Kinachovitafuna viwanja Ligi Kuu Bara hiki hapa
Muktasari:
- Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi inayofanya viwanja vingi kupoteza ubora sehemu ya kuchezea.
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kila msimu limekuwa likivifungia viwanja vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu Bara si chini ya vitatu. Hii inatokana na kutokidhi vigezo vya kikanuni. Baadhi ya yale yanayotajwa kutokidhi vigezo kikanuni, ni sehemu ya kuchezea kukosa ubora unaostahili.
Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi inayofanya viwanja vingi kupoteza ubora sehemu ya kuchezea.
Msimu huu 2025-2026, tayari TFF imetangaza kuufungia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi uliopo Tabora, uamuzi huo umefanyika Septemba 20, 2025 muda mchache baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya TRA United dhidi ya Dodoma Jiji iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Wakati msimu huu hali ikiwa hivyo, msimu uliopita 2024-2025, Uwanja wa Jamhuri uliopo Dodoma, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi (Tabora), Uwanja wa Benjamin Mkapa (Dar es Salaam), Uwanja wa Liti (Singida) na Uwanja wa CCM Kirumba (Mwanza), vilifungiwa kutumika baada ya sehemu ya kuchezea kupoteza ubora wake.
CHANZO CHA TATIZO
Takwimu za Rapid Transition Alliance zinaonyesha michezo inachangia asilimia 0.8 ya hewa ukaa duniani sawa na uzalishaji wa gesi chafu wa nchi ya kati kwa ukubwa.
Mabadiliko ya tabianchi tayari yanaathiri kwa kiasi kikubwa michezo katika ngazi zote, kitaifa na kimataifa. Maeneo ya kuchezea yanazidi kuwa hatarini kwa sababu ya hali mbaya ya hewa.
Mafuriko ya msimu wa baridi hufanya viwanja visitumiwe, na hivyo kuathiri ratiba za michezo, kushusha ushiriki wa wanamichezo na kupunguza hamasa ya mashabiki.
Ripoti zinabainisha ifikapo mwaka 2050, inakadiriwa kuwa karibu robo ya viwanja vya soka vitakuwa vimefurika kwa sehemu au kwa ujumla.
Majira ya joto yenye joto kali na vipindi virefu vya ukame pia vinatishia uhai wa viwanja na maeneo ya michezo katika michezo mbalimbali. Viwango vya juu vya joto pamoja na ubora duni wa hewa wakati wa kiangazi vinahatarisha shughuli za michezo katika ngazi zote.
Wanamichezo wengi sasa wamekuwa wakikumbwa na uchovu wa joto, hali inayoshusha kiwango cha utendaji wao na kuhatarisha afya na ustawi wao.
Sera za kukabiliana na joto kali, ambazo hapo awali zilionekana kama tahadhari kwa hali zisizotarajiwa, sasa zimekuwa sehemu ya kawaida katika mashindano mbalimbali ya michezo.
Uchunguzi wa Mwanaspoti uliofanyika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mbeya, Kigoma na Singida, umebaini athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia baadhi ya viwanja vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu Bara na Ligi ya Championship.
Athari hizo zimeenda mbali zaidi hadi kuchangia majeraha kwa wanasoka na wengine kunyemelewa na matatizo ya kiafya. Hiyo ni kwa mujibu wa madaktari waliofanya mahojiano na Mwanaspoti.
WAATHIRIKA WAKUU
Wachezaji
Wachezaji wa mpira wa miguu wanakumbwa na changamoto mbalimbali kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Joto kali huongeza hatari ya kupata madhara ya kiafya kama vile upungufu wa maji mwilini. Kwa mfano, katika Olimpiki ya Paris 2024, wachezaji walikumbwa na joto kali lililofikia nyuzi joto 35°C, hali iliyowalazimu baadhi yao kuhitaji huduma za matibabu kutokana na madhara ya joto.
Hali mbaya ya hewa huongeza hatari ya majeraha kwa wachezaji. Kwa mfano, joto kali husababisha uchovu wa haraka na upungufu wa maji mwilini, hali inayoweza kusababisha majeraha ya misuli na viungo.
Kwa msimu wa Ligi Kuu Bara 2024-2025, rekodi zinaonyesha zimechezwa mechi 36 mchana wa jua kali, huku timu 13 kati ya 16 zikiwa ndizo zimecheza mechi hizo.
Ni Simba, Yanga na Azam ndizo pekee ambazo hazijawahi kucheza mchana katika ligi hiyo tangu ipate udhamini wa Azam Media ambayo ndio yenye haki ya matangazo ya mechi upande wa televisheni. Ligi hiyo inashika nafasi ya nne kwa ubora Afrika baada ya Misri, Morocco na Algeria.
Baadhi ya timu kati ya hizo 13 zimekuwa zikicheza mechi zinazopigwa kati ya saa 7:00 mchana hadi saa 8:00 mchana na kuendelea, tofauti na ilivyozoeleka nyingi kupigwa kuanzia saa 10:00 jioni hadi zile za usiku.
Takwimu zinaonyesha katika mechi 36 kati ya 240 zilizochezwa msimu wa 2024-2025, timu tatu za KenGold iliyoshuka daraja, Tanzania Prisons na Singida Black Stars ndizo zilizopigika juani, zikishuka uwanjani mara nane kila moja.
Pia Uwanja wa Sokoine uliopo jijini Mbeya ndio unaoongoza kwa kuchezwa mechi nyingi za saa 8 mchana kwani zimepigwa 12, huku wenyeji wa uwanja huo, KenGold na Tanzania Prisons kila moja ikicheza mara sita.
Timu hizo za Mbeya pia zimeshuka viwanja vya ugenini mara mbili kukabiliana na wapinzani wao majira ya saa 8 mchana na kukamilisha idadi ya mechi nane kwa kila moja.
Kwa Singida Black Stars yenye maskani yake mjini Singida ikiutumia Uwanja wa Liti, mechi nane ilizocheza saa 8 mchana, tano imekipiga ikiwa nyumbani na tatu ugenini.
Licha ya kuelezwa kwamba upangwaji wa ratiba kwa mechi za mchana kwa baadhi ya timu umejikita zaidi kwa ishu za kibiashara kutoka kwa watangazaji wenye haki ya kurusha mechi hizo, lakini inaelezwa kuna athari ambazo hupatikana kwa wachezaji kucheza mchana wa jua kali, na wanaokosoa utaratibu huo wanaona klabu za nje ya Kariakoo na Mzizima tu ndizo zinazopangwa mchana.
Wajenga hoja wamesema hata Ulaya katika ligi kuu tano maarufu zipo mechi zinazogusa vigogo wa ligi hizo za England, Ufaransa, Hispania, Italia na Ujerumani zimekuwa zikipangwa mchana badala ya jioni na usiku ili kutoa uwiano sawa kwa timu zote, tofauti na hali ilivyo kwa Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, inaelezwa kwa mechi za Ulaya kupigwa mchana wa saa 8 au saa 6 mchana, huwa ni mazingira na hali ya hewa ambayo ni ya baridi kulinganisha na Afrika Mashariki ambao ni ukanda wa kitropiki wenye hali ya hewa ya joto na wachezaji hutokwa jasho jingi.
Mbali na hayo, lakini inaelezwa kuwa kucheza kwenye joto kali huweza kusababisha ngozi kubabuka, kizunguzungu na hata wachezaji kuzimia kwa upotezaji huo wa maji na chumvi chumvi mwilini.
Baadhi ya madaktari wa timu za Ligi Kuu Bara wamefichua kitendo cha kucheza mechi au kufanya mazoezi kipindi cha joto kali kuna madhara na kama wachezaji hawatapewa elimu ya kutosha, basi kuna hatari zaidi ya wengi wao kupata majeraha na matatizo mengine ya kiafya.
Daktari wa Simba, Edwin Kagabo amesema: “Sababu kubwa ya hatari hiyo ni kutokana na mwili kupoteza maji na chumvi au madini mwilini kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida. Ndio maana kumekuwa na utaratibu wa wachezaji kutumia maji kwa wingi hasa kipindi cha joto kali.
“Endapo upotevu wa maji mwilini hautadhibitiwa ndivyo hatari ya athari hizo zinavyokuwa juu na pia kadri hali ya hewa ya joto inapozidi kuwa juu ndivyo maji hupotea zaidi mwilini.”
Kagabo amesema kawaida mwili huhitaji maji na chumvichumvi kwa ajili ya kazi mbalimbali za mwili ikiwamo msukumo wa damu na kazi seli.
“Wachezaji ambao wamekuwa wakicheza mechi katika mazingira ya joto huku wakifanya mazoezi makali wanatakiwa kunywa maji mengi lakini pia wazungumze na waamuzi ili kuwazingatia kwa kuwapa mapumziko ya mara kwa mara ili waweze kunywa maji ya kutosha kuepusha shida ambazo zinaweza kuwapata.
“Kuvuja jasho sana huwa ni zaidi wakati wa kucheza katika joto kali na wakati huohuo kadri jasho linavyotoka kwa wingi na ndivyo pia mwili unavyopoteza maji kupita kiasi. Matatizo mbalimbali ya kiafya yanaweza kujitokeza endapo tu mchezaji atapata upungufu mkali wa maji mwilini na chumvichumvi kutokana na kuvuja jasho.
“Mara nyingi wachezaji ambao wanapata madhara haya kirahisi ni wale ambao hawanywi maji ya kutosha kabla ya mechi na vilevile kutokula vyakula vyenye maji na madini ikiwamo matunda na mboga.
“Madini chumvi kwenye mwili wa binadamu ni muhimu sana na hasa kwa wachezaji ambao wanafanya kazi ambayo inawatoa jasho jingi hivyo wakikosa hayo wanaweza kupoteza fahamu lakini pia anaweza akapata degedege,” amesema Dk Kagabo na kuongeza:
“Lakini pia wachezaji wanapata shida ya kuchanika nyama za paja na misuli kukaza kutokana na kukosa baadhi ya madini muhimu ambayo yanaondoka mwilini kwa njia ya jasho.”
Amesema hali hiyo kiafya imekuwa ikichangia pia wachezaji kuumia na kubana kwa makundi ya misuli ikiwamo ile ya nyuma ya paja ambayo ni muhimu kwa mchezaji kama wa soka.
Kagabo amesema madhara mengine yanayoweza kutokea kutokana na hali ya kutokwa sana na jasho na kupungiwa maji mwilini ni pamoja na kichwa kuuma, kuona mawimbi, mwili kuwa dhaifu, kushindwa kutulia, kukosa umakini mazoezini au mchezoni, kuchanganyikiwa, kichwa kuuma na mwili kuuma.
“Tatizo hilo la upungufu wa maji kutokana na joto kali linaweza kumfanya mchezaji akashindwa kucheza kwa kiwango bora hasa kukiwa na ratiba ngumu ya mechi mfululizo kwa sababu hawarudi haraka kwenye utimamu kutokana na kupoteza nguvu kazi nyingi kwa mchezo mmoja.”
Kwa upande wa Daktari wa KenGold, Amina Turusa amesema: “Ukiona mchezaji baada ya mechi ya mchana ambayo huchezwa kwenye jua kali amepata changamoto zozote, basi tambua huyo alikuwa na matatizo mengine ya kiafya mwilini mwake, ila tofauti na hapo hakuna athari zinazoweza kumpata.”
Dk Amina amesema kwa mechi zinazochezwa katika jua kali madaktari hushauriana na waamuzi kuweka muda maalumu wa kupumzika kwenye vipindi vyote viwili ‘cooling break’ ili kutoa nafasi kwa wachezaji kunywa maji kutokana na jasho linalowatoka.
“Suala la kucheza kwenye viwanja vyenye nyasi bandia katika jua kali athari zake zinazoweza kutokea ni majeraha madogo madogo ambayo husababishwa sana na aina ya viatu ambavyo mchezaji anatumia kutokana na kuungua miguu japo sio kwa wote,” amesema.
Daktari wa Fountain Gate, Shaaban Shija amesema kucheza katika jua kali na uwanja ambao ni wa nyasi bandia mchezaji anachopaswa kuzingatia ni kutotumia viatu vyenye meno ya chuma, kwa sababu inaweza kumsababishia majeraha mbalimbali.
“Shida iliyopo kuna baadhi ya wachezaji hawana uelewa wa jinsi ya kutumia viatu kutokana na aina ya mazingira yenyewe, ndio maana wengi wao wanakutana na majeraha ambayo unaweza kusema ni ya kujitakia kwa sababu hawafuati taratibu husika,” amesema daktari huyo.
Wakati hali ikiwa hivyo msimu wa 2024-2025, kwa upande wa msimu huu 2025-2026, ratiba ya Ligi Kuu Bara inaonyesha timu za Mashujaa, Tanzania Prisons, KMC na Pamba Jiji zitakuwa na mechi nyingi saa 8:00 mchana kipindi cha jua kali ambapo kila moja ikiwa nazo sita.
WAMILIKI WA VIWANJA
Hawa wanakabiliwa na gharama kubwa za matengenezo ya viwanja kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mvua kubwa na mafuriko huharibu viwanja, na joto kali huharibu nyasi za viwanja, hivyo kuongeza gharama za uendeshaji.
Joto kali na ukame husababisha nyasi za viwanja kukauka na kuwa ngumu, hali inayoongeza hatari ya majeraha kwa wachezaji. Mvua kubwa pia huharibu miundombinu ya viwanja, na hivyo kuathiri ubora wa mchezo.
Meneja wa Uwanja wa Jamhuri uliopo Morogoro ambao unamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Reuben Simkoko, amesema ni gharama kubwa kuutunza uwanja hasa kipindi cha kiangazi kulinganisha na wakati wa mvua nyingi.
Amesema licha ya changamoto hiyo, anachoshukuru ni kwamba ujio wa michuano ya AFCON 2027 itaokoa jahazi katika kuufanya uwanja anaousimamia kuwa bora tofauti na sasa ambapo anakumbana na changamoto nyingi za utunzaji hasa kipindi cha jua kali.
“Tangu nimeanza kuusimamia uwanja huu ni takribani miaka saba au nane imefika, ni gharama kubwa sana kuutunza uwanja.
“Unajua kwa sasa majani yanayotakiwa ni haya ya kawaida sio bandia, hivyo lazima uwe makini katika umwagiliaji.
“Kwa mfano hivi sasa tunakwenda kipindi cha kiangazi, inatakiwa wakati wote kiwe kibichi. Wakati wa kumwagilia haijalishi kwa siku umwagilie mara ngapi, bali wingi wa maji ndiyo utakupa majibu sahihi.
“Tunapata changamoto sana kipindi cha kiangazi kwa sababu jua huwa linatuzidia tofauti na wakati wa mvua
“Ukiangalia kiwanja chetu hiki majani yana muda mrefu, lakini tunashukuru AFCON inakuja na kiwanja chetu kitafanyiwa maboresho kuwa bora zaidi ya hapa.
“Morogoro imetajwa kuwa miongoni mwa mikoa ya utalii hapa nchini, ukiangalia mlima wa Uluguru ni sehemu nzuri ya utalii, sasa kama kiwanja chetu kikiwa bora basi tutapata namna nyingi sana ya kupata mashindano hapa.
“Ukiangalia mbuga ya Mikumi ipo karibu, tuna SGR kwamba mtu anaweza kulala hoteli ya nyota tano Dar es Salaam kisha akaja kucheza mechi hapa na kurudi.”
Meneja wa Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam, Daniel Madenyeka, amesema kuwa licha ya uwanja huo kuwa wa nyasi bandia, bado unahitaji matunzo ya gharama kubwa na ya kitaalamu ili kuendelea kuwa katika hali bora kwa matumizi ya mechi na mazoezi.
Madenyeka amesema kuna dhana potofu miongoni mwa wadau wa soka kuwa nyasi bandia hazihitaji matunzo ya mara kwa mara, jambo ambalo si sahihi.
“Watu wengi hufikiri kuwa nyasi bandia hazihitaji matunzo, lakini ukweli ni kwamba zinahitaji usafi wa kila siku, ukaguzi wa kiufundi mara kwa mara, na matengenezo ya sehemu zinazoharibika. Muda mwingine tunalazimika kuosha uso wa kuchezea kwa maji na dawa maalum ili kuondoa vumbi na taka ndogo ndogo,” amesema Madenyeka.
Ameongeza: “Kinachoharibu zaidi nyasi hizi ni jua kali la Dar es Salaam. Linachoma sana, na kama huna vifaa vya kupooza au kufunika baadhi ya maeneo kwa muda, uso wa uwanja unaweza kuchoka mapema.”
Meneja wa Uwanja wa Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar es Salaam, Ashrafu Omar Said, amesema uwanja unahitaji uangalizi wa karibu kila siku ili kuhakikisha unakuwa katika hali nzuri kwa ajili ya matumizi ya mechi, jambo ambalo linahitaji rasilimali za kutosha.
“Kuna wakati pampu za maji zinaharibika ghafla, mashine za kukatia majani hazifanyi kazi ipasavyo na zinahitaji matengenezo ya mara kwa mara. Hayo yote yanahitaji fedha, lakini pia muda na nguvu kazi,” amesema.
“Tunajitahidi kwa kiwango kikubwa kuhakikisha uwanja huu hauchafui jina la JKT. Tunauweka katika hali bora kadri ya uwezo wetu,” amesisitiza.
Meneja wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara, Jackson Mwendwa amesema ushirikiano ambao amekuwa akipata kutoka kwa viongozi mkoani humo pamoja na timu ya Fountain Gate, imemfanya kuwa na kazi nyepesi ya kuhaikikisha uwanja huo unakuwa kwenye kiwango kizuri. “Changamoto kubwa huwa wakati wa kiangazi, lakini jambo la kushuruku ni kwamba binafsi nimekuwa nikipata mahitaji yote ya msingi kuhakikisha eneo la kuchezea linakuwa na viwango ambavyo vinahitajika,” amesema.
ITAENDELEA KESHO
Makala hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation. Kama una maoni tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917