Kinachomkwamisha Salamba hiki hapa

Kinachomkwamisha Salamba hiki hapa

Muktasari:

ADAM Salamba (21), tangu arejee nchini Julai, mwaka jana akitokea nchini Kuwait alikokuwa anacheza timu ya Al-Jahra hajaonekana kuwa na mikikimikiki uwanjani akiwa na timu yake mpya ya Namungo FC.

ADAM Salamba (21), tangu arejee nchini Julai, mwaka jana akitokea nchini Kuwait alikokuwa anacheza timu ya Al-Jahra hajaonekana kuwa na mikikimikiki uwanjani akiwa na timu yake mpya ya Namungo FC.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na Salamba kujua sababu inayomkalisha benchi, tofauti na matarajio ya wengi ambao wanaamini angekuwa anaanza kikosi cha kwanza katika timu hiyo.

Salamba anafichua kilicho nyuma ya kukaa kwake benchi kuwa ni sababu iliyomfanya arejee Tanzania na kushindwa kuendelea na soka la kulipwa nchini Kuwait.

Anafunguka kuwa ugonjwa wa covid 19 nchini Kuwait uliingia Februari, mwaka jana na tangu hapo hazikuruhusiwa shughuli za mikusanyiko, hivyo alikuwa anafanya mazoezi mepesi ndani kwake, jambo lililomfanya aongezeka uzito.

“Nilikaa ndani kuanzia Februari mpaka Juni - Julai nikadandia ndege ya watalii kuja Dar, hivyo sikuwa na muda wa kufanya mazoezi ya kujiweka fiti, nimeanza kujifua kisawasawa nikiwa na Namungo baada ya kunisajili,” anasema na kuongeza kuwa:

“Mwili wangu ulikuwa mzito kutokana na kuwa na kilo 85 ambazo zilikuwa zinanisababisha usiwe na maamuzi ya haraka, nimepambana sasa nina 79, lakini natakiwa kupunguza mpaka zifike 75.”

Sababu ya pili anayoitaja Salamba inayomfanya akae benchi ni majeraha yaliyotokana na kujilazimisha kucheza kwa kutumia nguvu ilimradi tu aonekane ana msaada kwa timu, lakini matokeo yake alijikuta anaambulia kuumia.

“Mwili ulikuwa haujafunguka kucheza kutokana na kukaa kwa muda mrefu bila kucheza kwa sababu ya tatizo la covid 19, kwani ligi Kuwait ilifutwa tofauti na Tanzania ambako iliendelea na ndio maana wengi ambao tulikuwa tunacheza nje hatuwa na mwanzo mzuri katika timu zilizotuajiri,” anasema.

Anaeleza kwamba kwa sasa mwili wake unaimarika, hivyo anatarajia kutoa mchango wake ndani ya timu hiyo, ili uongozi uliomsajili ufaidi huduma yake kama walivyotarajia wakati wanampa ajira.

“Hakuna mchezaji ambaye anaweza akajisikia vizuri bila kucheza, ndicho kilichonitokea na mimi, lakini nilikuwa najipa moyo, ingawa wapo wanaonipa na mimi nikikaza kujituma, lakini pia hawakosekani wanaonikejeli.”

Mbali na hilo anaeleza kwamba ndoto zake za kucheza nje zipo palepale akitaja sababu iliyomkwamisha kwamba nchi ambazo alipata dili bado katikati ya mlipuko wa ugonjwa wa corona.

“Covid 19 imeharibu sana mipango ya wengi na sio wanasoka pekee, kama Mungu atasaidia hali ikatengamaa katika nchi hizo basi nitakwenda kucheza ikiwemo Kuwait yenyewe.”

Wakati Salamba yupo Kuwait aliwahi kuzungumzia suala la pesa kutokuwa tatizo kwake kutokana na mkwanja aliokuwa analipwa na klabu yake na je vipi aliporejea nchi?

Mchezaji huyo anasema jambo hilo kwake sio tatizo kwa kuwa anachokipata Namungo kinakidhi mahitaji yake na ana uwezo wa kufanya vitu vya kimaendeleo kama alivyokuwa nchini Kuwait.

“Napata kinachonitosheleza, kwa hilo nashukuru Mungu na ipo siku ninachokifanya cha kimaendeleo nikiwa na Namungo kikikamilika nitakuita uone, tuombea uzima,” anasema mshambuliaji huyo.

Salamba alijiunga na Al-Jahra ya Kuwait 2019 akitokea Namungo FC ambako alipelekwa na Simba kwa mkopo, lakini baada ya nchi hiyo kukumbwa na corona alivunja mkataba wa miaka mitatu ambao ulibakia na kurejea nchini.