu kati ya mabondia 31 wa uzani huo nchini kwao, huku duniani akiwa ni wa 164 kati ya 1361 huku uwezo wake wa kupiga kwa knockout ukiwa ni asilimia 81.82.
Salmin Kassim vs Noli Maquilan
Kutokuonyeshwa kwa mapambano huenda kumesababisha mashabiki wengi kutokushuhudia kipaji kikubwa cha bondia chipukizi, Salmin Kassim katika pambano la Knockout ya mama litakalopigwa Oktoba 5, mwaka huu.
Bondia huyo atapanda ulingoni dhidi ya Noli Maquilan kutoka Ufilipino, akiwa na rekodi ya kucheza mapambano saba pekee ambayo sawa na raundi 39, amefanikiwa kushinda mapambano matano kati ya hayo matatu ameshinda kwa Knockout, ametoka sare mara mbili na hajawahi kupigwa.
Kassim anakamata nafasi ya pili uzani wa super Bantam kati ya mabondia 53 akiwa na hadhi ya nyota mbili na nusu, duniani akiwa ni wa 79 kati ya 1361 huku uwezo wake wa kupiga Knockout ukiwa ni asilimia 60.
Mpinzani wake kutoka Ufilipino, Noli Maquian ambaye atapanda ulingoni kwenye pambano hilo la raundi nane lisilokuwa la ubingwa, rekodi yake ni moto kweli.
Bondia huyo hadi sasa amecheza mapambano 11 pekee akishinda 10 kati ya hayo saba ni kwa Knockout huku akiwa amepigwa mara moja.
Mfilipino huyo ndiye bondia pekee mwenye hadhi ya nyota nyingi, akimiliki tatu na nusu na atapanda ulingoni kwenye pambano hilo akishika nafasi ya pili nchini kwao kati ya mabondia 90 wa uzani wa bantam huku duniani akiwa wa 18 kati ya 1120.
Maquilan uwezo wake wa kushinda kwa Knockout ni asilimia 70 akimzidi Salmini kwa asilimia 10 katika kiwango hicho.
Kalolo Amiri vs Thato Bonokoane
Kipaji kingine ambacho kitaonekana kwenye pambano la Knockout ya Mama ni Kalolo Amiri pia kutoka Mafia Boxing Gym chini ya Mafia Promotion.
Bondia huyo kutoka katika uzani wa super bantam hadi sasa amecheza jumla ya mapambano tisa akishinda nane kati ya hayo matano, ameshinda kwa knockout na ametoka sare mara moja pekee, hajawahi kupigwa.
Kalolo anashika nafasi ya tatu katika uzani wa super bantam nchini kati ya mabondia 53 wakati duniani akiwa ni wa 96 kati ya 1361.
Bondia huyo mwenye hadhi ya nyota mbili ana uwezo wa kushinda kwa knockout kwa asilimia 62.5% pekee, wakati mpinzani wake Thato Bonokoane kutoka Afrika Kusini atakayepigana naye pambano la raundi nane lisilokuwa la ubingwa katika uzani wa super bantam ana rekodi ya kucheza mapambano 24 akishinda 14 kati ya hayo tisa ni kwa knockout na amechapwa mara saba kati ya hizo tatu ni kwa knockout, huku akiwa amtoka sare mara tatu.
Bondia huyo mwenye hadhi ya nyota moja na nusu anashika nafasi saba kati ya mabondia 44 wa uzani huo kwao Afrika Kusini na duniani akiwa wa 177 kati ya 1361, huku uwezo wake wa kushinda Knockout ukiwa ni asilimia 64.24.
Frank Shagembe vs Henriques Lando
Zao lingine kutoka Mafia ambalo litapanda ulingoni katika pambano la kimataifa ni Frank Shagembe atakayezichapa na Henriques Lando wa Angola.
Shagembe mwenye rekodi ya kucheza mapambano mawili akiwa ameshinda yote, moja likiwa ni kwa knockout, hadi sasa hajapigwa wala kutoka sare.
Bondia huyo wa uzani wa super middle atapanda ulingoni kwenye pambano lisilokuwa la ubingwa la raundi sita akiwa na hadhi ya nyota moja tu.
Shagembe anakamata nafasi ya nane kati ya mabondia 22 nchini na duniani akiwa wa 428 kati ya 1623 huku uwezo wake wa kushinda knockout ukiwa ni asilimia 50 pekee.
Mpinzani wake kutoka Angola, Henriques Lando ambaye hadhi yake ni nyota moja na nusu mpaka sasa amepigana mara 17, ameshinda mara tisa, kati hizo saba ni kwa knockout na amepigwa mara nane kati ya hizo moja ni kwa knockout.
Lando ni bondia pekee katika uzani wa super middle wakati duniani akiwa ni 191 kati ya mabondia 1623 wa uzani huo na uwezo wa kushinda kwa knockout ukiwa ni asilimilia 77.78.
Mabondia wengine wanaotarajia kupigana mapambano ya ndani yaani wote kutoka nchini katika pambano hilo ni Issa Nampepeche dhidi ya Prosper Alex, Hassan Mandula na Juma Thabit wakati Hussein Azenga akipewa Abada Ferouz huku Yohana Mchanja na Kato Machemba wapinzani wao upande wa kimataifa hawajawekwa wazi hadi sasa.