KINAPIGWA: Hatimaye Kiduku, Pialali warudi mjini

Muktasari:
- Katika pambano hilo ambalo limeandaliwa na promosheni ya Mafia Boxing, litawakutanisha mabondia kama Twaha Kiduku, Idd Pialali, Dullah Mbabe, Loren Japhet, Tanzania one, Fadhili Majiha huku Mchanja Yohana akitararajia kutetea mkanda wake wa ubingwa wa WBO Global dhidi ya bondia kutoka Namibia.
MEI 24, mwaka huu kwenye Viwanja vya Posta Kijinyama, jumla ya mabondia 30 watapanda ulingoni katika pambano la kimataifa la Knockout ya Mama phase 4, wakiwemo mabondia wenye majina makubwa ambao hawajaonekana muda mrefu kwenye majukwaa makubwa ya mchezo huo.
Katika pambano hilo ambalo limeandaliwa na promosheni ya Mafia Boxing, litawakutanisha mabondia kama Twaha Kiduku, Idd Pialali, Dullah Mbabe, Loren Japhet, Tanzania one, Fadhili Majiha huku Mchanja Yohana akitararajia kutetea mkanda wake wa ubingwa wa WBO Global dhidi ya bondia kutoka Namibia.
Ikumbukwe baadhi ya mabondia wenye majina ambao kwa sasa ndiyo wanabeba taswira ya mchezo huo hakuonekana ulingoni tangu katikati ya mwaka jana baada ya Azam kusitisha kuonyesha mchezo huo kupitia runinga.
Mwanaspoti linakuchambulia mapambano hayo ambayo yatawarudisha wanyama wakali wa mchezo huo walioanza kusahaulika na kutazamiwa kuwa yenye mvuto mkali.
MCHANJA YOHANA VS FILLEMON NGHUTENANYE
Bingwa wa WBO Global, Mchanja Yohana ndiye anatarajia kupanda ulingoni kucheza kwenye pambano kuu ‘main card’ akiwa na kibarua cha kutetea mkanda wake wa ubingwa wa WBO Global dhidi ya Fillemon Nghutenanye wa Namibia.
Mchanja mwenye rekodi ya kucheza mapambano 27 akiwa ameshinda 20, kati ya hayo 14 kwa Knockout, amepigwa mara sita na ametoka sare moja, huku akiwa bondia wa namba moja kwenye uzani wa Fly kati ya mabondia 40 wakati duniani ni wa 33 kati ya 790 huku akiwa na hadhi ya nyota mbili na nusu.
Wakati mpinzani wake siyo bondia wa kawaida kutokana na hadhi ya nyota tatu akiwa na jumla ya mapambano 14 pekee hali inayosababisha ugumu wa pambano hilo litakalopigwa kwa raundi 12.
Fillemon ameshinda mapambano 12 kati ya hayo manne ni kwa Knockout na ametoka sare mara nne huku akiwa bondia namba moja kwenye uzani wq fly nchini Namibia wakati duniani akiwa bondia wa 20 kati ya 790.
IDD PIALALI VS SNOWDEN MUNYANJE
Julai 20, mwaka jana ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kwa Pialali kuonekana ulingoni baada ya kumchapa Kiaku Ngoy wa Malawi jijini Mbeya kabla ya Mafia Boxing kumrudisha mjini Mei 24, mwaka huu.
Pialali mwenye rekodi ya kucheza mapambano 49 atapanda ulingoni kwenye pambano la raundi nane, uzani wa walter dhidi ya Snowden Munyanje kutoka Malawi, ameshinda mara 36 kati ya hizo 25 kwa Knockout na amepigwa mara 10 kati hizo saba ni kwa Knockout huku akitoka sare mara moja.
Bondia huyo mwenye nyota moja na nusu, anakamata nafasi ya sita kati ya mabondia 56 wa uzani wake nchini wakati duniani ni wa 332 kati ya 2498.
Mpinzani wake, Munyanje amecheza jumla ya mapambano saba, ameshinda manne yote kwa Knockout, amepigwa mara tatu kati ya hizo moja ni kwa Knockout, anakamata nafasi ya kwanza nchini kwao katika mabondia tisa wa uzani huo, wakati duniani ni wa 606 kati ya 2693.
DULLAH MBABE VS ALICK MWENDA
Februari 28, mwaka huu alimwaga machozi baada ya kuchapwa na Mzambia, Mbachi Kaonga, Dullah Mbabe atapanda ulingoni kujiuliza katika pambano la raundi nane lisilokuwa la ubingwa kwenye uzani wa super middle dhidi ya Alick Mwenda kutoka Malawi.
Mbabe atapanda ulingoni akiwa na rekodi ya kucheza mapambano 52, ameshinda 35 kati ya hayo 30 ni Knockout, amepigwa mara 15 kati ya hizo mara tatu ni kwa Knockout huku akitoka sare mara moja.
Bondia huyo kwa sasa anakamata nafasi ya saba katika mabondia 37 nchini kwenye uzani huo wakati duniani ni wa 338 kati ya 1773 huku akiwa na nyota moja.
Kwa upande wa mpinzani wake, Alick Mwenda kutoka Malawi mwenye nusu nyota, amecheza jumla ya mapambano 29, ameshinda 11, kati ya hayo matano ni kwa Knockout, amepigwa mara 18 kati ya hizo tisa ni kwa Knockout.
Snowden anakamata nafasi ya tatu katika mabondia wa uzani wa lightheavy kati ya mabondia watano wakati duniani ni wa 821 kati ya 1772.
TWAHA KIDUKU VS LIMBANI LANO
Kiduku akiwa na hadhi ya nyota mbili, mara ya mwisho kupanda ulingoni ndani ya nchi ilikuwa ni Aprili mwaka jana kabla ya kwenda kudundwa Ujerumani kwa pointi.
Mafia Boxing kupitia Knockout ya Mama phase 4, inamrudisha tena bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 35 akiwa ameshinda 24 kati ya hayo tisa kwa Knockout, amepigwa mara 10 kati hizo moja ni Knockout huku akitoka sare mara moja.
Kiduku atapanda ulingoni akiwa bondia namba mbili kwenye uzani wa supermiddle katika mabondia 37 wa uzani huo nchini, huku duniani ni wa 160 kati ya 1773.
Lakini mpinzani wake kutoka Malawi, Limbani Lano, mwenye hadhi ya nusu nyota, amecheza mapambabano 27, ameshinda nane kati ya hayo manne kwa Knockout, amepigwa mara 17, kati ya hizo nane kwa Knockout na ametoka sare mara mbili.
Lano ni bondia wa nne katika mabondia watano wa uzani wa lightheavy wa Malawi na duniani anakamata nafasi ya 894 kati ya 1772.
FADHILI MAJIHA VS MOHAMED FUSEIN
Tanzania One, Fadhili Majiha ni miongoni mwa mabondia watakaopanda ulingoni kwenye pambano hilo na atapanda ulingoni dhidi ya Mohamed Fusein wa Ghana katika pambano la raundi nane, uzani wa Bantam.
Majiha mwenye hadhi ya nyota nne na rekodi ya kucheza mapambano 52 akiwa ameshinda 34 kati ya hayo 15 ni kwa Knockout, amepigwa mara 14 kati hizo tatu ni kwa Knockout na ametoka sare mara nne.
Majiha ndiye bondia namba moja katika orodha ya mabondia bora wa Tanzania kwa sasa na namba moja kwenye uzani wake wa bantam kati ya mabondia 62, huku duniani akiwa wa 10 kati ya 1159.
Mpinzani wake, Fusein mwenye nyota mbili ana rekodi ya kucheza mapambano 12 akiwa ameshinda mapambano 11, kati ya hayo 10 ni Knockout na ametoka sare mara moja.
Fusein kutoka Ghana ni bondia namba moja katika mabondia 13 wa uzani wake nchini kwao wakati duniani ni wa 126 kati ya 1159.
RICHARD MTANGI VS MICHAEL MUTUMBA
Richard Mtangi mwenye hadhi ya nyota mbili na nusu akiwa ni zao la Mafia Boxing Promotion, atapanda ulingoni kwenye pambano hilo akiwa na rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 10, ameshinda manane kati ya hayo saba ni Knockout, amepigwa mara moja na ametoka sare moja.
Mtangi ni bondia wa pili kwa ubora katika uzani wake wa middle kati ya mabondia 50 nchini wakati duniani ni wa 95 kati ya 2013.
Mpinzani wake kutoka Uganda, Michael Mutumba ana rekodi ya kucheza pambano moja pekee ambalo ameshinda kwa knockout. Mutumba ambaye ana hadhi ya nyota moja na nusu ni bondia wa tano kati ya mabondia 27 wa uzani wa walter nchini kwao wakati duniani anashika nafasi ya 398 kati ya 2498.
Wengine watakaopanda ulingoni kwenye pambano hilo ni Said Bwanga ambaye mpinzani wake bado hajawekwa wazi, Tano Juma dhidi ya Sahar Chauha kutoka India, Luqman Kimoko dhidi ya Sagar Chand wa India, Saleh Kassim dhidi ya Sowali Ssentongo wa Uganda.
Lakini Loren Japhet atamvaa Farehet Manirola, George Kanduru wa Malawi akipewa Abdulrahman Magoma wengine ambao watapanda ulingoni kwenye pambano hilo ambao wapinzani wao hawajawekwa wazi ni Oscar Richard, Asemahle Wellem na Kalolo Amiri.